1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Nguvu zaidi zahitajika kukabiliana na ulanguzi wa binadamu

Hawa Bihoga-Dar es Salaam24 Agosti 2018

Ripoti kuhusu biashara haramu ya usafirshaji binadamu kwa nchi wananchama wa SADC imeonesha idadi kubwa ya waathiriwa wakuu wa biashara haramu ya usafirishaji binadamu, ni wale wa umri wa chini ya miaka 18 hadi 34

https://p.dw.com/p/33iKE
Lagos | Proteste gegen Menschenhandel
Picha: Getty Images/AFP/P. U. EkPei

Ofisi ya umoja wa mataifa inayopambana na dawa za kulevya pamoja na uhalifu imezitaka nchi wanachama wa Jumuiya ya maendeleo kusini mwa Afrika SADC, kuweka nguvu ya ziada katika kukabiliana na uhalifu wa usafirishaji binadamu unaoendelea kushuhudiwa hasa katika mataifa yananyoendelea. Hayo yamewekwa wazi katika uzinduzi wa ripoti kuhusu biashara haramu ya usafirshaji binadamu kwa nchi wananchama wa SADC.

Ripoti hiyo yenye kurasa sabini na nne, inaonesha idadi kubwa ya waathirika wa biashara haramu ya usafirishaji binadamu katika nchi wanachama wa Jumuiya ya maendeleo kusini mwa Afrika SADC, ni kuanzia umri wa chini ya miaka 18 hadi 34. Takwimu hizo zilikusanywa kutoka katika vyanzo rasmi ikiwemo polisi, uhamiaji, asasi za kiraia pamoja na mashirika yalio chini ya umoja wa mataifa.

Kwa nchini zimbabwe ripoti inaonesha visa takriban sabini na tano vya watu kusafirishwa kwa ajili ya biashara ya ngono viliripotiwa katika mamlaka za nchini humo, katika kipindi cha mwaka 2016 ambapo waathirika wengi walipelekwa nchini Angola na Kuwait huku wanawake wakiwa ni waathirika zaidi.

Ripoti hiyo imeendelea kueleza kuwa, katika kipindi cha desemba 2013 hadi machi 2014 takriban watoto 268 waliokolewa kutoka kwa wasafirishaji haramu wa binadamu katika Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo ambapo wengi walitumikishwa kama wabeba mizigo, wapishi, wasindikizaji pamoja na wapiganaji.

Katika kipindi cha desemba 2013 hadi machi 2014 takriban watoto 268 waliokolewa kutoka kwa wasafirishaji haramu wa binadamu katika Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo
Katika kipindi cha desemba 2013 hadi machi 2014 takriban watoto 268 waliokolewa kutoka kwa wasafirishaji haramu wa binadamu katika Jamhuri ya Kidemokrasia ya KongoPicha: Getty Images/AFP/G. Khan

Samantha Manodawafa, Mwakilishi wa Umoja wa Mataifa katika ofisi ya kupambana na kuzuia dawa za kulevya na uhalifu anasema kuwa, ni muhimu nguvu zikielekezwa katika uwelewa wa jamii juu ya biashara hiyo yenye nguvu na ushawishi duniani.

Ripoti hiyo imeiangazia Tanzania pia, ambapo imeonesha idadi kubwa ya waathhirika waliobainika katika kipindi cha mwaka 2015 hadi 2017 walitoka katika mkoa wa Rukwa ulio nyanda za Juu Kusini, na katika baadhi ya miji mikubwa ya kibiashara kama Mwanza, Arusha na Dare s salaam wahanga walibainika pia ambapo wengi walisafirishwa kuelekea nchini Oman.

Katika hili, serikali ya Tanzania inasema kuwa, uchunguzi uliofanyika wengi wa waathirika hudanganywa na watu wa karibu, na wazazi huruhusu watoto wao bila kuwa na uchunguzi wa kina kwa mawakala wa biashara hiyo, ambapo inasisitiza katika maboresho ya sheria ili kukabiliana na biashara hiyo. 

Nchi kumi na tano za SADC zilihuduria uzinduzi wa ripoti hiyo huku Tanzania ikiwa mwenyeji.

 

Mhariri:Iddi Ssessanga