Obama- Afghanistan | Matukio ya Kisiasa | DW | 27.10.2009
  1. Inhalt
  2. Navigation
  3. Weitere Inhalte
  4. Metanavigation
  5. Suche
  6. Choose from 30 Languages
Matangazo

Matukio ya Kisiasa

Obama- Afghanistan

"Sitaharakisha kutuma majeshi vitani."-Obama.

Obama na Gen. Stanley McChrystal .

Obama na Gen. Stanley McChrystal .

Rais Barack Obama wa Marekani ,akiwakaripikia vikali wakosoaji wake wanao mtuhumu kusitasita kuamua kupeleka vikosi zaidi nchini Afghanistan,aliapa jana kuwa, hataharakisha uamuzi wa kuwapeleka askari wa kimarekani vitani bila ya kwanza kupuima kila kitu sawa sawa.

Rais Hamid Karzai wa Afghanistan amelikataa dai la mpinzani wake Abdullah Abdullah la kumtimua Kiongozi mkuu wa Tume ya Uchaguzi kabla ya duru yao ya pili ya uchaguzi wa rais. Upinzani unaituhumu Tume hiyo kuvuruga mambo na kufanya mizengwe.

Rais Obama akikihutubia kikosi cha wanamaji wa Marekani Jacksonville, siku ile ile wanajeshi 14 wa Marerkani wameuwawa nchini Afghanistan,aliapa jana kuwa, hataachia kuharakishwa kupitisha uamuzi wa kupeleka majeshi vitani.Alisema:

"Sitaharakisha kupitisha uamuzi mgumu wa kuwapeleka nyinyi vitani."

Rais Obama anazingatia iwapo afuate ushauri wa amirijeshi wake mkuu nchini Afghanistan, Jamadari Stanley McChrystal, anadai kupelekwa nchini Afghanistan alao askari 40.000 zaidi .

Ni wiki iliopita tu, pale Ikulu mjini Washington, ilipolikanusha shtaka la makamo rais wa zamani enzi ya utawala wa George Bush, Dick Cheney, kuwa Obama anayumbayumba juu ya mkakati wa kupeleka Afghanistan wanajeshi zaidi.

Rais Obama akawaambia wanamaji hao huko Jacksonville :

"Sitahatarisha maisha yenu isipokuwa imelazimika kufanya hivyo."

Rais Obama akaongeza:

"Na ikilazimika ,tutakuwa nyuma yenu kikamilifu,kwavile, mnastahiki mkakati barabara,ujumbe wazi na shabaha iliofafanuliwa pamoja na silaha mnazohitaji kutimiza jukumu mliopewa."

Wiki iliopita,uchunguzi wa maoni nchini Marekani, ulionesha kuwa , wananchi hawaungi-mkono tena kwa dhati vita vya Afghanistan na wanachama wa chama cha rais Obama cha Democratic party, wamegawika iwapo Marekani itume wanajeshi zaidi nchini Afghanistan au la.Kwani, Marekani wakati huu tayari ina askari 65.000 nchini Afghanistan,idadi ambayo inatazamiwa kupanda hadi askari 68,000 baadae mwaka huu.

Na nchini Afghanistan kwenyewe, mvutano kabla ya duru ya pili ya uchaguzi wa rais unazidi kupambamoto kati ya rais Hamid Karzai na mpinzani wake Abdullah Abdullah.

Rais Karzai amelipinga kabisa dai la Abdullah kuwa mkuu wa Tume ya uchaguzi atimuliwe kwavile, ameelemea upande wa rais.Abdullah amedai pia mawaziri 3 katika Baraza la Karzai wasimamishwe kazi hadi duru yao ya pili ya uchaguzi imepita.

Mwandishi: Ramadhan Ali /RTRE

Mhariri: Abdul-Rahman

Matangazo

Unaweza kusikiliza matangazo yetu hapa

Kusikiliza matangazo ya Idhaa ya Kiswahili ya DW, tafadhali bonyeza alama ya spika ya masikioni hapo chini, na kuwasiliana nasi, tafadhali tuandikie moja kwa moja kupitia: kiswahili@dw.com