1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Netanyahu azuwia mpango wa ubaguzi dhidi ya Wapalestina

Admin.WagnerD20 Mei 2015

Waziri mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu amesitisha utekelezaji wa mpango tata unaowapiga marufuku Wapalestina kusafiria mabasi sawa na walowezi wa Kiyahudi wakati wanatoka kazini Israel kwenda Ukingo wa Magharibi.

https://p.dw.com/p/1FTMC
Israel Bus Reisende
Picha: Getty Images/AFP/M. Kahana

Afisa kutoka ofisi ya waziri mkuu alisema Netanyahu alimpigia waziri wa ulinzi Moshe Yaalon kumuambia kuwa mpango wake huo haukubaliki na wawili hao waliamua kuusitisha. Yaalon alikuwa ameuzindua mpango huo wa majaribio wa miezi mitatu, kufuatia malalamiko ya mara kwa mara kutoka kwa walowezi wa Kiyahudi wanaotumia usafiri wa mabasi, na wanasema wafanyakazi wa Kipalestina wanatoa kitisho cha usalama na kwamba wanawanyanyasa abiria wa kike wa Kiyahudi.

Mamia kwa maelfu ya Wapalestina husafiri kila siku kwenda kazini ndani ya Israel, hususani katika biashara ya ujenzi, wakitumia vibali vya kusafiri kila wakati wanapovuka, lakini mapendekezo ya mabadiliko hayo yangewalaazimisha kurudi nyumbani kupitia kituo sawa walichopitia wakati wanakwenda asubuhi, na kuwazuwia kusafiria katika mabasi ya Ukingo wa Magharibi pamoja na Waisrael.

Waziri Mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu.
Waziri Mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu.Picha: picture-alliance/epa/MENAHEM KAHANA

Wakosoaji walaani mpango huo

Wakosoaji waliushambulia mpango huo wakiutaja kuwa wa kibaguzi na kusema kuwa ungeharibu sifa ya Israel, ambayo tayari inakabiliwa na shinikizo kutokana na kuendeleza shughuli za ulowezi katika Ukingo wa Magharibi. Israel ililiteka eneo la Ukingo wa Magharibi kutoka kwa Jordan wakati wa vita vya mwaka 1967, na Wapalestina wanalitaka eneo hilo kama sehemu ya taifa lao lijalo.

Kiongozi wa upinzani Isaac Herzog, aliandika kwenye ukurasa wake w aFacebook kwamba kutenganishwa Wapalestina na Wayahudi kwenye usafiri wa umma ni idhalilishaji usiyostahili na doa kwa Israel na raia wake, na kwamba hatua hiyo inaongeza tu mafuta kwenye moto wa chuki dhidi ya Israel duniani.

Naye Zehava Galon, kiongozi wa chama cha dovish Meretz, alikwenda mbali zaidi akisema kwamba "hivi ndivyo ubaguzi wa rangi na utengano Arpatheid" unavyofanana.

"Sheria hiyo siyo jambo jipya, ni sehemu ya mwendelezo wa sheria za kibaguzi dhidi ya watu wetu na wafanyakazi wa Kipalestina wanaofanya kazi ndani ya Israel," alisema Hussein Fuqahaabi, afisa kutoka chama cha wafanyakazi cha Wapalestina.

Waungaji ulowezi waukataa pia

Pendekezo hilo lilishambuliwa pia na waungaji mkono wa ulowezi, wakisema halisaidii malengo yao na badala yake linasababisha tu uharibifu usiyo na msingi kwa taswira ya Israel.

Netanyahu alibadili mwelekeo haraka kufuatia ukosoaji mkubwa, hatua iliyoashiria mwanzo usiyo mzuri sana kwa serikali iliyoingia madarakani wiki hii na ambayo haijafanya hata kikao kimoja cha baraza la mawaziri.

Waziri wa ulinzi wa Israel Moshe Yaalon.
Waziri wa ulinzi wa Israel Moshe Yaalon.Picha: picture-alliance/dpa

Muungano wa Netanyahu unahodhiwa na wabunge wenye msimamo mkali wanaojishajiisha na vuguvugu la walowezi wa Ukingo wa Magharibi. Ungaji wao mkono wa ujenzi wa makaazi zaidi ya walowezi, na upinzani wao kwa mchakato wa amani na Wapalestina, unaweka uwezekano wa misuguano kati ya Israel na washirika wake wa magharibi.

Mpango huo wa mabasi, laiti kama ungelitekelezwa, ungezua ulinganishaji na mfumo wa Arptheid wa nchini Afrika Kusini, na pia ubaguzi wa rangi kwenye mabasi uliyoibua vuguvugu la haki za kiraia la Marekani.

Rais wa heshima wa Israel Reuvin Rivlin, amesifu usitishaji mpango huo, akisema utenganishaji kati ya Waisrael na Waarabu ni jambo ambalo halingeliwazika.

Mwandishi: Iddi Ssessanga/ape.rtre

Mhariri: Mohammed Khelef