1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Ni miaka 50 tangu kifo cha Martin Luther King Jr

Caro Robi
3 Aprili 2018

Je, ndoto ya kiongozi huyo wa harakati za haki za kiraia Martin Luther King Jr, ya kuwepo usawa Marekani imetimika au imegeuka kuwa jinamizi?

https://p.dw.com/p/2vQck
USA Martin Luther King Jr. - Rede "I have a dream", 1963
Picha: picture-alliance/AP Photo

Mnamo tarehe 4, mwezi Aprili mwaka 1968, vuguvugu la kupigania haki za kiraia nchini Marekani lilimpoteza kiongozi wao mkuu. Martin Luther King Jr aliuawa kwa kupigwa risasi akiwa amesimama katika kibaraza cha hoteli moja mjini Memphis. 

Martin Luther King Jr, kiongozi wa vuguvugu la amani la kupigania haki hasa za Wamarekani weusi aliuawa akiwa na umri wa miaka 39, hakuishi kuona kama ndoto yake ya kuwepo usawa Marekani ingefikiwa au la.

Licha ya kuongezeka kwa uhuru wa watu weusi nchini Marekani katika kipindi cha miaka 50 tangu kifo cha King Jr, watu wengi weusi nchini humo bado wanakabiliwa na changamoto chungu nzima katika karibu kila nyanja.

Je, ndoto ya usawa imetimia?

Kutokuwa na usawa wa kiuchumi, kubaguliwa,kukamatwa na kufungwa jela kwa Wamarekani weusi  na polisi kuwaua kiholela watu weusi yanajitokeza kama mambo matatu makuu ya mifano ya changamoto nyingi zinazoonesha bado watu weusi hawajapata hadhi ya kujihisi sawa na wazungu,kuthaminiwa na kufanikiwa maishani.

USA Memphis Martin Luther King 1968
Martin Luther King Jr(katikati) wakati wa maandamano mjini MemphisPicha: picture-alliance/AP Photo/J. Thornell

Katika jela za Marekani, kuna takriban wafungwa milioni 2.3 ambao ni watu weusi, hiyo ni asilimia 34 ya wafungwa wote nchini humo. Rekodi za kihalifu zinawafanya vijana kupata ugumu wa kupata kazi, kuwa na matatizo ya kisaikolojia na kuziathiri familia nyingi kwa kila nyanja. Uwezekano wa wanaume weusi kuuawa na polisi ni mara tatu kuliko wanaume wazungu.

Na hasa ikizingatiwa kuwa hivi sasa Marekani inaoongozwa na Rais ambaye anaonekana kuwa na ubaguzi wa rangi, wengi wanahofu kuwa juhudi zilizopigwa na Martin Luther King Jr na wanaharakati wengine wa kutetea usawa na haki za kiraia huenda zikahujumiwa.

Mkurugenzi wa kituo cha Ronald W. Walters kinachotoa mafunzo ya uongozi na sera za umma katika chuo kikuu cha Howard mjini Washington DC Elsie Scott anasema anatiwa wasiwasi na hali ilivyo hivi sasa Marekani.

Scott anasema hakuna matumaini makubwa nchini humo wakati taifa linapokumbuka miaka 50 tangu kuuawa kwa King Jr akiongeza kuwa anadhani watu wengi weusi wanatiwa wasiwasi na msimamo wa utawala wa Rais Donald Trump.

Licha ya kuwa kiwango cha elimu na kupenya kwa watu weusi katika tabaka la wastani na la juu kimeongezeka tangu miaka ya sitini lakini idadi ya wanaosalia katika umasikini na kutopata elimu ya kutosha inasalia kuwa juu mno.

Wamarekani weusi bado wanahisi kubaguliwa

Margaret Simms, mtafiti katika taasisi ya Urban mjini Washington D.C anasema asilimia ya watu weusi wanaopata kipato cha wastani inasalia kuwa kama ilivyokuwa miaka 50 iliyopita. Simms anasema viwnago vya umasikini hivi sasa vinawaathiri Wamarekani weusi mara tatu kuliko inavyowaathiri wazungu.

USA Protest der Black lives matter - Bewegung in Memphis, Tennessee
Nembo ya vuguvugu la kutetea haki za watu weusi MarekaniPicha: picture-alliance/dpa/M. Brown

Kunasalia kuwa na pengo kubwa la upatikanaji wa ajira kati ya watu weusi na wazungu nchini Marekani.

Ibrahim Kendi mkurugenzi wa kituo cha kupambana dhidi ya ubaguzi wa rangi katika chuo  kikuu cha Washington anasema  wakati King alipokuwa hai, wamarekani weusi walikuwa na uwetzekano wa mara mbili kutopata ajira ikilinganishwa na wazungu na sasa miaka 50 baada ya kifo chake bado hali ni hiyo hivyo kuashiria bado kubaguliwa kwa misingi ya rangi ya ngozi upo.

Wanaharakati wa kutetea usawa Marekani wanasema bila ya kuwepo fursa sawa za kiuchumi, Wamarekani weusi wamshindwa kujitengeza mali na hivyo kuwa na nafasi ndogo ya kufanikiwa maishani na kuwaachia vizazi vyao mali.

Mbali na hayo, katika mitaa wanayoishi Watu weusi, shule ni za viwango vya chini na hivyo watoto wa Wamarekani weusi wanashindwa kuvunja mkondo wa kutokuwepo elimu ya kiwango bora. Wachambuzi wanasema hadi pale hatua madhubuti zitakapochukuliwa kuvunja mkondo huo wa umasikini na ubaguzi wa Wamarekani weusi, hali hiyo itaendelea kwa miaka mingine 50 ijayo.

Mwandishi: Caro Robi/http://www.dw.com/en/50-years-after-martin-luther-king-jrs-death-a-dream-of-equal-opportunity-unfulfilled/a-43230622

Mhariri: Mohammed Abdul-Rahman