1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Ndovu na faru huenda wakapungua Tanzania

3 Machi 2021

Jumatano ni siku ya Wanyamapori Duniani, lakini wataalam Tanzania wanaonya kuhusu uwezekano wa kupungua wanyama kama ndovu na faru iwapo juhudi za kukabiliana na vitendo vya ujangili hazitaratibiwa kwa uangalifu.

https://p.dw.com/p/3q9I9
Afrika Savanne Elefanten
Picha: Zoonar.com/David Freigner/picture alliance

Wanyama hao ambao ni sehemu tu ya wale wengi wanaoendelea kuzipamba mbuga nyingi wamekuwa wakiwindwa mara kwa mara ya makundi yanayaoendesha genge la ujangili wanaotumia masoko yaliyoko mashariki ya mbali na barani Asia kwa ajili ya kujinufaisha kifedha.

Ingawa takwimu za serikali ya Tanzania zilizotolewa katika miaka za hivi karibuni zinaonyesha idadi ya wanyama hao imeongezeka, lakini hata hivyo, wasiwasi wa kupungua kwao ni mkubwa mno kutokana na mbinu mpya zinazoendesha na magenge hayo.

Breitmaulnashorn
Faru ni miongoni mwa wanyama wanaohofiwa kupungua TanzaniaPicha: Getty Images/AFP/T. Karumba

Kusambaratisha masoko ni njia bora ya kukabiliana na ujangili

Kulingana Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Maliasili na Utalii, Dokta Allan Kijazi wimbi la vitendo vya ujangili limekuwa likidhibitiwa lakini hata hivyo, baadhi yao wamekuwa wakijipenyeza kutekeleza jinai hizo kwa kutumia mbinu mpya.

Mtaalamu wa masuala ya wanyamapori wa Mfuko wa Uhifadhi wa Mazingira Duniani (WWF), Profesa Noah Sitaki anasema njia rahisi inayoweza kuleta ushindi katika vita ya kukabiliana na vitendo vya kijangili ni kubinya na kusambaratisha masoko yote yanayotumika kusambaza bidhaa zitokanazo na wanyama hao.

Tanzania yaimarisha vita dhidi ya ujangili

Ripoti moja ya serikali iliyotolewa miaka ya hivi karibuni inaonyesha kuwa idadi ya faru ambao ni aina ya viumbe iliyoko hatarini kutoweka iliongezeka kutoka wanyama 15 hadi 167, hii ikiwamo wale walioingizwa nchini kutoka Afrika Kusini.

Siku hii inaadhimishwa wakati sekta ya utalii inaendelea kuporomoka

Hata hivyo, hivi karibuni kulizuka mjadala mpya kuhusu idadi ya tembo nchini Tanzania, baada ya mbunge mmoja kudai bungeni kuwa idadi yao imeongezeka maradufu tangu Rais John Magufuli alipoingia madarakani, hoja ambayo hadi sasa bado haijapata majibu ya moja kwa moja.

Ama, wakati Jumatano kukiadhimishwa Siku ya Wanyamapori duniani na siku hii inaadhimishwa katika wakati ambapo sekta ya utalii imeendelea kuporomoka kutokana na janga la maambukizi ya virusi vya corona.

Mataifa mengi yanayotegemea utalii kama njia mojawapo ya kujiingizia mapato ya kigeni yanatarajiwa kurekodi anguko kubwa la mapato hayo kutokana na kupungua kwa idadi ya watalii.