Netanyahu kukutana na Rais Obama | Matukio ya Kisiasa | DW | 23.03.2010
 1. Inhalt
 2. Navigation
 3. Weitere Inhalte
 4. Metanavigation
 5. Suche
 6. Choose from 30 Languages

Matukio ya Kisiasa

Netanyahu kukutana na Rais Obama

Licha ya kufanyika mkutano huo, Netanyahu amesisitiza kuhusu mpango wa Israel kujenga makaazi mapya ya Walowezi huko Jerusalem Mashariki.

default

Waziri Mkuu wa Israel, Benjamin Netanyahu.

Waziri Mkuu wa Israel, Benjamin Netanyahu amesisitiza tena juu ya haki ya nchi yake kujenga makaazi ya wayahudi katika eneo wanalolikalia la Jerusalem Mashariki kabla ya mazungumzo yake na Rais Barack Obama yanayotarajiwa kufanyika baadaye hii leo, ambayo yatakuwa ya faragha.

Akionyesha dalili ya kutofikia maafikiano kuhusu mzozo ulioharibu uhusiano kati ya Israel na Marekani, Waziri Mkuu wa Israel, Benjamin Netanyahu, alisema Wayahudi waliijenga Jerusalem miaka 3,000 iliyopita na Wayahudi hao hao wataujenga mji huo hii leo. Bwana Netanyahu aliyasema hayo alipokuwa akiihutubia jumuiya inayoiunga mkono Israel, mjini Washington. Aidha, alisisitiza kuwa Jerusalem sio eneo wanalolikalia bali ni mji mkuu wao. Palestina inataka eneo la Jerusalem Mashariki linalokaliwa na Waarabu wengi ambalo lilichukuliwa na Israel baada ya vita vya mwaka 1967, liwe mji mkuu wa taifa lao la baadaye.

Awali kabla ya Netanyahu kuhutubia ujumbe wa watu 7,500 katika mkutano wa kamati ya uhusiano wa umma wa Marekani na Israel-AIPAC, alipewa onyo na Waziri wa Mambo ya Nchi za Nje wa Marekani, Hillary Clinton kuhusu mpango wa Israel wa kujenga maakazi mapya ya wayahudi katika eneo hilo. Bibi Clinton alisema, ''Kuna njia nyingine, njia ambayo inatuongoza kuelekea kwenye usalama na ustawi wa Israel, Wapalestina na watu wote wa eneo hilo. Lakini, itazilazimu pande zote, ikiwemo Israel kufanya maamuzi magumu lakini ambayo ni muhimu.''

Mkutano kati ya Rais Obama na Bwana Netanyahu uanfanyika kwa mara ya kwanza tangu Marekani ilipoishutumu vikali nchi hiyo kufuatia hatua yake ya kutangaza mpango huo wa kujenga makaazi mapya ya wayahudi wakati wa ziara ya Makamu wa Rais wa Marekani, Joe Biden. Ziara hiyo ya Bwana Biden ilikuwa ni katika jitihada za kuunga mkono mazungumzo ya amani.

Wakati huo huo, Waziri wa Mambo ya Nchi za Nje wa Ujerumani, Guido Westerwelle amesema kwamba Ujerumani na Umoja wa Ulaya hazina shaka kuwa sera ya kuendeleza ujenzi wa makaazi huko Jerusalem Mashariki ilikuwa inakwamisha juhudi zozote za kuelekea katika kupatikana kwa amani huko Mashariki ya Kati. Akizungumza katika kituo cha redio cha taifa-DLF, Westerwelle alisema, ''Huo ndio msimamo wa serikali kuu ya Ujerumani. huo pia ndio msimamo wa Umoja wa Ulaya na jumuiya ya kimataifa. Tunaamini kwamba hivyo ndivyo ilivyotajwa katika utaratibu mpya wa amani ulioandaliwa na pande nne yaani Roadmap, ujenzi wa makaazi ya walowezi lazima usitishwe.''

Ingawa siku ya Jumatatu Umoja wa Ulaya uliahirisha mkutano wake wa ngazi ya juu na Waziri wa Mambo ya Nchi za Nje wa Israel, Avigdor Lieberman, Westerwelle alikutana naye mjini Brussels. Katika hatua nyingine vyombo vya habari vya Uingereza vimeripoti kuwa nchi hiyo inajiandaa kumfukuza balozi wa Israel kwa kuhusika kwake na matumizi ya pasi bandia za kusafiria ambazo zilitumiwa na watuhumiwa wa mauaji ya kiongozi wa ngazi ya juu wa kundi la Hamas, Mahmud al-Mabhuh huko Dubai. Waziri wa Mambo ya Nchi za Nje wa Uingereza, David Miliband muda sio mrefu atatoa taarifa kwa bunge la nchi hiyo baada ya nchi hiyo kuitaka Israel kutoa ushirikiano kamili katika uchunguzi wa mauaji ya kamanda huyo wa Hamas aliyeuawa mwezi Januari, mwaka huu.

Mwandishi: Grace Patricia Kabogo (AFPE/IPS)

Mhariri:Abdul-Rahman,Mohammed

 • Tarehe 23.03.2010
 • Mwandishi Kabogo Grace Patricia
 • Chapisha Chapisha ukurasa huu
 • Kiungo https://p.dw.com/p/MaCk
 • Tarehe 23.03.2010
 • Mwandishi Kabogo Grace Patricia
 • Chapisha Chapisha ukurasa huu
 • Kiungo https://p.dw.com/p/MaCk
Matangazo

Unaweza kusikiliza matangazo yetu hapa

Kusikiliza matangazo ya Idhaa ya Kiswahili ya DW, tafadhali bonyeza alama ya spika ya masikioni hapo chini, na kuwasiliana nasi, tafadhali tuandikie moja kwa moja kupitia: kiswahili@dw.com