1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Nipo tayari kumkabili Anthony Joshua, asema Fury

Bruce Amani
24 Februari 2020

Bondia Tyson Fury anasema anataraji kuwa Deontay Wilder atachukua uamuzi wa kuitisha marudiano ya pambano lao la heavyweight lakini yuko tayari kuvaana na Muingereza mwenzake Anthony Joshjua

https://p.dw.com/p/3YKJX
Boxen Deontay Wilder vs Tyson Fury
Picha: Reuters/S. Marcus

Bondia Tyson Fury anasema anataraji kuwa Deontay Wilder atachukua uamuzi wa kuitisha marudiano ya pambano lao la heavyweight lakini yuko tayari kuvaana na Muingereza mwenzake Anthony Joshjua kama Mmarekani huyo atakataa fursa hiyo.

Akizungumza baada ya ushindi wake wa raundi ya saba kwa kumrambisha sakafu Wilder mjini Las Vegas Jumamosi, Fury alionekana kuwa mwenye furaha kupambana na yeyote kati ya hao wawili "Faida ya vita vyetu imepatikana, nahitaji kufurahia ushindi huu. Deontay atahitaji muda kujiweka sawa kutokana na pigano hili lakini nna uhakika kuwa atataka marudio kwa sababu ni bondia mwenye ngumi nzito na wakati wowote anaweza kumbwaga mtu chini. Kwa hiyo nna uhakika atataka kufanya hilo tena na kama hatachukua fursa hiyo, basi hawa ndio ma promota na unajua kuwa chochote wanachotaka kufanya mimi nitakifurahia. Atakayekuja kwa hakika atapata kipigo hicho hicho.

Fury alinyakua mkanda wa WBC kwa mara ya pili kutoka kwa Wilder, ijapokuwa Joshua anaishikilia mikanda mingine ya kitengo hicho cha heavyweight ya IBF, WBA na WBO. Pigano la kwanza la Fury na Wilder la mwaka wa 2018 liliishia sare. Wolder sasa ana siku 30 kuamua kama atakubali kushuka ulingoni kwa mara ya tatu na Fury.