Nepal yasubiri kwa hamu kuondolewa kwa utawala wa kifalme na kuanzishwa upya kwa jamhuri ya kidemokrasia | Matukio ya Kisiasa | DW | 28.05.2008
 1. Inhalt
 2. Navigation
 3. Weitere Inhalte
 4. Metanavigation
 5. Suche
 6. Choose from 30 Languages
Matangazo

Matukio ya Kisiasa

Nepal yasubiri kwa hamu kuondolewa kwa utawala wa kifalme na kuanzishwa upya kwa jamhuri ya kidemokrasia

Nepal inajiandaa kwa mabadiliko makubwa yatakayoingia kwa historia ya nchi hiyo

Mmoja wa wanachama wa baraza la kikatiba nchini Nepal akiwa amevalia mavazi ya kitamaduni.

Mmoja wa wanachama wa baraza la kikatiba nchini Nepal akiwa amevalia mavazi ya kitamaduni.

Baraza jipya la wanasheria lenye wafuasi wengi wa falsafa ya Mao linapanga kuondoa miaka 240 ya utawala wa kifalme na kuanzisha jamhuri ya kidemokrasia ya Nepal.


Hata hivyo kumekuwa na mabishano makali miongoni mwa waasi hao wa zamani na vyama vikuu vya kisiasa kuhusu kiongozi atakaekuwa rais wa kwanza wa Taifa la Nepal.


Wanasiasa wa Nepal tayari wamewasili katika kikao hicho cha kihistoria kinachotarajiwa kushuhudia wanasheria wakipiga kura ya kuundoa utawala wa kifalme katika ardhi ya Nepal.


Akiingia katika jumba la mkutano waziri wa amani wa Nepal Ram Chandra ameambia wanahabari kwamba nchi hiyo itabadilishwa na kufanywa jamhuri ya kidemokrasia na kwamba mfalme wake ataondolewa ili nafasi hiyo ichukuliwe na rais.


Wafuasi wa falsafa ya Mao ambao wamejaribu kwa miaka 10 kuundoa utawala wa kifalme nchini humo walishinda viti vingi zaidi vya ubunge katika uchaguzi uliofanyika mwezi uliopita.


Mkutano wa leo unafanyika kufuatia mkataba wa amani uliotiwa sahihi mwaka wa 2006 kati ya vyama vya kisiasa na kundi hilo la waasi.


Kulingana wafuasi wa falsafa ya Mao Mfalme Gyanendra atapewa siku 7 -15 aondoke katika kasri ya kifalme mjini Kathmandu.


Jiji kuu la Nepal limejaa waandamanaji wanaosubiri kwa hamu kutangazwa kwa taifa jipya la Nepal na kumalizika kwa utawala wa kifalme.


Ripota wa shirika la habari la AFP ambaye yumo jijini humo amesema polisi wamelazimika kutumia vitoa machozi kwa waandamanaji hao wanaoshinikiza kuondolewa kwa Mfalme Gyanendra.


Licha ya kukatazwa kujumuika nje ya jengo ambalo tume mpya ya kuunda katiba inatarajiwa kukutana waandamanaji walikusanyika wakisherehekea siku ya kwanza ya Taifa la Nepal.


Utawala wa ufalme wa Nepal umekuwa ukikabiliwa na matatizo mbali mbali tangu wakati wa Prithvi Narayan Shah ambaye ni wakwanza katika jamii ya Shah miaka 240 iliyopita.


Kulingana na mwanahistoria Manjushree Thapa tangu alipofariki Mfalme Narayan Shah mwaka wa 1775, Nepal imekuwa ikitawaliwa na wafalme ambao walikuwa wadogo au wasiofaa kuongoza au wendawazimu, au labda vyote vitatu.


Wafalme wa zamani waliabudiwa na wafuasi wao kama miungu ya Ki-hindu na walikuwa na tabia za kuoa bibi wengi na kuzaa watoto chungu nzima ambao baadaye walikuwa wakizusha vita vya kung'ang'ania ufalme.


Mtaalamu wa historia za kifalme Sanu Bhai Dangol amesema wengi wa wafalme hawakufa vifo vya kawaida.


