1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Nkunda awafurusha MaiMai kutoka Kiwanja

Kalyango Siraj7 Novemba 2008

Inadaiwa vijana wake waliwauwa kinyama raia 20

https://p.dw.com/p/Fp7l
Generali Laurent Nkunda kiongozi wa tawi la kijeshi la chama cha CNDP (Congress Nationale pour la Defense du Peuple)Picha: picture-alliance/ dpa

Mapigano kati ya vikosi vya waasi wa kitutsi dhidi ya wanamgambo wanaoegemea upande wa serikali katika Jamhuri ya Kidemokrasi ya Kongo yamekuwa yakiendelea mashariki mwa nchi hiyo huku kukiwa na taarifa kuwa waasi wa kitutsi wanadaiwa kutekeleza mauaji ya kiholela katika eneo wanalodhibiti.

Mkutano wa kikanda kushughulikia hali ya mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasi ya Kongo ukiwa unaendelea mjini Nairobi nchini Kenya, hali katika eneo lenyewe ni ya wasiwasi.

Inasemekana kuwa waasi watiifu kwa Generali Muasi Laurent Nkunda wamekuwa wakipigana dhidi ya wapiganaji wa MaiMai-ambao ni wanamgambo ambao ni watiifu kwa serikali ya Kinshasa. Inaarifiwa kuwa wapiganaji wa Nkunda walifaulu kuwafurusha wanamgambo wa Maimai kutoka mji wa Kiwanja unaopatikana mashariki mwa nchi hiyo lakini baada ya mapigano makali yaliyodumu siku mbili.

Kuna taarifa kuwa wapiganaji wa Nkunda, wakiwa katika shughuli za kuwafurusha Maimai kutoka mji wa Kiwanja, waliwaua kiholela raia kadhaa.

Mashirika ya habari yanaripoti kuwa takriban watu 20 waliuawa wakiwa majumbani mwao. Shirika linalotetea haki za binadamu la Amnesty International linasema kuwa hayo ni mauji ya halaiki.

Serikali ya jamhuri ya Kidemokrasi ya Kongo inawalaumu wanajeshi wa kikosi cha Umoja wa Mataifa kinacholinda amani nchini humo cha MONUC kwa kushindwa kuwalinda raia wa nchi hiyo. Msemaji wa rais Joseph Kabila amenukuliwa kusema kuwa watu wanauawa kinyama na MONUC inashindwa kuchukua hatua madhubuti.

Umoja wa Mataifa unasema unachunguza taarifa za mauaji hayo. Yeye Generali Nkunda anasema kuwa vijana wake waliwashambulia tu wanamgambo wanaoiunga mkono serikali ya Kinshasa ambao walikuwa wamejihami na silaha.

Lakini walioshuhudia mauaji hayo wanasema vingine .Wanadai kuwa waliouawa ni raia wa kawaida ambao hawakuwa na silaha.Wanaongeza kuwa walikuwa wakiondolewa majumbani mwao na watu waliokuwa na silaha na kuwapiga risasi.Mama mmoja amewambia maripota katika mji huo kuwa,mume wake nae aliuawa pamoja na watu wengine wanne na miili yao ilikuwa katika chumba kimoja katika nyumba yake.

Serikali ya Kinshasa inamchukulia Nkunda kama gaidi. Nkunda anadai kuwa yeye anapigana kulinda maslahi ya Watutsi wenzake dhidi ya mashambulizi ya waasi wa kihutu kutoka Rwanda ambao wamejificha katika misitu ya Kongo tangu mauaji ya halaiki ya mwaka wa 1994 nchini Rwanda.

Mkutano wa Nairobi unajaribu kutafuta ufumbuzi wa mzozo huo.Nkunda ambae hakuhudhiria mkutano huo ameiambia DW kuwa anasubiri kuona kitakachofuata.

Serikali ya Kinshasa imekataa kuzungumza nae na badala yake inapendelea kuzungumza na serikali ya Kigali inayodai kuwa inampa msaada wa hali na mali.

Kwa upande wake rais wa Rwanda Paul Kagame ameilaumu jamii ya kimataifa kwa kushindwa kushughulikia anachosema ni chanzo cha mgogoro huo,mbali na kumimina madola mengi katika eneo hilo'.Yeye anasema kuwa kiini cha mzozo huo ni kile alichoita 'udhaifu wa utawala wa Kinshasa 'ambao umeshindwa kuwapokonya silaha waasi wa kihutu.

Na kwa mda huohuo kuna taarifa kuwa wanamgambo wa MaiMai wanaripotiwa kumteka nyara mwandishi habari wa Kibeligiji ambae alikuwa anafanyia kazi gazeti la Ujerumani.Hakuna taarifa zaidi kwa sasa kuhusu kisa hicho.