1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Nigeria: Waandishi wa habari na wanaharakati wakamatwa

Zainab Aziz
21 Agosti 2018

Shirika la kutetea haki za binadamu la Human Rights Watch limelaani kukamatwa kwa waandishi habari na wanaharakati nchini Nigeria, limesema hali hiyo inaashiria hatari ya kubanwa kwa uhuru wa kutoa maoni.

https://p.dw.com/p/33SXY
Human Rights Watch Logo Symbolbild
Picha: Getty Images/AFP/J. Macdougall

Shirika la kutetea haki za binadamu la Human Rights Watch limesema mkasa mmoja umebainisha  kwamba mwandishi habari mmoja aliwekwa mahabusi na kutengwa na mahabusu wengine kwa muda wa karibu miaka miwili. Asasi hiyo pia imesema katika mkasa mwingine mahabusu mwingine  aliteswa. Mtafiti wa masuala ya haki za binadamu kwenye shirika hilo Anietie Ewang amesema. Kuwakamata maripota kwa sababu tu ya kufanya kazi yao ya kuwapa habari wananchi ni jambo linalotoa ujumbe wa kuchoma roho nchini Nigeria. Wahusika wanapaswa kuacha  mara moja kuwaandama waandishi wa habari ili kuhakikisha kwamba wanafanya kazi zao bila kuhofia.

Wiki iliyopita mahakama moja ya mjini Abuja ilimwachia huru bila ya masharti yoyote mwandishi na mchapishaji wa jarida la kila wiki, Jones Abiri katika jimbo la Bayelsa. Mwandishi huyo aliwekwa ndani kwa muda wa miaka zaidi ya miwili baada ya kukamatwa na maafisa wa idara ya usalama.

Idara hiyo ya usalama ilitoa tamko kudai kwamba mwandishi habari Abiri alikamatwa kwa sababu alikuwa analiongoza jeshi la kulikomboa jimbo la Delta, linalodaiwa kuendesha harakati za kujitenga. Hata hivyo kamati ya kutetea haki za waandishi wa habari imesema katika ripoti yake kuwa ndugu wa mwandishi huyo wanaamini kwamba kwa sababu za kukamatwa kwake zimetokana na kuandika makala ya utatanishi katika jarida la wiki.

Rais wa Nigeria Muhammadu Buhari
Rais wa Nigeria Muhammadu BuhariPicha: picture alliance/AP Photo/S. Aghaeze

Mwandishi huyo Abiri aliwekwa katika mahabusu na kutenganishwa na wafungwa wengine katika  sehemu ambayo haikujulikana, licha ya juhudi za wanasheria na chama cha waandishi wa habari za kutaka kuwasiliana naye. Hata hivyo kutokana na kampeni za wanaharakati wa mitandao ya kijamii na wanasheria mwandishi huyo alifunguliwa mashtaka ya vitisho vya kihalifu.Kesi yake itaanza kusikilizwa tarahe 5 mwezi ujao.

Mnamo mwaka 2010 shirika la kutetea haki za binadamu la Human Rights Watch liliorodhesha mikasa ya kukiukwa haki za binadamu nchini Nigeria ikiwa pamoja na kukamatwa kiholela na kinyume cha sheria kwa wanaharakati na waandishi wa habari.

Idara za usalama za serikali nchini Nigeria zimehusishwa na utumiaji vibaya wa madaraka na ukiukaji wa haki za binadamu. Mtafiti wa masuala ya haki za binadamu Anietie Ewang amesema mamlaka za Nigeria zinapaswa kuchukua hatua za haraka ili kukomesha hali ya kueneza hofu na kutishiwa na mashirika ya usalama, na badala yake kutoa mfano mzuri kwa kumuachia huru mwandishi Jones Abiri na wengine.

Mwandishi: Zainab Aziz/HWR Press Release

Mhariri: Josephat Charo