Netanyahu asitisha makubaliano na UNHCR kuhusu wahamiaji | Matukio ya Kisiasa | DW | 03.04.2018
  1. Inhalt
  2. Navigation
  3. Weitere Inhalte
  4. Metanavigation
  5. Suche
  6. Choose from 30 Languages

Matukio ya Kisiasa

Netanyahu asitisha makubaliano na UNHCR kuhusu wahamiaji

Waziri mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu amefutilia mbali makubaliano na shirika la Umoja wa Mataifa la kuwashughulikia wakimbizi-UNHCR yaliyolenga kuepusha kurejeshwa makwao kwa lazima wahamiaji wa Kiafrika.

Siku moja tu baada ya Netanyahu kutangaza kuwa Israel imefikia makubaliano na shirika la Umoja wa Mataifa kuhusu wakimbizi UNHCR yatakayowapeleka maelfu ya wahamiaji katika nchi kadhaa za magharibi, leo, waziri huyo mkuu wa Israel amebatilisha uamuzi huo kutokana na shinikizo kali kutoka kwa wanasiasa wenye misimamo mikali wa mrengo wa kulia, wakiwemo washirika wake na wengi wa wafuasi wake wa tangu jadi.

Msemaji wa shirika hilo la UNHCR William Spindler amemuomba Netanyahu kutafakari upya uamuzi huo wa kufutilia mbali makubaliano yaliyotangazwa Jumatatu. Spindler ameongeza wamepata taarifa za kufutiliwa mbali kwa makubaliano waliyoyafikia kupitia vyombo vya habari.

Hatma ya wahamiaji iko mashakani

Kiongozi wa chama cha Labor Avi Gabbay ameshutumu kukengeuka kwa Netanyahu akihoji kama pia maamuzi ya kijeshi yanachukuliwa kwa njia hiyo ya kubadilisha maamuzi kiholela, akimshutumu Netanyahu kwa kuchukua maamuzi kutokana na maoni katika mitandao ya kijamii na tafiti za kupima umaarufu.

Israel Migranten protestieren gegen israelische Asylpolitik (Imago/UPI Photo)

Wahamiaji wakiandamana nje ya majengo ya bunge ya Israel

Baada ya kushutumiwa vikali, Netanyahu ametoa taarifa kusema kuwa anasitisha makubaliano hayo ambayo yangewaruhusu maelfu ya wahamiaji kusalia Israel kwa muda baada ya kufanya mashauriano kuhusu manufaa na athari za makubaliano hayo.

Makubaliano hayo kati ya Israael na UNHCR yalipaswa kukomesha mpango wa kurejesha kwa lazima wahamiaji Afrika chini ya mpango wenye utata uliowasilishwa na Netanyahu mnamo mwezi Januari ambapo alitaka wapelekwe Rwanda au Uganda la sivyo wafungwe na kurejeshwa makwao kwa lazima.

Rwanda na Uganda zilikanusha kufikiwa kwa makubaliano hayo ya kuwapokea wahamiaji kutoka Israel ambao wanarejeshwa Afrika kwa nguvu. Chini ya makubaliano na Umoja wa Mataifa, wahamiaji takriban 16,000 walikuwa wapewe hifadhi katika nchi za magharibi.

Netanyahu abadilika ghafla

Netanyahu jana alizitaja Ujerumani, Italia na Canada kuwa nchi ambazo zimekubaliana na UNHCR kuwapokea wahamiaji hao.

Israel PK Netanjahu (REUTERS)

Waziri mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu

Badala yake, Israel ilikuwa iwape wahamiaji wanaosalia hifadhi ya muda. Kuwepo kwa wahamiaji wa Kiafrika nchini humo wengi wao kutoka Sudan na Eritrea limekuwa suala msumari moto katika siasa za Israel. Netanyahu mara kwa mara amekuwa akiwataja wahamiaji hao kuwa sio wakimbizi halali bali wavamizi wanaotafuta fursa za kujiimarisha kiuchumi.

Leo asubuhi, kiongozi huyo alifanya mazungumzo na wakaazi wa kusini mwa mji mkuu wa Tel Aviv ambako wengi wa wahamiaji hao wanaishi. Baadhi ya wakazi wa Tel Aviv wamekosoa vikali makubaliano ya kuwaruhusu wahamiaji kuendelea kuwepo Israel. Wahamiaji na wanaowaunga mkono pia wameandamana nje ya ofisi za Netanyahu mijini Jerusalem na Tel Aviv.

Kulingana na takwimu za wizara ya mambo ya ndani ya Israel kuna wahamiaji wa Kiafrika 42,000 wanaoishi nchini humo nusu ya idadi hiyo wakiwa watoto, wanawake na wanaume wenye famili ambao hawawezi kurejeshwa makwao mara moja.

Mwandishi: Caro Robi/afp/reuters/ap

Mhariri:Josephat Charo

Matangazo

Unaweza kusikiliza matangazo yetu hapa

Kusikiliza matangazo ya Idhaa ya Kiswahili ya DW, tafadhali bonyeza alama ya spika ya masikioni hapo chini, na kuwasiliana nasi, tafadhali tuandikie moja kwa moja kupitia: kiswahili@dw.com