1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Ni siku ya hukumu Marekani

Iddi Ismail Ssessanga/rtre, ape, afpe6 Novemba 2012

Raia wa Marekani wanapiga kura leo kuchagua kiongozi mpya wa taifa hilo lenye nguvu zaidi duniani . Rais Barack Obama na mpinzani wake kutoka chama cha Republican Mitt Romney walitoa hoja zao za mwisho kwa wapiga kura.

https://p.dw.com/p/16dNj
Wapiga kura kumi wa kwanza katika kijiji kidogo cha Doxville Notch, New Hampshire, wakisubiri kupiga kura yao muda mfupi baada ya saa sita usiku.
Wapiga kura kumi wa kwanza katika kijiji kidogo cha Doxville Notch, New Hampshire, wakisubiri kupiga kura yao muda mfupi baada ya saa sita usiku.Picha: Reuters

Rais Barack Obama alimalizia kampeni zake jimboni Iowa ambako ndiko alikoanzia harakati zake za kuingia ikulu ya White House miaka minne iliyopita, akiwaomba wakaazi wa jimbon hilo wamsaidie kukamilisha kile walichokianzisha miaka minne iliyopita. "Nimekuja tana Iowa kuomba ridhaa yenu kwa mara ya mwisho, nimekuja kuwaomba mnisaidie kukamilisha kile tulichokianzisha, kwa sababu hapa ndipo vuguvugu letu lilikoanzia."

Rais Barack Obama akimkumbatia mkewe Michelle kabla ya kuhutubia mkutano wake wa mwisho mjini Des Moines, Iowa Jumatatu usiku.
Rais Barack Obama akimkumbatia mkewe Michelle kabla ya kuhutubia mkutano wake wa mwisho mjini Des Moines, Iowa Jumatatu usiku.Picha: Reuters

Bruce Springsteen, Jay-Z wato burudani

Akisindikizwa na wanamuziki maarufu Bruce Springsteen na Jay-Z Obama alijitahidi kutetea rekodi yake katika miaka minne iliyopita. "Mnaweza kuwa hamkubaliani na kila maamuzi niliyoyafanya, mnaweza kuwa mmekatishwa tamaa na kasi ya mabadiliko niliyowaahidi huko nyuma, lakini mnajua kwamba namaanisha ninachosema na nasema ninachomaanisha," alisema Obama.

Hoja ya rais Obama katika dakika hizo za mwisho ilikuwa kwamba  wapiga kura wanaweza wasimpende kwa yale yote aliyoyafanya, lakini mpinzani wake anatisha zaidi. Obama alikamilisha kampeni hiyo akiwa na matumaini ya ushindi. Kwake mkutano wa Iowa ulijaa kumbukumbu ya yaliyopita. Ushindi wake katika mkutano wa chama cha Democrats jimboni humo mwaka 2008 ndiyo iliyokuwa hatua ya kwanza katika mbio zake za urais. Na mkutano wake wa mwisho siku ya Jumatatu ulifanyika mbele ya jengo yalimokuwa makao makuu  ya kampeni zake katika uchaguzi huo wa 2008.

Mitt Romney kufanya kampeni hata siku ya uchaguzi

Mitt Romney kwa upande wake aliamua kusogeza kampeni yake ya miezi 18 hadi siku ya Jumanne, ili aweze kufanya ziara tena katika majimbo muhimu ya Ohio na lile linaloegemea upande wa Democrats la Pennyslivania katika siku ya uchaguzi. Kambi yake ilisema mgombea wao ataenda katika mji wa Cleveland, jimboni Ohia na Pittsburg katika jimbo la Pennyslvania, ambalo hakulitembelea kwa zaidi ya mwezi moja hadi siku ya Jumapili.

U.S. Republican presidential nominee and former Massachusetts Governor Mitt Romney and his wife Mitt Romney na mke wake Ann wakiwa katika mkutano wa kampeni mjini Manchester New Hampshire Jumatatu.
Mitt Romney na mke wake Ann wakiwa katika mkutano wa kampeni mjini Manchester New Hampshire Jumatatu.Picha: Reuters

Kampeni inasisitiza kuwa jimbo hilo sasa linaweza kuelekea kwake, hata wakati kura za maoni zinaonyesha Obama anaongoza kidogo tu katika majimbo yote yenye maamuzi. Ujumbe wa Romney kwa wapiga kura ni kwamba Obama ameshindwa na yeye ndiye atakayeweza. "Mlitarajia kuwa rais Obama atatekeleza ahadi yake kuwaleta watu pamoja na kutatua matatizo. Hajafanya hivyo, mimi nitafanya hivyo."

Kampeni siku ya uchaguzi???

Je, Kurefusha ratiba kwa Mitt Romney kutaongeza nafasi yake ya kushinda mchuano mkali na uliogharimu zaidi ya dola bilioni mbili? Jensin Johnson ni mchambuzi wa masuala ya kisiasa na meneja wa zamani wa kampeni za Congress: "Hakuna mtu utakayemshawishi siku ya mwisho, nadhani ni dalili kwamba Mitt Romney hajiamini vya kutosha na hajui mchuano huu utaisha vipi kwa hiyo anajaribu kila linalowezekana, sijui kama hii italeta mabadiliko yoyote lakini ndivyo nnavyoona," anasema.

Wapiga kura kumi waliyosajiliwa katika kijiji kidogo cha Dixville Notch, New Hampshire wakipiga kura za kwanza katika siku ya uchaguzi, dakika chache baada ya saa sita za usiku siku ya Jumanne. Kihistoria jimbo la Hampshire ndiyo linakuwa la kwanza kupiga kura nchini Marekani.
Wapiga kura kumi waliyosajiliwa katika kijiji kidogo cha Dixville Notch, New Hampshire wakipiga kura za kwanza katika siku ya uchaguzi, dakika chache baada ya saa sita za usiku siku ya Jumanne. Kihistoria jimbo la Hampshire ndiyo linakuwa la kwanza kupiga kura nchini Marekani.Picha: Reuters

Wagombea wote wanahitaji kura 270 za majimbo ili kupata ushindi. Licha ya ushindani kuwa mkali, njia ya ushindi kwa Obama ni nyepesi. Kama atashinda majimbo matatu aliyoyatembelea siku ya Jumatatu - yaani Wisconsin, Ohio na Iowa, basi atakuwa tayari amemaliza kazi.