1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Netanyahu ashindwa kuunda serikali

Lilian Mtono
22 Oktoba 2019

Waziri mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu ametangaza kushindwa kuunda serikali yenye wingi wa kutosha bungeni, hatua inayoashiria kikwazo kikubwa dhidi ya kiongozi huyo anayekabiliwa na matatizo mengi.

https://p.dw.com/p/3Rh2x
Israel Regierungsbildung | Benjamin Netanjahu & Reuven Rivlin
Picha: Reuters/R. Zvulun

Waziri mkuu huyo sasa analitumbukiza taifa hilo kwenye mwanzo mpya wa sintofahamu ya kisiasa. 

Kwenye taarifa yake, Netanyahu amesema pamoja na kufanya kazi bila kuchoka ili kufanikisha uundwaji wa serikali hiyo ya mseto pamoja na mpinzani wake mkubwa Benny Gantz lakini hajafanikiwa. Wakati kesho ikiwa ndio siku ya mwisho ya kukamilisha mchakato huo, Netanyahu amesema anarejesha mamlaka kwa rais Reuven Rivlin ambaye atalazimika sasa kumuomba Gantz kujaribu kuunda serikali.

"Kila jitihada nilizofanya za kuunda serikali ya kitaifa na kuzuia uchaguzi mwingine hazikufanikiwa. Amekataa tu. Ninasikitika kwamba kukataa kwake kunaonyesha jambo moja tu kwamba anaendelea kuwa mateka wa Avigdor Lieberman ambaye anaendeshwa na maswala ya nje yanayohusiana na mambo yake ya kibinafsi na Yair Lapid ambaye anafaidika na kushindwa kwake. Gantz, Lapid na Lieberman wanazungumza tu kuhusu umoja, lakini wanatekeleza kinyume kabisa." alisema Netanyahu.

Kwa Netanyahu aliyetimiza miaka 70 jana, hilo ni pigo kubwa. Kwenye uchaguzi wa mwezi Aprili, Netanyahu pia alishindwa kulishawishi bunge na kulazimika kuitisha uchaguzi mwingine uliofanyika Septemba 17. Hivi sasa, ikiwa ni mara ya kwanza tangu alipochaguliwa mapema mwaka 2009, taifa hilo linakabiliwa na uwezekano wa kuchagua kiongozi mwingine.

Israel Regierungsbildung | Benjamin Netanjahu & Reuven Rivlin
Waziri mkuu Benjamin Netanyahu akiwa na rais Rivlin, anayetarajiwa kumuomba Gantz kuunda serikaliPicha: Reuters/R. Zvulun

Hata hivyo Gantz pia atakabiliwa na kizingiti kigumu, kwa kuwa bila ya chama cha Likud cha Netanyahu atakabiliwa na wakati mgumu kupata wingi wa viti bungeni.

Kwenye taarifa fupi iliyotolewa na chama chake cha Bluu na Samawati amesema, sasa ni wakati wa kuchukua hatua. Chama hicho kimesema kimedhamiria kuunda serikali ya umoja ya kiliberali iliyoongozwa na Benny Gantz, ambayo watu wa Israel waliichagua miezi michache iliyopita.

Gantz ameapa kuliunganisha tena taifa hilo baada ya utawala wa muda mrefu wa Netanyahu, ambao amesema umezidisha mgawanyiko wa kidini na kisiasa, lakini pia madai ya ufisadi yanayomkabili kiongozi huyo.

Wakati mwanasheria mkuu wa Israel naye akijiandaa kutoa maamuzi katika wiki chache zijazo kuhusu kumfungulia mashitaka ya mlolongo wa madai hayo ya ufisadi, waziri mkuu huyo huenda akakabiliwa na wakati mgumu zaidi kutokana na shinikizo la kumtaka ajiuzulu.

Kwenye uchaguzi mkuu wa mwezi uliopita, Netanyahu alishindwa kupata wingi wa viti bungeni. Lakini rais Rivlin alimpa nafasi ya kwanza ya kuunda serikali kwa kuwa alikuwa na uungwaji mkono wa wabunge 55, kuliko Gantz aliyekuwa akiungwa mkono na wabunge 54.