Njama mpya ya mapinduzi Malawi yazusha mashaka | Matukio ya Kisiasa | DW | 22.05.2008
  1. Inhalt
  2. Navigation
  3. Weitere Inhalte
  4. Metanavigation
  5. Suche
  6. Choose from 30 Languages
Matangazo

Matukio ya Kisiasa

Njama mpya ya mapinduzi Malawi yazusha mashaka

Malawi iliyotangaza kuwa imefanikiwa kuzuia njama ya nne ya kutaka kuipindua serikali,imezusha mashaka kuhusu wasiwasi wa serikali,unaozozidi kuongezeka.

Rais wa Malawi Bingu wa Mutharika amesifiwa kwa mageuzi yaliyochangia kukuza uchumi wa nchi hiyo kila mwaka kwa asilimia 7 tangu miaka mitatu iliyopita na nchi yake yenye wakazi milioni 12 kupunguziwa deni lake kwa mabilioni ya Dola.Lakini juma lililopita,walipokamatwa wanachama waandamizi wa upinzani kuhusika na tuhumu za njama hiyo mpya ya mapinduzi,majadiliano kati ya serikali na upinzani yalikaribia kuvunjika na hali mbaya ya kisiasa inayomuandama Rais wa Mutharika ndio imezidi kutibuka.

Miongoni mwa wale waliokamatwa safari hii ni majemadari watatu,maafisa waandamizi wawili wa polisi waliostaafu na wanachama wanne wa chama cha upinzani - United Democratic Front -UDF.Vile vile imetolewa waranti ya kumkamata rais wa zamani Bakili Muluzi alieteuliwa na UDF kugombea urais katika uchaguzi wa mwakani lakini hivi sasa yupo nje ya nchi.

Kwa kweli utawala wa Rais wa-Mutharika umekumbwa na matatizo tangu mwanasiasa huyo kushika madaraka mwaka 2004,baada ya kushinda uchaguzi ulioingia dosari kwa sababu ya machafuko na tuhuma za udanganyifu wa kura.

Uamuzi wa kiongozi huyo kujitoa chama cha UDF kilichomteua kugombea uchaguzi,ni kiini cha mgogoro wa kisiasa unaoendelea hivi sasa kuhusika na kifungu kimoja katika katiba ya nchi.Kuambatana na kifungu hicho wabunge hawana ruhusa ya kutoka chama kimoja na kuingia kingine.Majadiliano yanayofanywa kati ya Rais na upande wa upinzani kuhusu wabunge 70 waliohamia chama chake cha Democratic Progressive Party DPP yamekwama.

Mzozo huo hivi karibuni ulisababisha mgomo wa siku tano wa wabunge wa upinzani na vikao vya bunge kuahirishwa.Kwa mara nyingine tena mzozo huo huenda ukachelewesha midahalo muhimu kuhusu bajeti ya taifa na hatua za kuchukuliwa kuambatana na mwongozo wa wafadhili wake.

Kiuchumi kuna matumaini katika nchi hiyo inayotegemea zaidi kilimo,hasa mauzo ya nje ya tumbaku.Shirika la Fedha la Kimataifa-IMF limetathmini kuwa mwaka huu mauzo hayo ya yataongezeka kwa asilimia 7.

Lakini mizozo ya kisiasa inagubika mafanikio kama hayo.Mwaka jana upande wa upinzani ulichukua miezi mitano kabla ya kuidhinisha bajeti ya serikali ya Dola bilioni moja nukta mbili kwa mwaka wa fedha wa 2007 na 2008.

Safari hii vyama vya upinzani UDF na Malawi Congress Party vimeapa kuizuia bajeti mpya ikiwa spika wa bunge hatowatoa wabunge wa upunzani waliojiunga na chama cha rais - DPP.

Ikiwa vyama hivyo vitafanikiwa kuwatoa bungeni wafuasi wa rais,basi vitakuwa na wingi wa kuweza kupitisha kura ya kutokuwa na imani na serikali na hata kumshtaki rais.Lakini upinzani unasema,hauna mpango wa kufanya hivyo.Hata hivyo,ikiwa bajeti haitopitishwa,basi msaada wa wafadhili unaotegemewa sana na serikali kugharimia huduma za kijamii,utakuwa hatarini.

Matangazo

Unaweza kusikiliza matangazo yetu hapa

Kusikiliza matangazo ya Idhaa ya Kiswahili ya DW, tafadhali bonyeza alama ya spika ya masikioni hapo chini, na kuwasiliana nasi, tafadhali tuandikie moja kwa moja kupitia: kiswahili@dw.com