1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
SiasaNew Zealand

New Zealand: Jacinda Ardern ashinda kwa kishindo

Daniel Gakuba
17 Oktoba 2020

Waziri Mkuu wa New Zealand Jacinda Ardern amepata ushindi mkubwa katika uchaguzi mkuu uliofanyika leo Jumamosi. Ushindi huo unakipa chama chake cha Labour nafasi ya kuunda serikali bila ya kuvishirikisha vyama vingine.

https://p.dw.com/p/3k4PJ
Neuseeland Wahl | Premierministerin Jacinda Ardern
Jacinda Ardern: Waziri Mkuu wa New ZealandPicha: Mark Baker/AP Photo/picture-alliance

Waziri Mkuu wa New Zealand Jacinda Ardern ameshinda kwa kishindo uchaguzi mkuu uliofanyika leo na kupata wingi wa viti bungeni utakaomwezesha kutekeleza mpango wake wa mageuzi.

Baada ya kuhesabiwa theluthi mbili ya kura zote, chama cha Waziri Mkuu Adern cha Labour kimepata asilimia 49.2 ya kura zote, huku kikitarajiwa kupata viti 64 katika bunge la New Zealand lenye viti 120.  

Soma zaidi:  Watu 49 wauawa kwenye shambulio la misikiti New Zealand 

Hakuna kiongozi mwingine aliyeweza kupata ushindi mkubwa kiasi hicho tangu New Zealand ilipoidhinisha mfumo wa uchaguzi unaozingatia uwiano wa uwakilishi wa kivyama mwaka 1996. Kukosa ushindi wa moja kwa moja kumevilazimisha vyama vilivyoongoza katika kura tangu wakati huo, kuunda serikali zinazovishirikisha vyama kadhaa vingine.

Upinzani wanyoosha mikono

Hata kabla ya kukamilika kwa zoezi la kuhesabu kura, kiongozi wa chama kikuu cha upinzani Judith Collins amekwishampigia simu Waziri Mkuu Ardern, akikubali kushindwa.

Neuseeland Wahl | Strafvollzugsministerin Judith Collins
Judith Collins: Kiongozi wa upinzani nchini New ZealandPicha: Mark Mitchell/New Zealand Herald/AP Photo/picture-alliance

Chama cha kihafidhina cha National Party cha Judith Collins kinatazamiwa kuambulia viti 35 bungeni, hayo yakiwa matokeo mabaya zaidi kwa chama hicho kwa kipindi cha miaka 20 iliyopita.

''Hongera kwa ushindi wako, kwa sababu naamini ni ushindi mkubwa kwa chama cha Labour. Imekuwa kampeni ngumu sana,'' amesema Bi Collins mbele ya umati mjini Auckland.

Soma zaidi: New Zealand yasitisha utafutaji miili katika volcano iliyoripuka

Ushindi huu wa Bi Jacinda Ardern ni mkubwa kuliko ilivyokuwa imetabiriwa katika uchunguzi wa maoni ya wapigakura, na wa juu zaidi kwa chama cha Labour tangu mwaka 1946.

Rais wa chama cha Labour Claire Szabo amesifu kampeni iliyofanywa na Ardern, mwanasiasa mchangamfu ambaye amesababisha wimbi la ushabiki kwa chama hicho alipochukua uongozi wake mwaka 2017, wakati huo chama hicho kikiwa kinaburura mkia katika chunguzi za maoni.

Szabo amesema ''bila shaka yoyote uongozi mahiri wa Jacinda Ardern umetoa mchango mkubwa katika maendeleo mazuri chamani.''

Ushindi uliotokana na kuyakabili majaribu

Jacinda Ardern alikuwa ameupachika uchaguzi huu jina la ''Uchaguzi wa Covid'' na juhudi zake zilikuwa kunadi mafanikio ya serikali yake katika kusimamisha maambukizi ya ugonjwa huo. New Zealand yenye wakazi milioni tano, imekwisharekodi vifo 25 tu kutokana na ugonjwa wa Covid-19.

Neuseeland Parlamentswahlen 2020
Uchaguzi huu ulisogezwa nyuma kutokana na kuripuka kwa ugonjwa wa COVID-19Picha: Hagen Hopkins/Getty Images

Lakini janga la virusi vya corona ni moja tu kati ya changamoto lukuki zilizodhihirisha sifa za uongozi wa Ardern mnamo muhula wake wa kwanza uongozini.

Mama huyo mwenye umri wa miaka 40 alionyesha moyo wa huruma, lakini pia ujasiri wa maamuzi baada ya shambulizi la bunduki lililofanywa mwaka jana na mtu mwenye itikadi ya kuwatukuza wazungu, ambaye aliuawa watu 51 waliokuwa wakisali misikitini katika mji wa Christchurch.

Soma zaidi: New Zealand yatangaza visa vipya vya corona

Kiongozi huyo alijikuta pia akikabiliwa na jukumu la kulifariji taifa lake baada ya mripuko wa volkeno katika kisiwa cha Whakaari, ambao uliuwa watu 21 na kuwaacha dazeni kadhaa wakiwa na majeraha mabaya.

''Bila kujali ukubwa wa mzozo ninaokabiliana nao, nawahakikishieni kuwa nitajitolea kikamilifu kwa kazi hii, hata kama hali hiyo itanilazimu kulipa gharama kubwa,'' aliyasema hayo Jacinda Ardern mapema wiki hii.

Uchaguzi huu ulikuwa umepangwa kufanyika Septemba 19, lakini ulisogezwa mbele kutokana na mripuko wa ugonjwa wa COVID-19 katika mji wa Auckland, ambao hivi sasa umekwishadhibitiwa.

afpe, dpae