1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Netanyahu afanya ziara ya kwanza nchini Chad

Oumilkheir Hamidou
22 Januari 2019

Waziri mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu yuko ziarani Chad kwa lengo la kufufua uhusiano wa kidiplomasia uliopooza tangu miaka 50 iliyopita.

https://p.dw.com/p/3BrTI
Israel Staatsbesuch Idriss Deby Präsident des Tschad und Benjamin Netanjahu
Picha: Getty Images/AFP/r. Zvulun

 

Takriban miongo mitano tangu uhusiano wa kidiplomasia ulipovunjika kati ya Israel na Chad, waziri mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu amewasili Ndjamena leo  kwa lengo la kuanzisha upya uhusiano kati ya nchi hizo mbili.

Benjamin Netanyahu ameamkiwa alipowasili mji mkuu Ndjamena na waziri wa mambo ya nchi za nje Mahamat Zene Cherif pamoja na maafisa wengine wa serikali kabla ya kwenda moja kwa moja kukutana na rais wa Chad Idriss Deby.

Waziri mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu
Picha: Getty Images/AFP/L. Correa

Netanyahu anaitaja ziara yake Chad kuwa ni sehemu ya mapinduzi katika ulimwengu wa kiarabu na kiislam

Kabla ya kuondoka Israel waziri mkuu Netanyahu alisema:"Nnaondoka kwa lengo la kufikia ufanisi  mwengine muhimu na wa kihistoria nchini Chad, nchi kubwa ya kiislam inayopakana na Libya na Sudan."

"Hii ni sehemu ya mapinduzi yetu katika ulimwengu wa kiarabu na kiislam. Nnaahidi yatatokea. Habari zaidi muhimu zitatolewa. Nchi zaidi zitafuatia." Ameendelea kusema, ziara hiyo inaisumbua na kuikera Iran na pia miongoni mwa Wapalestina wanaojaribu kuizuwia. Hawatofanikiwa" amesema waziri mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu.

Rais Idriss Deby wa Chad
Rais Idriss Deby wa ChadPicha: Getty Images/AFP/L. Marin

Uhusiano wa kibalozi kati ya Israel na Chad, nchi yenye wakaazi wengi wa kiislam umevunjika mwaka 1972.

Deby alikutana na Netanyahu Novemba iliyopita mjini Jerusalem. Kwa mujibu wa taarifa iliyochapishwa na ofisi ya waziri mkuu Netanyahu wakati ule, viongozi hao walizungumzia mapambano dhidi ya ugaidi sawa na kuimarisha ushirikiano wa pande mbili katika sekta ya kilimo, juhudi za kupambana na ugaidi, ulinzi wa mpakani, teknolojia, nishati ya juwa, maji na afya.

Idriss Deby, akiwa madarakani tangu miongo mitatu iliyopita, anaitawala Chad kwa mkono wa chuma. Lakini juhudi za jeshi la Chad linalosaidia katika mapambano dhidi ya kundi la itikadi kali la Boko Haram katika nchi jirani za Nigeria, Niger na Cameroon, zimeipatia Chad sifa na kuangaliwa kuwa mshirika mkubwa wa nchi za magharibi.

Mwandishi:Hamidou Oummilkheir/dpa

Mhariri: John Juma