1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Ntaganda : Mahakama ya ICC yaunga mkono hukumu ya mwanzo

Saleh Mwanamilongo
30 Machi 2021

Mahakama ya kimataifa inayo shughulikia kesi za uhalifu wa kivita ICC imeendelea kushikilia mashtaka ya uhalifu wa kivita na hukumu ya miaka 30 dhidi ya Bosco Ntaganda.

https://p.dw.com/p/3rOl7
Niederlande | Prozess Dominic Ongwen | Internationaler Strafgerichtshof in Den Haag
Picha: ICC-CPI/REUTERS

Majaji wa mahakama ya Kimataifa ya Uhalifu, ICC hii leo Jumanne wametupilia mbali rufaa iliyowasilishwa na mbabe wa kivita wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo ambaye pia ni kiongozi wa waasi Bosco Ntaganda, kupinga hukumu ya kifungo cha miaka 30 aliyopewa mnamo mwaka 2019. 

Majaji wa mahakama ya rufaa wamesema hawakuona kosa lolote kwenye hukumu ya iliyotolewa awali na majaji wa mahaka ya ICC. Kwa hiyo kesi ya rufaa imethibitisha hatia dhidi ya Bosco Ntaganda.

Hatia ya makosa makosa kumi na nane

Bosco Ntaganda,jenerali wa zamani wa jeshi la Congo
Bosco Ntaganda,jenerali wa zamani wa jeshi la CongoPicha: AFP/Getty Images/L. Healing

Ntaganda mwenye umri wa miaka 47 mzaliwa wa Rwanda aliyepewa jina la "Terminator", alihukumiwa na mahakama ya ICC ya mjini The Hague mnamo mwaka 2019 kifungo cha miaka 30 baada ya kupatikana na hatia ya makosa 18 ya uhalifu wa kivita na uhalifu dhidi ya binadamu, pamoja na mauaji,ubakaji na kutumia wanajeshi watoto. Ntaganda ni mtu wa kwanza aliyewahi kushtakiwa kwa kosa la kuwatumia watu kama watumwa wa kingono na mahakama hiyo ya kimataifa.

Mashtaka mengine ni pamoja na mauaji ya wanakijiji katika eneo lenye utajiri wa madini la Ituri nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo. Majaji walisema Bosco Ntaganda alikuwa ndio kiongozi mkuu  wa kundi la waasi linalojiita umoja wa wakongomani wazalengo UCP na tawi lake la kijeshi la ukombozi wa Kongo, FPLC.Waasi hao wanalaumiwa kwa mauaji ya raia wapatao 800 katika jimbo la Ituri mashariki mwa Kongo.kundi hilo lilikuwa likiendesha hujuma zake katika eneo hilo mwaka 2002 hadi 2003.

Fidia ya dola milioni thalasini kwa wathirika

Mbabe wa zamani wa kivita nchini Congo, Bosco Ntaganda aliyehukumiwa kifungu cha miaka 30 na majaji wa ICC.
Mbabe wa zamani wa kivita nchini Congo, Bosco Ntaganda aliyehukumiwa kifungu cha miaka 30 na majaji wa ICC.Picha: Reuters/P. Dejong

Mwanzoni mwa mwezi Machi, ICC ilipitisha kiasi cha Dola milioni 30 kama fidia kwa wahanga wapatao 100,000 wa Bosco Ntaganda. Fedha hizo zitachangiwa na nchi wanachama, kwa sababu Ntaganda mwenyewe hana mali ya kuigharimia fidia hiyo.

Watu zaidi ya 60,000 wameuliwa tangu machafuko yalipozuka katika eneo hilo la Ituri mnamo mwaka 1999 kwa mujibu wa mashirika ya kutetea haki za binadamu, wakati waasi walipokabiliana kupigania udhibiti wa raslimali ya madini.

Ntaganda pia alishirikishwa na vuguvugu la M23, ambalo lilisaini mkataba wa amani na serikali ya Congo mwaka 2013. Alijisalimisha mwenyewe kwa ubalozi wa Marekani katika mji mkuu wa Rwanda, Kigali, mwaka 2013 baada ya kuepuka mitego ya kumkamata kwa miaka saba.