1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Netanyahu aunda serikali ya mseto Israel

7 Mei 2015

Waziri mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu amefanikiwa kuunda serikali mpya ya mseto dakika chache kabla ya kumalizika muda uliopangwa kwa kiongozi huyo kuwasilisha serikali yake.

https://p.dw.com/p/1FMEc
Symbolbild - Isreal Premierminister Benjamin Netanjahu
Picha: DAN BALILTY/AFP/Getty Images

Netanyahu alifanikiwa kukishawishi chama cha kiyahudi cha mrengo wa kulia cha Jewish Home Party baada ya Waziri wa Mambo ya Nje katika serikali inayoondoka madarakani, Avigdor Lieberman, kukataa chama chake cha Yisrael Baitenu, kuwa sehemu ya muungano wa Likud.

Makubaliano hayo ya serikali ya mseto yanamhakikishia kupata wingi wa viti 61 katika bunge la nchi hio lenye viti vya wabunge 120.

Mtazamo wa Netanyahu

"Nina hakika kuwa hamna aliyeshangazwa na jinsi mazungumzuo yalivyofanywa na pande mbali mbali na pia hamna aliyeshangazwa kuwa makubaliano yametokea wakati yalipotokea" Alisema Netanyahu siku ya Jumatano.

Waziri Mkuu huyo wa Israel ameapa kwamba kufikia wiki ijayo ataweza kukamilisha "serikali iliyo na nguvu na iliyo imara kwa ajili ya watu wa Israel", hata hivyo aliashiria kwamba kuna umwezekano siku za mbele kuupanua muungano wa serikali hio mpya kwa kushirikisha washirika zaidi.

"Sitini na moja ni nambari nzuri, na zaidi ya sitini na moja ni nambari nzuri zaidi," alisema. "Lakini serikali itaanzia na viti 61na tutaanzia hapo. Tuna kazi kubwa mbele yetu."

Naftali Bennett und Benjamin Netanjahu
Naftali Bennett akiwa na Benjamin NetanjahuPicha: Getty Images/Afp/G.Tibbon

Vyama vya siasa vilivyoungana kuunda serikali hio ya pamoja inayoongozwa na Netanyahu ni pamoja na chama chake cha kihafidhina cha Likud kilichoshinda viti 30 katika uchaguzi uliopita wa mwezi Machi.

Kimo pia chama cha Kulanu kinachoongozwa na waziri wa zamani wa mawasiliano Moshe Kahlon ambacho kilishinda viti 10 katika uchaguzi uliopita, nakukifanya chama hicho kama mshirika muhimu katika serikali ya Netanyahu.

Vyama vingine katika serikali hiyo ya mseto ni viwili vya kiorthodox ikiwa ni pamoja na kile cha Jewish Home kinachongozwa na Naftali Bennet ambacho kilishinda viti 8 pamoja na chama cha United Torah Judaism ambacho kilipata viti 6.

Maoni ya kuipinga serikali hio

Kwa upande wa Palestina, wanaingalia serikali hio mpya ya muungano wa kidini inayoelemea mrengo wa kulia, kama kizuwizi kikubwa kufikia makubaliano ya amani na Israel.

Serikali hii "itakuwa ya kuchochea vita na pia itakuwa dhidi ya jitihada za kuleta amani na utulivu katika mkoa wetu," Saeb Erakat mzungumzaji wa Palestina aliliambia shirika la habari la AFP.

Kuna wasiwasi kwamba serikali hio mpya itavutana na Marekani pamoja na washirika wengine muhimu, kwa sababu vyama vyote vinne vinavyoiunda ni vevye msimamo mkali wa mrengo wa kulia vinavyopinga hatua za kuleta amani baina ya Israel na Palestina. Jambo hilo yumkini litamfanya Netanyahu kupata wakati mgumu katika kupata msaada na ungwaji mkono wa kimataifa.

Kiongozi wa chama cha upinzani cha mrengo wa kushoto cha Zionist Union,Isaac Herzog, ameuita muungano huo kuwa ni "Serikali ya kulifedhehesha taifa." Amesema serikali hio ni"ni kinyago cha aibu" na "aibu ya mwisho katika historia ya Israel."

Mwandishi: Yusra Buwayhid/APE/AFP/DPAE

Mhariri:Gakuba Daniel