Nikol Pashinyan aonya juu ya ′Tsunami′ asipochaguliwa Armenia | Matukio ya Kisiasa | DW | 01.05.2018
  1. Inhalt
  2. Navigation
  3. Weitere Inhalte
  4. Metanavigation
  5. Suche
  6. Choose from 30 Languages

Matukio ya Kisiasa

Nikol Pashinyan aonya juu ya 'Tsunami' asipochaguliwa Armenia

Kiongozi wa upinzani wa Armenia, Nikol Pashinyan, amewataka wafuasi wake kulishinikiza bunge kumchagua yeye kuwa waziri mkuu mpya na kuonya juu ya "tsunami ya kisiasa" iwapo chama tawala kitakataa kuwaachia madaraka.

Pashinyan aliyeongoza maandamano ya karibu wiki mbili yaliyopelekea kiongozi wa muda mrefu wa nchi hiyo, Serzh Sarksyan, kujiuzulu uwaziri mkuu wiki iliyopita, ndiye mgombea pekee aliyeteuliwa kuchukuwa wadhifa huo wa waziri mkuu, lakini atahitaji uungaji mkono kutoka kwa bunge ambalo wengi wa wabunge ni wa kutoka chama tawala cha Sarksyan.

Pashniyan amelionya bunge la nchi hiyo dhidi ya uwezekano wa kutokea mgogoro mkubwa, endapo halitomchagua yeye kuwa waziri mkuu katika mchakato wa kupiga kura bungeni siku ya Jumanne.

Ameonya kwamba viongozi hao wasifanye kosa la kuutafsiri ukimya wa wananchi kuwa ni udhaifu kwa sababu hilo linaweza kuigeuza nchi hiyo kutumbikia katika kile alichokiita siasa za gharika ya Tsunami. Takriban wafuasi 20,000 wa Pashiyan wamemiminika katika mji mkuu Yerevan kumuunga mkono.

Proteste in Armenien (Reuters/G. Garanich)

Wafuasi wa Pashinyan wakisubiri nje ya bunge kusikia matokeo ya kura ya kumchaguwa waziri mkuu.

Akizungumza bungeni kabla ya kura hiyo ya kumteua rasmi waziri mkuu, Pashinyan amesema wanaoumuunga mkono Sarksyan katika chama tawala cha Republican hapaswi kuyapuuza matakwa ya Warmenia ya kutaka mageuzi na kuongeza kuwa mtu angedhani kufikia sasa wanasiasa hao wa Republican wangekuwa wameelewa kule upepo wa kisiasa unapovuma lakini ndiyo mwanzo wameanza mchezo wa paka na panya na wananchi.

Nguvu ya umma 

Sarksyan alikuwa rais wa Armenia kwa miaka 10 kabla ya kuteuliwa mwezi Machi mwaka huu kuwa waziri mkuu, jambo ambalo lilipingwa vikali na Warmenia waliomuona kama kiongozi anayetaka kung'angania madaraka.

Maelfu ya raia waliojitokeza kati kati ya mji mkuu Yerevan wamebeba bendera za Armenia huku wakisema Nikol ndiye waziri mkuu. Pashinyan ana uungwaji mkono wa vyama vya kisiasa ambavyo kwa jumla vina viti 47 katika bunge lenye wabunge 105. Anahitaji wingi wa kura ili kuidhinishwa kuwa waziri mkuu.

Iwapo atachuguliwa kuwa waziri mkuu, itaashiria mkondo mpya wa uongozi katika taifa hilo lililokuwa chini ya utawala wa Kisovieti ambalo limetawaliwa na tabaka moja la viongozi wale wale tangu miaka ya tisini.

Armenien Premierminister Karen Karapetyan (imago/ITAR-TASS/A. Geodakyan)

Kaimu waziri mkuu wa Armenia ambaye ndiye spika wa bunge la nchi hiyo Karen Karapetyan.

Armenia lenye idadi ya watu takriban milioni tatu linapakana na Uturuki na Iran na lina mzozo wa mipaka na Arzebaijan. Nchi hiyo ina mahusiano ya karibu mno na Urusi ambayo ina kambi kadhaa za kijeshi Armenia.

Maafisa wa Urusi wanafuatilia kwa karibu yanayojiri Armenia kuona kama siasa za nchi hiyo zitachukua mkondo wa Georgia na Ukraine ambako maandamano ya umma yalipelekea uongozi mpya wa viongozi ambao waliziondoa nchi zao kutoka uhusiano wa karibu na Urusi.

Pashinyan mwenye umri wa miaka 42, mhariri wa zamani wa gazeti moja nchini mwake amesema iwapo atachaguliwa kuwa waziri mkuu atadumisha uhusiano wa karibu na Urusi.

 

Mwandishi: Caro Robi/Reuters/Ap

Mhariri: Mohammed Khelef

Matangazo

Unaweza kusikiliza matangazo yetu hapa

Kusikiliza matangazo ya Idhaa ya Kiswahili ya DW, tafadhali bonyeza alama ya spika ya masikioni hapo chini, na kuwasiliana nasi, tafadhali tuandikie moja kwa moja kupitia: kiswahili@dw.com