Karne moja baada ya ufalme wa Nepal kukumbwa na masaibu mengi utawala wa jamii ya Shah ulijikuta ukishirikiana na kabila lengine lenye siasa kali la Ranas.


Baada ya karne ya ishirini jamii ya Shah ilikuwa tayari imewekwa mikononi mwa ile ya Ranas maharajas ambao walikuwa wamejitangaza mawaziri wakuu.


Ranas walichukua uongozi na kuipatia wakati mgumu jamii ya Shah hadi mwaka wa 1950 wakati Mfalme Tribhuvan alidanganya anafunga safari ya kuenda kuwinda kumbe alikuwa anaelekea India kuanza maisha mapya.


Mfalme huyo alimuacha nyuma mjukuu wake Gyanendra, ambaye alikabidhiwa ufalme mara moja na wa-Ranas waliokuwa na nia ya kumtumia kwani alikuwa angali mchanga.


Majadiliano kati ya jamii ya Shah, ya Ranas na vyama vya kisiasa yalipelekea kurejea kwa mfalme Trbhuvan mwaka mmoja akiwa angali mfalme kikatiba; Ubembei na demokrasia ambao ulipelekea kupinduliwa kwa ufalme huo mwaka wa 1960.

Jamii ya Shah ilikumbwa na mizozo zaidi mwaka wa 2001. Mwanae Mfalme Dipendra ambaye alikuwa anapenda kutumia bunduki na ambaye alikuwa amekatazwa kumuua mwanamke aliekuwa amempenda aliamua kunywa pombe na madawa mengine ya kulevya katika sherehe zilizokuwa zinafanyika ndani ya kasri. Baadaye aliwapiga risasi na kuwauwa watu tisa katika jamii ya kifalme akiwemo Mfalme Birendra alikuwa anapendwa na wengi. Baada ya kuwamaliza wote aligeuza bunduki na kujitoa uhai.


Janga hilo lililopewa jina "palace massacre" lilipelekea kuanzishwa kwa utawala wa Gyanendra nduguye Mfalme alieuwawa. Gyanedra hakupendwa na wengi kwani alihusishwa na njama iliyopelekea kuuwawa kwa watu tisa katika kasri ya mfalme.


Mfalme huyo alichukiwa zaidi pale alipochukua mamlaka kamili mwaka wa 2005 kwa nguvu akidai kwamba anajaribu kukabiliana na wafuasi wa falsafa ya Mao.


Utawala wake ulichukua miezi 14 hadi pale vyama vya kisiasa na waasi wa kundi la Maoist walipomlazimisha aondoke mamlakani Aprili 2006.

Isitoshe mwanae Paras ambaye alikuwa anatarajiwa kuchukua ufalme baada yake alikuwa anashutumu kwa kuhusika katika ufyetulianaji risasi, kusababisha ajali za barabarani na kutoweka na pia kujihusisha na wanawake wengi kimapenzi.


Paras aliugua ugonjwa wa moyo mwaka jana akiwa na umri wa miaka 36.


Gyanendra na mwanae sasa wanatarajiwa kuanza kufikiria jinsi watakavyoishi kama raia wa kawaida wa Nepal kwani wafuasi wa falsafa ya Mao wametishia kuwapatia adabu kali iwapo watakataa kuondoka mamlakani kwa amani.

 • Tarehe 28.05.2008
 • Mwandishi Mwakideu, Alex
 • Chapisha Chapisha ukurasa huu
 • Kiungo https://p.dw.com/p/E7nc
 • Tarehe 28.05.2008
 • Mwandishi Mwakideu, Alex
 • Chapisha Chapisha ukurasa huu
 • Kiungo https://p.dw.com/p/E7nc
Matangazo

Unaweza kusikiliza matangazo yetu hapa

Kusikiliza matangazo ya Idhaa ya Kiswahili ya DW, tafadhali bonyeza alama ya spika ya masikioni hapo chini, na kuwasiliana nasi, tafadhali tuandikie moja kwa moja kupitia: kiswahili@dw.com