1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

NEW YORK : Korea Kaskazini yawekewa vikwazo

15 Oktoba 2006
https://p.dw.com/p/CD2j

Nchi 15 wanachama wa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa kwa kauli moja zimeidhinisha azimio lenye kuweka vikwazo vikali kwa Korea Kaskazini kutokana na madai yake kwamba imefanya jaribio la bomu la nuklea.

Azimio hilo limepita baada ya Marekani,Uingereza na Ufaransa kuweza kuondowa tofauti za dakika ya mwisho na Urusi na China.Russia hususan ilikuwa ikisisitiza kwamba vikwazo hivyo visiwekwe kwa muda usiokuwa na kikomo.

Balozi wa Korea Kaskazini kwenye Umoja wa Mataifa Pak Gil Yon amesema nchi yake inalikataa azimio hilo na kusema kwamba jaribio hilo la bomu la nuklea limetekelezwa kutokana na kukabiliwa na sera za uhasama za Marekani.Amelishutumu Baraza la Usalama kwa kuwa ndumila kuwili na kusema kwamba hatua zaidi zitakazochukuliwa na chombo hicho cha dunia zitamaanisha tangazo la vita dhidi ya nchi hiyo.

Akilikaribisha azimio hilo Rais George W Bush wa Marekani amesema dunia imepeleka ujumbe wa wazi kwa kiongozi wa Korea Kaskazini kwamba hatua hiyo ya Umoja wa Mataifa iliochukuliwa kwa haraka na kali imeonyesha kwamba dunia imeungana pamoja katika azma yao ya kuona kwamba bara la Korea halina silaha za nuklea.

Rais huyo wa Marekani amesema Korea Kaskazini inaweza kuepukana na kutengwa huko kimtataifa na kupatiwa msaada wa kiuchumi wa Marekani iwapo itaachana na mipango yake ya silaha za nuklea.

Azimio hilo la Baraza la Usalama linataka Korea Kaskazini itokomeze mipango yake yote ya silaha za nuklea na kuepuka kufanya majaribio zaidi ya silaha hizo lakini limefuta uwezekano wa kuchukuliwa kwa hatua ya kijeshi dhidi ya nchi hiyo.