1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Netanyahu: IDF itafanya vita vikubwa makubaliano yakikiukwa

Angela Mdungu
29 Novemba 2024

Waziri Mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu amesema amelielekeza jeshi lake kujiandaa kwa vita vikali zaidi kama makubaliano ya kusitisha vita na kundi la Hezbollah yatakiukwa.

https://p.dw.com/p/4nYin
Benjamin Netanyahu ameonya kuwa jeshi lake litafanya vita vikubwa zaidi kama Hezbollah litavunja makubaliano ya usitishaji vita
Waziri Mkuu wa Israel Benjamin NetanyahuPicha: Uncredited/Israeli Government Press Office/AP/dpa/picture alliance

Waziri Mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu amesema amelielekeza jeshi lake kujiandaa kwa vita vikali zaidi kama makubaliano ya kusitisha vita na kundi la Hezbollah yatakiukwa. Ameitoa kauli hiyo wakati pande hizo mbili za mzozo zikishutumiana kwa kwenda kinyume na makubaliano yaliyoanza kutekelezwa Jumatano Asubuhi.

Benjamin Netanyahu amesema ametoa maagizo ya jeshi lake kujiandaa kurejea tena vitani ikiwa kundi la Hezbollah linaloungwa mkono na Iran ilitavunja makubaliano ya kusitisha vita. Ameyasema hayo Alhamisi alipokuwa katika mahojiano na kituo cha televisheni cha channel 14 cha Israel.

Soma zaidi: Lebabon: Israel haitaki kusitisha vita

Kauli ya Netanyahu imetolewa mara baada ya jeshi lake kusema Alhamisi kuwa, lilifanya mashambulizi ya anga yaliyolilenga ghala la Hamas lililotumika kuhifadhi roketi kusini mwa Lebanon.

Hayo yakijiri, msemaji wa jeshi la Israel Avichay Adraee kupitia jukwaa la mtandao wa kijamii wa X amesema, wakaazi wa Lebanon hawaruhusiwi kwenda katika vijiji 60 vilivyo upande wa kusini na maeneo yanayovizunguka hadi itakapotangazwa tena. 

Adraee ameonya kuwa yeyote atakayeelekea katika eneo hilo anajiweka hatarini. Awali jeshi la Lebanon liliishutumu Israel kwa kukiuka makubaliano ya kusitisha vita mara kadhaa Jumatano na Alhamisi.

Hatari inayakabili makubaliano ya kusitisha vita

Kutupiana lawama kati ya pande za mzozo huo kunaashiria udhaifu wa makubaliano ya kusitisha vita yaliyosimamiwa na Marekani na Ufaransa kwa lengo la kuumaliza mzozo kati ya Hezbollah na Israel. Makubaliano hayo yanatarajiwa kudumu kwa siku 60 kwa matumaini ya kupata suluhisho la kudumu la vita hivyo.

Lebanon
Mji wa Kusini mwa Lebanon wa Nabatiyeh ulioathiriwa na mashambulizi ya IsraelPicha: Adnan Abidi/REUTERS

Katika hatua nyingine, wahudumu wa afya katika Ukanda wa Gaza wamesema mashambulizi ya anga ya Israel yamewauwa takriban Wapalestina 26 Alhamisi. Majeshi ya Israel yamezidisha mashambulizi yake katikati mwa Gaza na kupeleka vifaru vya kivita Kaskazini na Kusini mwa Ukanda huo.

Hospitali ya Al Adwa pekee iliyo katikati mwa Gaza imesema imepokea miili 16 ya watu waliouwawa na majeruhi 55 tangu mashambulizi makali yalipoanza kufanywa katika eneo la Nuseirat.

Nalo shirika la habari la Palestina WAFA limesema vikosi vya Israel vimeshambulia pia kambi ya watu wasio na makazi huko Khan Younis kusini mwa Gaza na kuwauwa watu wanne wakiwemo mtoto mmoja, na kuwajeruhi wengine.