Neymar afunga hat-trick kuizamisha Baseksehir | Michezo | DW | 09.12.2020
  1. Inhalt
  2. Navigation
  3. Weitere Inhalte
  4. Metanavigation
  5. Suche
  6. Choose from 30 Languages
Matangazo

Michezo

Neymar afunga hat-trick kuizamisha Baseksehir

Neymar alifunga hat-trick wakati Paris Saint-Germain illipoigaragaza Istanbul Baseksehir 5-1 Jumatano (09.12.2020) mechi yao ya ligi ya mabingwa mjini Paris

Wachezaji wa timu zote mbili pamoja na wasimamizi wa mechi walipiga magoti uwanjani kabla mechi kuanza tena. Mechi hiyo ilisitishwa dakika ya 14 Jumanne kufuatia madai kwamba afisa wa nne wa mechi kutoka Romania alikuwa ametumia neno la kibaguzi kumueleza kocha msaidizi wa Baseksehir, raia wa Cameroon, Pierre Webo.

Neymar aliiweka kifua mbele timu yake ya PSG baada ya dakika saba za mchezo. Klabu hiyo ya Ufaransa tayari ilikuwa imefuzu kwa duru ya 16 bora katika michuano ya ligi ya mabingwa barani Ulaya baada ya Manchester United kuangukia pua ilipolazwa 3-2 na RB Leipzig siku ya Jumanne. Hata hivyo vijana wa kocha Thomas Tüchel walihitaji kushinda mechi yao dhidi ya Baseksehir ili wamalize katika nafasi ya kwanza ya kundi H.

Kylian Mbappe alimpa pasi Neymar akafunga bao la pili na baadaye Neymar akapata penalti ambayo Mbappe aliifunga muda mfupi kabla kipindi cha mapumziko. Lilikuwa bao la 20 la Mbappe katika ligi ya mabingwa, lakini ni lake la kwanza katika mechi 10 za mashindano hayo tangu mwezi Desemba mwaka uliopita.

Neymar alikamilisha hat-trick yake na bao maridadi baada ya kucheza na kuonana vyema na Angel di Maria mwanzoni mwa kipindi cha pili. Mbappe aliifungia PSG bao la tano baada ya Mehmet Topal kuifungia Baseksehir bao la pekee. Timu hiyo ya Uturuki imemaliza duru ya kwanza ya mashindano ikiburuza mkia katika kundi H.

(afp)