1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Netanyahu atishia kuufuta mkutano wake na Sigmar Gabriel

Oumilkheir Hamidou
25 Aprili 2017

Mkutano kati ya waziri mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu na waziri wa mambo ya nchi za nje wa Ujerumani Sigmar Gabriel unakabiliwa na kitisho cha kutofanyika. Habari hizo zimetangazwa na afisa wa serikali ya Israel.

https://p.dw.com/p/2brQJ
Israel Bundesaußenminister Sigmar Gabriel auf dem Flughafen in Tel Aviv
Picha: picture-alliance/dpa/B. von Jutrczenka

 

Kwa mujibu wa afisa huyo wa serikali ya Israel, waziri mkuu Benjamin Netanyahu ametishia kufutilia mbali mkutano huo ikiwa waziri wa mambo ya nchi za nje wa Ujerumani Sigmar Gabriel atakutana na wawakilishi wa mashirika yanayoikosoa serikali yake. Akizungumza na kituo cha televisheni cha Ujerumani ZDF, mwanasiasa huyo wa chama cha Social Democrat amesema tunanukuu" litakuwa jambo la kusikitisha sana pindi akiamua kuufuta mkutano huo."

 

Waziri wa mambo ya nchi za nje wa Ujerumani , akiwa ziarani nchini Israel alishiriki jana katika kumbukumbu za wahanga wa mauwaji ya halaiki ya wanazi Holocaust katika makumbusho ya Yad Vashem. Leo amepanga mbali na mengineyo kuzungumza na wawakilishi wa mashirika ya "Breaking the Silence"- na "B'T Salam ". Mashirika hayo yasiyomilikiwa na serikali yanakosoa ujenzi wa makaazi ya wayahudi pamoja pia na mambo yanayofanywa na wanajeshi wa Israel katika maeneo ya wapalastina.

Waziri wa mambo ya nchi za nje Sigmar Gabriel akizungumza na mchamungu Nikodemus Schnabel mjini Jerusalem
Waziri wa mambo ya nchi za nje Sigmar Gabriel akizungumza na mchamungu Nikodemus Schnabel mjini JerusalemPicha: picture-alliance/dpa/B. von Jutrczenka

 Ni muhimu kupata sura halisi namna ilivyo

Afisa wa serikali ya Israel ambae hakutaka jina lake lijulikane amethibitisha kwamba maazungumzo pamoja na mashirika hayo ndio sababu iliyomfanya  Netanyahu atishie kufutilia mbali mkutano wake pamoja na waziri wa mambo ya nchi za nje wa Ujerumani-Sigmar Gabriel. Kwanza habari hizo zilitangazwa na kituo cha matangazo cha Israel Channel 2.

 

Gabriel amekiambia kituo cha televisheni cha ZDF leo asubuhi," amepata habari kuhusu uwezekano wa kufutwa mazungumzo yake na Netanyahu kupitia vyombo vya habari vya Israel. Anasema "anashindwa kuamini hayo kwasababu jambo kama hilo lingekuwa la kusikitisha kupita kiasi". Kinyume chake kisingewezekana hata kidogo, mazungumzo pamoja na Netanyahu kufutiliwa mbali kwasababu anataka kukutana na wakosoaji wa serikali nchini Ujerumani."

Kitambulisho cha uhusiano mzuri kati ya Ujerumani na Israel
Kitambulisho cha uhusiano mzuri kati ya Ujerumani na IsraelPicha: picture-alliance/dpa/R. Schlesinger

Sigmar Gabriel kukutana na rais Reuven Rivlin

 Sigmar Gabriel ameongeza kusema tunanukuu" hupati picha halisi ya mambo ikiwa utabakia katika ofisi za serikali kuu, mtu anabidi akutane na waandishi vitabu, wasanii, wanafunzi na pia mashiirika yanayoikosoa serikali. Ameongeza kusema mazungumzo yake pamoja na masahirika hayo anahisi ni muhimu kwasababu yanajishughulisha na masuala ya uhusiano kati ya Israel na wapalastina-mada ambayo anasema wanaizungumzia kila siku na wanahitaji kupata sura halisi namna ilivyo. Hata hivyo Sigmar Gabriel amesema anataraji yaliyosemwa kuhusu uwezekano wa kufutwa mkutanao wake pamoja na waziri mkuu Netanyahu ni uvumi tu. Sigmar Gabriel atakutana na rais Reuven Rivlin baadae leo,tukio ambalo waziri wa mambo ya nchi za nje wa Ujerumani analisema kuwa ushahidi kwamba ujumbe wa Ujerumani unapokelewa vizuri na kwa urafiki nchini Israel. Itafaa kusema hapa kwamba waziri mkuu wa Israel alighadibishwa mwezi february mwaka huu pale waziri mkuu wa Ubeligiji Charles Michel alipokutana na wawakilishi wa Breaking The Silence na B'TSalam nchini Israel.

 

Mwandishi:Hamidou Oumilkheir/AFP

Mhariri:Yusuf Saumu