1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Nigeria: Ndoa za utotoni bado tatizo kubwa

Lilian Mtono
17 Januari 2022

Shirika la kimataifa la utetezi wa haki za binaadamu la Human Rights Watch limesema Nigeria kwa kiasi kikubwa bado inakiuka haki za wasichana kutokana na kusalia kuwa na kiwango cha juu cha ndoa za utotoni barani Afrika.

https://p.dw.com/p/45cp5
Weltspiegel 03.03.2021 | Nigeria Zamfara | Freilassung entführter Schulmädchen
Picha: Afolabi Sotunde/REUTERS

Shirika la kimataifa la utetezi wa haki za binaadamu la Human Rights Watch limesema kwenye ripoti yake kwamba Nigeria kwa kiasi kikubwa bado inakiuka haki za wasichana kutokana na kusalia kuwa na kiwango cha juu cha ndoa za utotoni barani Afrika licha ya taifa hilo kupitisha sheria ya haki za mtoto takriban miongo miwili iliyopita. 

Kulingana na ripoti ya shirika hilo la Human Rights Watch, ingawa sheria ya shirikisho nchini humo inayozungumzia Haki za Mtoto, CRA, 2003 inazuia ndoa za chini ya miaka 18 lakini katiba ya Nigeria bado ina vifungu vinavyokinzana na umri huo. Human Rights Watch aidha limesema majimbo yenye mifumo ya sheria za Kiislamu pia yameshindwa kutekeleza sheria hiyo.

Mkurugenzi wa shirika hilo kanda ya Afrika Mausi Segun amesema inasikitisha kuona kwa takriban miongo miwili tangu kupitishwa kwa sheria hiyo, wasichana wa Nigeria bado wanalazimishwa kuolewa.

Mwezi Agosti na Septemba mwaka jana, Human Rights Watch liliwahoji wasichana 16 walioolewa kati ya miaka 14 na 19 pamoja na wawakilishi katika mashirika manane ya kiraia yanayopigania kumaliza tatizo hilo pamoja na unyanyasaji wa kijinsia kwenye majimbo ya Imo na Kano.

Soma Zaidi:Unicef: Ndoa za utotoni zimepungua duniani 

Nigeria | Entführung hunderter Mädchen in Zamfara
Msichana wa Nigeria akiwa kwenye harakati za kimaisha. Wengi wa wasichana hawa wanakabiliwa na wasiwasi kuhusu kesho yao.Picha: Afolabi Sotunde/REUTERS

Umasikini, mila na desturi bado ni vichocheo vikubwa vya ndoa za mapema.

Kwenye mahojiano hayo liligundua, wasichana walioolewa hukosa haki za msingi za kupata elimu, makazi salama na kujiepusha na unyanyasaji. Lakini pia wasichana hao hawapati huduma muhimu za afya. Baadhi ya wasichana waliliambia shirika hilo kwamba waliwahi hata kujaribu kuwakimbia waume zao. Mmoja ya wasichana hao aliyeolewa akiwa na miaka 14 amesema alijaribu kutoroka mara sita katika kipindi cha miaka mitatu lakini kila alipotoroka, familia yake ilimrudisha kwa nguvu.

Familia za wasichana hawa huwalazimisha kuolewa wakiwa wadogo kutokana na sababu za kiimani na kimila lakini pia huogopa kutengwa na jamii iwapo watoto watapata mimba za mapema.

Jimbo la Imo kwa mfano lenye Wakristo wengi kusini mashariki mwa Nigeria lilipitisha sheria ya haki za mtoto mwaka 2004. Lakini ndoa hizo bado ni tatizo kubwa. Wasichana waliohojiwa walisema familia zimekuwa zikiwalazimisha kuolewa.

Kano, linalotawaliwa na Sharia, lina idadi kubwa ya ndoa hizo. Mwezi Februari bunge la jimbo lilipiga kura ya kupitisha sheria ya kumlinda mtoto lakini gavana Abdullahi Umar Ganduje bado hajiidhinisha. Kwenye jimbo hilo, Human Rigts Watch iligundua familia ndio huaanda ndoa bila ya kumshirikisha msichana juu ya muda na hata kumjua mwenza wake. Wasichana wenyewe wanasema ndoa huzingatia mila na hali ya umasikini wa familia zao.

Igawa baadhi ya familia huchukulia ndoa kama njia ya kupambana na umasikini, wasichana wanaoolewa wanasema hali yao ya kiuchumi huwa mbaya zaidi baada ya kuolewa, kiasi cha kukosa hata chakula.

Sikiliza Zaidi: 

Ndoa za mapema zapigwa marufuku Tanzania

Shirika hilo limesema, ili kupambana na tatizo hili kuna haja ya dharura kwa Nigeria kuzioanisha sheria zake ili kuendana na viwango vya kimataifa vya sheria ili kuwalina watoto. Limesema, sheria ya Haki za Mtoto inapaswa kupitishwa na kutekelezwa na majimbo lakini pia mamlaka za shirikisho zilizopitisha sheria hiyo zinapaswa kuwa na mpango madhubuti wa kuhakikisha utekelezaji mzuri wa sheria hiyo.

Soma Zaidi:Benki ya Dunia: Nchi zapoteza mabilioni ya mapato kwa ndoa za mapema 

Mashirika: HRW