Netanyahu, Obama kukutana leo mjini Washington | Matukio ya Kisiasa | DW | 09.11.2015
  1. Inhalt
  2. Navigation
  3. Weitere Inhalte
  4. Metanavigation
  5. Suche
  6. Choose from 30 Languages

Matukio ya Kisiasa

Netanyahu, Obama kukutana leo mjini Washington

Waziri Mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu yuko mjini Washington leo kukutana na rais Barack Obama, katika juhudi za kusuluhisha tofauti baina yao, hususan kuhusiana na makubaliano juu ya mpango wa nyuklia wa Iran.

Israel Benjamin Netanjahu

Waziri Mkuu wa Israel, Benjamin Netanyahu

Mazungumzo hayo ambayo yatafanyika katika Ikulu ya Marekani mjini Washington ndiyo ya kwanza ya uso kwa uso kati ya Waziri Mkuu Netanyahu, na Rais Obama ambaye siku hizi hatafuni maneno katika kuelezea tofauti baina yake na kiongozi huyo wa Israel. Mara ya mwisho walikutana Oktoba, 2014. Ufa katika uhusiano ya viongozi hao wa nchi washirika ulizidi kupanuka mwezi Machi mwaka huu, baada ya hatua ya Netanyahu kwenda mjini Washington kuwashawishi wabunge wa chama cha Republican kuyakataa makubaliano kuhusu mpango wa nyuklia wa Iran, na kutoa hotuba ambayo iliichukiza Ikulu ya White House.

Mkutano wa leo ambao ni wa kikazi zaidi kuliko wa kirafiki, unalenga kupunguza pengo lililoachwa na ziara hiyo ya Netanyahu, na kusisitiza ushirikiano usiotetereka kiulinzi kati ya Marekani na Israel. Na hilo ndilo aliloligusia Waziri Mkuu Netanyahu, kabla ya kufunga safari kuelekea Marekani.

Mara ya mwisho Netanyahu na Obama walikutana Oktoba, 2015

Mara ya mwisho Netanyahu na Obama walikutana Oktoba, 2015

''Mazungumzo yangu na rais Obama yatajikita juu ya hali ya mambo katika Ukanda wa Mashariki ya Kati, ukiwemo mzozo wa Syria, na hatua zinazowezekana kusuluhisha mgogoro kati yetu na Wapalestina, angalau kutuliza hali ya sasa.'' Amesema Netanyahu na kuongeza kwamba bila shaka yatahusu pia kuimarisha usalama wa Israel, kitu ambacho ''daima ni kipaumbele kwa Marekani'' .

Ikulu ya White House yapoza malumbano

Kabla Netanyahu kuwasili mjini Washington, msemaji wa Ikulu ya Marekani Josh Earnest ameashiria kuupunguza mvutano baina ya Netanyahu na Obama, akisema tofauti zao ni ndogo zinapolinganishwa na utayarifu wao kushirikiana katika masuala muhimu.

Iron Dome, mfumo wa kujikinga makombora wa Israel

Iron Dome, mfumo wa kujikinga makombora wa Israel

Agenda kuu itakuwa hakikisho la wizara ya ulinzi ya Marekani kwa usalama wa Israel, kufuatia hofu iliyoelezewa na nchi hiyo kutokana na kusainiwa kwa makubaliano juu ya mpango wa nyuklia wa Iran. Netanyahu ameyaita makubaliano hayo kosa kubwa la kihistoria, akidai hayataweza kuizuia Iran, hasimu mkubwa wa Israel, kuunda silaha za nyuklia.

Mabilioni ya dola kila mwaka

Hadi sasa Israel inapokea kutoka Marekani, msaada wa dola bilioni 3 kila mwaka kwa ajili ya matumizi ya kijeshi, na msaada mwingine wa pembeni kama kujengewa mfumo wa kisasa wa kujikinga na makombora ujulikanao kama Iron Dome.

Makubaliano ya msaada huo ni ya miaka 10 ambayo itamalizika mwaka 2017, na kuna taarifa kwamba Netanyahu anataka uongezwe kwa kiasi kikubwa. Inatarajiwa kwamba Obama na Netanyahu watajadiliana mpango mwingine ambamo Marekani itaipa Israel ndege 33 chapa F-35 zenye teknolojia ya hali ya juu ambazo tayari Israel imeziagiza. Hali kadhalika, Marekani inatarajiwa kuipa Israel silaha zenye uwezo mkubwa wa kulenga shabaha, na silaha nyingine za kisasa kabisa ambazo zitaifanya Israel kuziacha mbali kijeshi nchi nyingine katika Ukanda wa Mashariki ya Kati.

Mwandishi: Daniel Gakuba/afpe/rtre

Mhariri: Josephat Charo

DW inapendekeza

Matangazo

Unaweza kusikiliza matangazo yetu hapa

Kusikiliza matangazo ya Idhaa ya Kiswahili ya DW, tafadhali bonyeza alama ya spika ya masikioni hapo chini, na kuwasiliana nasi, tafadhali tuandikie moja kwa moja kupitia: kiswahili@dw.com