Nigeria: Mwaka mmoja baada ya maandamo ya #EndSARS | Matukio ya Afrika | DW | 19.10.2021
  1. Inhalt
  2. Navigation
  3. Weitere Inhalte
  4. Metanavigation
  5. Suche
  6. Choose from 30 Languages
Matangazo

Matukio ya Afrika

Nigeria: Mwaka mmoja baada ya maandamo ya #EndSARS

Mwaka mmoja baada ya maandamano makubwa ya kupinga ukatili wa polisi Nigeria, watetezi wa haki za binaadamu wanasema visa vya ukatili vinaendelea nchini humo kutokana na serikali ya Nigeria kutowawajibisha wahusika.

Monsurat Ojuade alikuwa ametimiza umri wa miaka 18 wakati alipouawa na afisa wa polisi, dada yake Omolara alisema kwa sauti ya huzuni.

Habari za kifo chake, kilichotokea wakati wa uvamizi katika kitongoji cha Lagos mwezi uliopita, ziliwashtua wengi katika nchi hiyo yenye idadi kubwa ya watu barani Afrika na inayojiandaa kuadhimisha kumbukumbu ya mwaka mmoja ya EndSARS.

#EndSARS zilikuwa harakati za maandamano dhidi ya ukatili wa polisi uliotikisa miji mikubwa kusini mwa Nigeria, maandamano ambayo yalisitishwa baada ya Oktoba 20,2020, siku iliyoshuhudia ukandamizaji mkali dhidi ya waandamanaji wa amani katika lango la Lekki mjini Lagos, kitovu cha maandamano.

Soma pia: Wanajeshi Nigeria wafyatua risasi dhidi ya waandamanaji

Kwa vijana ambao walijiunga na maandamano hayo kwa mara ya kwanza katika miongo kadhaa, kifo cha Monsurat Ojuade ilikuwa ni ishara kuwa madai yao ya mabadiliko hayajasikilizwa na kwamba vitendo vya kutowawajibisha wahalifu na ufisadi bado vipo.

Afisa wa polisi aliyehusika na mauaji hayo alisimamishwa kazi na anakabiliwa na kesi ya mauaji lakini familia ya Ojuade inasema hatua zaidi zinahitajika. Wamesema pia kuwa, serikali haitoi mafunzo sahihi kwa polisi kwa kuwa, kama ingelikuwa hivyo, polisi hawezi kwenda kwenye lango la mtu na kuanza kufyatua risasi kiholela.

Nigeria Abuja | End Sars Proteste | Demonstranten

Waandamanaji wakiwa wamebeba bango wakati wa maandamano ya kushinikiza kuvunjwa kwa kikosi cha kupambana na ujambazi, SARS, mjini Abuja, Nigeria, Oktoba 19, 2020.

Harakati za maandamano za mwaka jana na zilizopewa jina "EndSARS2" katika mitandao ya kijamii, ilikuwa kwanza kampeni ya kukomesha vitendo vya unyang´anyi, mateso na mauaji vilivyokua vikifanywa na kikosi maalum cha kupambana na ujambazi cha Nigeria (SARS), baadae maandamano hayo yaligeuka na kuwa mapana zaidi ya kupinga utawala mbaya.

Soma pia: Amnesty: Waandamanaji 12 wameuwawa Nigeria

Serikali ililazimika kukivunja kikosi hicho na kuahidi mageuzi. Lakini vijana wa nchi hiyo hawakuridhika na hilo na waliendelea kuandamana hadi kulipotokea ukandamizwaji wa huko Lekki.

'Mabadiliko hewa'

Mwaka mmoja baadae, wengi wanajiuliza ikiwa juhudi zao zilikua na athari yoyote. Damian Ugwu, mtafiti wa shirika la Amnesty International anasema hakuna kilichobadilika, Kikosi cha SARS kinaweza kuwa kilivunjwa lakini kulikuwepo tu na mabadiliko hewa.

Ugwu ameendelea kusema kuwa vitu vyote ambavyo watu walilalamikia kama unyang´anyi, mauaji ya kiholela, mateso, unyanyasaji, bado vipo ndani ya jeshi la polisi na ingawa mafunzo yalitolewa, hakukuwa na marekebisho ya kina na pia vikosi vya usalama havipewi uwezo wa kutosha huku maafisa wakiendelea kulipwa vibaya.

Soma pia: Rais wa Nigeria aacha mauwaji ya watu 12 nje ya hotuba yake

Unyanyasaji wa maafisa wa polisi mafisadi katika mitaa ya Lagos umeanza tena, ni lazima uwape pesa, la sivyo utakua na matatizo nao, alisema dereva teksi mmoja aliefahamika kwa jina la Femi. Nje ya mji mkuu wa kiuchumi, mwandishi wa habari wa AFP alishuhudia maafisa wengine wakiwa na mavazi ya kiraia wakitumia bakora au mijeledi kuwatisha madereva.

Nigeria Abuja | End Sars Proteste | Demonstranten

Waandamanaji wanaopinga ukatili wa polisi nchini Nigeria wakiwa na mabango ya kudai kukomeshwa kwa ukatili wa kikosi cha kupambana na uhalifu cha SARS.

Rinu Oduala, mmoja wa watu mashuhuri wa harakati ya EndSARS alisema, baada ya maandamano ya mwaka jana, ghasia za polisi mwanzoni zilipungua lakini katika miezi ya hivi karibuni zilianza tena kwa ukatili zaidi kuliko hapo awali.

Soma pia: Polisi Nigeria wako katika hali ya tahadhari

Kijana huyo wa miaka 22 ameanzisha Connect Hub, shirika lisilo la kiserikali ambalo linaorodhesha vurugu za polisi ili kuuonyesha ulimwengu ni kwa nini wanapambana. Oduala amesema kwa muda wa mwezi mmoja, karibu kesi 100 za ukatili wa polisi tayari zimeripotiwa. Lakini serikali haijatoa kauli yoyote juu ya madai hayo.

Kama ilivyo kwa Wanaigeria wengi, Agboola Onileowo mwenye umri wa miaka 29 amesema kamwe hatosahau usiku wa Oktoba 20 mwaka jana wakati maafisa wa usalama walipowafyatulia risasi maelfu ya waandamanaji mjini Lekki ambapo kulingana na shirika la Amnesty International, watu 10 waliuawa. Onileowo amesema hatarajii chochote kutoka kwa serikali na kwamba Mungu atawaadhibu waliohusika na mauaji hayo.

Chanzo: AFPE