Ndoto ya Leicester City yaendelea | Michezo | DW | 12.04.2016
  1. Inhalt
  2. Navigation
  3. Weitere Inhalte
  4. Metanavigation
  5. Suche
  6. Choose from 30 Languages

Michezo

Ndoto ya Leicester City yaendelea

Meneja wa viongozi wa ligi hiyo Leicester City Claudio Ranieri alibubujikwa na machozi baada ya kufurahishwa na vijana wake walipoitandika Sunderland kwa mabao 2-0

Ushindi huo uliongeza uwezekano wa timu hiyo kutawazwa mabingwa wa Premier League kwa mara ya kwanza katika historia ya timu hiyo, baada ya kufungua mwanya wa pointi 7. Alikuwa Jamie Vardy aliyeipa ushindi Leicester kwa kupachika mabao mawili muhimu jana Jumapili.

Na Tottenham Hotspurs iliyoko katika nafasi ya pili ilipachika mabao matatu dhidi ya Manchester United jana Jumapili, kipigo ambacho kina maana Leicester imejihakikishia kuwamo katika timu nne za juu ambazo zitashiriki katika michezo ya Champions League msimu ujao.

Kocha wa Manchester United Louis van Gaal amesema kwamba hajutii kutochukua kazi ya kuifunza Tottenham Hotspurs baada ya timu hiyo ya mjini London kuchafua matumaini ya timu yake kucheza katika Champions League jana.

Arsenal nayo imepoteza mwelekeo baada ya kulazimisha sare ya mabao 3-3 dhidi ya West Ham United siku ya Jumamosi.

Kocha wa Liverpool Jurgen Klopp anaamini kijana chipukizi Divock Origi yumo mwanzoni mwa kitu muhimu baada ya kupachika mabao mawili katika ushindi wa mabao 4-1 dhidi ya Stoke City jana Jumapili. Klopp anahisi Origi ataimarika siku hadi siku, akisema yuko katika njia nzuri , na hii ni msingi mzuri na sasa watafanyakazi kwa pamoja kufikia lengo lake.

La Liga: Barca yateleza

Katika La Liga nchini Uhispania Barcelona iliteleza tena wiki hii na kupunguza mwanya wa pointi kileleni hadi pointi tatu baada ya kugaragazwa kwa kipigo cha bao 1-0 dhidi ya Real Sociedad.

Atletico Madrid na Real Madrid sasa zinainyemelea Barcelona zikitengana kwa pointi tatu na nne kwa Real. Real Madrid iliirarua Eibar kwa mabao 4-0 na Atletico Madrid iliizaba Espanyol kwa mabao 3-1.

Mwandishi: Sekione Kitojo / rtre / afpe / dpae / ZR
Mhariri:Iddi Ssessanga

Matangazo

Unaweza kusikiliza matangazo yetu hapa

Kusikiliza matangazo ya Idhaa ya Kiswahili ya DW, tafadhali bonyeza alama ya spika ya masikioni hapo chini, na kuwasiliana nasi, tafadhali tuandikie moja kwa moja kupitia: kiswahili@dw.com