Njaa yapungua Somalia , lakini Magonjwa yasambaa | Masuala ya Jamii | DW | 19.11.2011
  1. Inhalt
  2. Navigation
  3. Weitere Inhalte
  4. Metanavigation
  5. Suche
  6. Choose from 30 Languages
Matangazo

Masuala ya Jamii

Njaa yapungua Somalia , lakini Magonjwa yasambaa

Madaktari katika mji mkuu Mogadishu wanaonya wahanga wa njaa wanakabiliwa na magonjwa, wakati hali inaonekana ni mbaya tayari kwa magonjwa kuripuka.

Somalia Mogadischu Lebensmittel gestohlene Hilfsgüter Markt

misaada iliotolewa imeshindwa kufika kwa baadahi ya wahitaji.

Waliolazimika kukimbilia kwenye makambi baada ya kuyahama makaazi yao,wanasema misaada katika baadhi ya kambi imepungua mno au imesita kabisa.

Daktari Abdi Ahmed ambaye ni mkuu wa kikundi cha madaktari wa Kisomali wanaojitolea wakiwasaidia wahanga wa baa la njaa wanaoishi katika makambi nje ya mji mkuu-Mogadishu anasema hali ya usafi ikiwa ni pamoja na uhaba wa vyoo katika kambi hizo ni moja wapo ya mambo yanayozusha wasiwasi na kuwa watu wengi wanashindwa kupata maji safi.

"Hali katika kambi hizo imefikia kiwango cha kuwa wakati wowote ule, yanaweza kuzuka magonjwa yanayouawa," amesema daktari huyo huku akiitaka serikali ya Somalia ilizingatie kwa makini onyo lao.

Ameongeza tayari kuna watu waliotawanyika baada ya kuyakimbia makaazi yao na sasa wanaishi katika kambi hizo walioambukizwa magonjwa mbali mbali kama matatizo ya kupumuwa,surua, malari na homa ya uti wa mgongo. Amesisitiza kwa hivyo kwamba ,Uboreshaji wa usafi ni muhimu katika kuepusha kuzuka kwa magonjwa.

Kambi ya Sigale nje ya Mogadishu na ambayo ndiyo pekee katika sehemu hiyo, ina wakimbizi zaidi ya 3,0000 na hawajapata msaada wowote tangu mwezi Agosti. Mkuu wa kambi hiyo Mohamed Hassan Sheikh Abdi amesema shehena ya mwisho ya msaada iliwasili kambini humo wakati wa mwezi wa Ramadhani ikitoka Qatar na tangu wakati huo hakuna aliyefika na msaada wa aina yoyote.

Mapema asubuhi, akina mama na akina baba katika kambi hiyo huelekea mjini, kuomba chakula na misaada mengine na kurudi kambini jioni wakiwa na kile walichojaaliwa kukipata, ili kuwalisha watoto wao ambao hubakia siku nzima bila chakula.

Kwa mujibu wa Daktari Abdi, watu 10 na hasa watoto walio chini ya umri wa miaka mitano, wamekufa katika kambi ya Sigale tangu Septemba kwa sababu ya kuharisha na kifaduro.

Janga hilo nchini Somalia limesababishwa na ukame unaosemekana kuwa mbaya zaidi kuwahi kutokea Afrika mashariki kwa miaka 60 iliopita.

Mkurugenzi wa Shirika la misaada la Qatar nchini Somalia Duran Ahmed Farah ameliambia shirika la habari la IPS kwamba shirika lake limetoa msaada wa chakula kwa maelfu ya Wasomali na sasa linakusudia kuyatatua matatizo ya usafi na mengineyo yanayohusiana na afya katika makambi.

Akasema kwamba baada ya kwanza kujaribu kufanya kampeni ya kuokoa maisha kwa sababu watu walikuwa wakifariki kwa njaa na walitaka kupata chakula, hivi sasa wataanza kuwa na vikundi vya matabibu watakaohusika ana huduma za afya katika makambi.

Pamoja na hayo alisisitiza kwamba mahitaji makubwa yaliopo hayawezi kutimizwa katika kipindi kifupi.

Wakati huo huo shirika la misaada linalojulikana kama kituo cha kijamii cha Usmani, nalo limeanza mradi muhimu wa kuchimba visima katika kambi za wakimbizi hao wa ndani. Tayari vimeshachimbwa visima katika kambi za wilaya ya Hamar Weyne na Abdel Aziz .

Msemaji wa serikali ya Somalia Mohamed Abdullahi Arig, alisema serikali nayo inachukua juhudi kusaidia kuhakikisha unaepushwa uwezekano wa kuripuka magonjwa hatari kama kipindupindu katika kambi hizo za wakimbizi wa ndani. Lakini pamoja na kujizatiti kwa serikali, uwezo wake ni mdogo na hivyo akaitaka jumuiya ya kimataifa isaidie zaidi katika sekta hiyo.

Kwa upande wake Umoja wa mataifa unasema janga la njaa na ukame yanapungua nchini Somalia lakini watu 250,000 bado wanakabiliwa njaa kubwa.Taarifa ya Umoja wa mataifa ilisema njaa imepunguwa kidogo katika mikoa mitatu ya Bakool,Bay na Shabelle ya chini, lakini usalama wa chakula bado ni wa kiwango cha chini.

Juhudi za usambazaji misaada zinaendelea kukwamishwa katika baadhi ya maeneo yanayodhibitiwa na waasi wa Al-Shabaab wanaoendelea kupigana na serikali ya mpito, inayoungwa mkono na kikosi cha kusimamia amani cha Umoja wa Afrika.

Mwandishi:Mohammed Abdul-Rahman/IPS

Mhariri:Josephat Charo

Matangazo

Unaweza kusikiliza matangazo yetu hapa

Kusikiliza matangazo ya Idhaa ya Kiswahili ya DW, tafadhali bonyeza alama ya spika ya masikioni hapo chini, na kuwasiliana nasi, tafadhali tuandikie moja kwa moja kupitia: kiswahili@dw.com