Netanyahu aapa kujibu mashambulizi dhidi ya Israel | Matukio ya Kisiasa | DW | 29.05.2018
  1. Inhalt
  2. Navigation
  3. Weitere Inhalte
  4. Metanavigation
  5. Suche
  6. Choose from 30 Languages

Gaza

Netanyahu aapa kujibu mashambulizi dhidi ya Israel

Majeshi ya Israel yameushambulia Ukanda wa Gaza baada ya wanamgambo wa Kipalestina kufanya mashambulizi mapya ya makombora kuelekea kusini mwa Israel.

Jeshi la Israeli limefanya mashambulizi katika Ukanda wa Gaza baada ya wanamgambo hao wa Kipalestina kurusha takriban makombora 28 ndani ya Israeli, ambayo yaliufyatua mfumo wa kinga dhidi ya silaha wa Israel wa Iron Dome.

Kundi la Hamas linalotawala katika Ukanda wa Gaza, na washirika wake wa kundi dogo la wapiganaji la Islamic Jihad wamethibitisha kwamba kambi zao za kijeshi zimeshambuliwa kwa mabomu ingawa hakuna watu walioripotiwa kujeruhiwa kwenye mashambulizi hayo ya Israel. 

Mashambulizi ya leo kutoka Gaza ndiyo ya kwanza kutokea tangu kuanza wimbi jipya la maandamano tarehe 30 Machi. Haijajulikana bado ni kundi gani limehusika na mashambulio hayo dhidi ya Israel hata ingawa Hamas na Kundi la Islamic Jihad wamepongeza kitendo hicho. Waziri Mkuu wa Israel, Benjamin Netanyahu amelaani mashambulizi hayo kuilenga jamii ya Waisraeli kutokea kwenye Ukanda Gaza na amewalaumu wanamgambo wa Hamas kwa kuchochea vurugu na hali ya wasiwasi.

Waziri mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu (picture-alliance/AP Photo/M. Kahana)

Waziri mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu

Msemaji wa jeshi la Israel Jonathan Conricus amewaambia waandishi wa habari kwamba mashambulizi hayo ya roketi na mizinga ni makubwa ukilinganisha na vita vya mwaka 2014 hali kadhalika lilivyokuwa jibu la Israeli. Msemaji huyo wa jeshi la Israel ameelezea kwamba wameyashambulia malengo zaidi ya 30 ya kijeshi ya mashirika ya kigaidi.

Wakati huo huo mashua iliyokuwa na wanaharakati 20 wa Kipalestina waliokuwa wakijaribu kuvunja marufuku ya miaka 11 katika pwani ya Gaza ilizuiwa na vikosi vya Israeli kwa mujibu wa mratibu wa maandamano hayo.

Wanaharakati wa Kipalestina wanaopinga marufuku ya Israel katika pwani ya Gaza (picture-alliance/ZumaPress/M. Ajour)

Wanaharakati wa Kipalestina wanaopinga marufuku ya Israel katika pwani ya Gaza

Israeli imesema kutokana na sababu za usalama inazizuia boti zote kutoka Gaza kuvuka eneo la uvuvi lililowekewa marufuku kwa umbali wa kilomita kadhaa. Hapo awali wavuvi wa Gaza walipigwa risasi na majeshi ya Israel kwa sababu ya kuivunja amri hiyo. Mmoja wa waandaaji wa maandamano hayo, Adham Abu Selmeya, amesema manowari za kijeshi nne za Israel zilitumika kuyazuia maandamano ya mashua maili tisa kutoka pwani.

Mvutano katika Ukanda wa Gaza umefikia kiwango cha juu katika wiki za hivi karibuni. Wapalestina zaidi ya 100 waliuawa na majeshi ya Israeli wakati wa maandamano makubwa yaliyofanyika mpakani mnamo mwezi Machi.

Eneo la Ukanda wa gaza linakumbwa na hali mbaya ya kiuchumi, kutokana na uharibifu wa miundombinu uliosababishwa na vita vilivyotokea mara tatu kati ya Wanamgambo wa Hamas huko Gaza na Israeli na  pia kuna ukosefu mkubwa wa bidhaa.

Mwandishi:Zainab Aziz/DPA/RTRE/DPAE

Mhariri:Mohammed Abdul-Rahman

Matangazo

Unaweza kusikiliza matangazo yetu hapa

Kusikiliza matangazo ya Idhaa ya Kiswahili ya DW, tafadhali bonyeza alama ya spika ya masikioni hapo chini, na kuwasiliana nasi, tafadhali tuandikie moja kwa moja kupitia: kiswahili@dw.com