New Zealand yatangaza visa vipya vya corona | Matukio ya Kisiasa | DW | 12.08.2020
  1. Inhalt
  2. Navigation
  3. Weitere Inhalte
  4. Metanavigation
  5. Suche
  6. Choose from 30 Languages
Matangazo

Matukio ya Kisiasa

New Zealand yatangaza visa vipya vya corona

New Zealand hii leo imesogeza mbele muda wa kuahirisha bunge kwa ajili ya kujiandaa na uchaguzi, wakati taifa hilo likifunga jiji lake kubwa la Auckland kufuatia kugundulika visa vipya vya virusi vya corona.

Visa hivi vipya vinatangazwa baada ya siku 102 za kutokuwepo kwa maambukizi miongoni mwa jamii nchini humo, wakati maambukizi ulimwenguni yakipindukia milioni 20.1. 

Auckland itafungwa baada ya kuripotiwa visa vinne vya COVID-19 jana Jumanne kutoka familia moja. Visa hivi vipya vinatangazwa baada ya siku 102 za kutokuwepo kwa maambukizi miongoni nchini New Zealand.

Bunge lilitarajiwa kuvunjwa hii leo, lakini waziri mkuu Jacinda Arden aliwaambia waandishi wa habari kwamba itasogezwa mbele hadi angalau Jumatatu ijayo ili kutoa nafasi ya kushughulikia suala la afya ambalo ni la msingi kwao.

Mkurugenzi mkuu wa afya katika wizara ya afya ya New Zealand Ashley Bloomfield amesema, baada ya mazungumzo na familia iliyogundulika na maambukizi, mamlaka zimepata mwangaza wa chanzo cha maambukizi na kuwataka watu kuwa waangalifu.

Neuseeland Coronavirus, PK Jacinda Ardern

Kulia ni mkurugenzi mkuu wa afya katika wizara ya afya ya New Zealand, Ashley Bloomfield

Alisema "familia bado imejitenga nyumbani kwao na tunashirikiana ili kuona kama baadhi yao ama familia nzima inaweza kupelekwa kwenye karantini za Auckland. Sasa, kufuatia mahojiano na kitengo cha afya ya umma na walioambikizwa, tumegundua kwamba kisa kimoja ni cha msichana wa miaka ya 20 aliyesafiri kwenda Rotorua siku ya Jumamosi wakati akiwa na dalili."

Kiwango cha tahadhari kwenye jiji hilo kimepandishwa hadi ngazi ya 3 kuanzia usiku wa kuamkia leo hadi usiku wa manane Ijumaa.

Na huko Urusi baada ya kutangaza kupata chanjo, shirika la afya ulimwenguni, WHO limesema ili iweze kupata kibali chake inahitaji kupitia tathmini ya hali ya juu ikiwa ni pamoja na usalama wake.

Msemaji wa WHO Tarik Jasarevic amesema wanawasiliana na mamlaka za afya za Urusi na majadiliano yanaendelea kuhusiana na uwezekano wa kutumika kwa chanjo hiyo kabla ya kuidhinishwa. Mkuu wa wakfu wa uwekezaji nchini humo unaofadhili mradi huo Kirill Dmitriev amesema awamu ya tatu ya majaribio huenda ikaanza leo.

Rais Vladimir Putin alisema Urusi imekuwa taifa la kwanza kuidhinisha chanjo inayotoa kile alichoita kinga endelevu dhidi ya virusi vya corona. Chanjo hiyo iliyopewa jina Sputnik V imetengenezwa na taasisi ya Gamaleya kwa kushirikiana na wizara ya ulinzi katika wakati ambapo tayari chanjo 168 zinafanyiwa uchunguzi kote ulimwenguni.

Russland Moskau | Nach der Abstimmung über Verfassungsänderung: Wladimir Putin

Rais wa Urusi Vladimir Putin anasema hana wasiwasi na chanjo hiyo iliyojaribiwa pia na binti yake.

Hata hivyo, hatua hiyo inaibua wasiwasi kwa baadhi ya wataalamu. Ni asilimia 10 ya majaribio ilionyesha mafanikio na baadhi yao wanahofia kwamba Moscow inatanguliza sifa kabla ya usalama.

Putin na maafisa wake wanasema chanjo hiyo ni salama kabisa na hasa baada ya binti yake kujitolea kuijaribu na baadae aliendelea kujisikia vizuri.

Kulingana na takwimu ya AFP, visa vilivyothibitishwa ulimwenguni vimepindukia milioni 20.1 na vifo 737,000.

Barani Ulaya, taasisi ya magonjwa ya ECDC imeyaonya mataifa kurejesha baadhi ya vizuizi wakati maambukizi yakiongezeka. Mataifa kama Ufaransa na Uhispania tayari yametangaza lazima ya watu kuvaa barakoa kwenye mikusanyiko.

Nchini Marekani, rais Donald Trump wa Marekani, amesema serikali yake itanunua dozi milioni 100 za chanjo ya majaribio ya Moderna, ambayo ipo katika hatua ya mwisho ya majaribio. Aidha serikali inaingia kwenye ushirikiano na kampuni ya Johnson&Johnson na mengineyo ya Marekani kusaidiana kutengeneza kiwango kikubwa wa chanjo.

Soma Zaidi: WHO yautaka ulimwengu kupambana vikali na COVID-19

Mashirika: DPAE/RTRE/DPAE/APE