1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Ndege ya shirika la ndege la Malaysia yatoweka angani

9 Machi 2014

Wakati wa hatari zaidi kwa safari za ndege ni wakati wa kuruka na kutua. Ni mara chache matukio yanatokea wakati ndege inapaa hewani maili saba kutoka ardhini.

https://p.dw.com/p/1BMMF
Großbritannien Luftfahrt Messe in Farnborough Airbus A380
Ndege ya shirika la ndege la Malaysia ikiwa anganiPicha: dapd

Kwa hiyo kupotea kwa ndege ya shirika la ndege la Malaysia wakati ikiwa angani siku ya Jumamosi asubuhi katika bahari ya kusini mwa China kumesababisha wataalamu wa safari za anga kushuku kuwa chochote kilichotokea kimetokea kwa haraka na rubani wa ndege hiyo hakupata muda wa kutoa taarifa ya tahadhari.

Inaweza kuwachukua wachunguzi miezi kadhaa , iwapo sio miaka , hadi kujua kile kilichoipata ndege hiyo chapa Boeing 777 ikisafiri kutoka mji mkuu Kuala Lumpur kwenda Beijing.

Malaysia Airlines Flug
Ubao unaoashiria ndege zinazowasiliPicha: picture alliance/AA

Tukio huenda lilitokea kwa ghafla

"Katika wakati huu wa mwanzo, tunaangalia zaidi kuhusu taarifa ambazo hatuzijui," amesema Todd Curtis, mhandisi wa zamani wa masuala ya usalama aliyekuwa akifanya kazi na shirika la Boeing katika ndege za shirika hilo chapa 777 zenye umbo pana na hivi sasa ni mkurugenzi wa wakfu wa Airsafe.com.

Iwapo kulikuwa na hitilafu ndogo za kiufundi - ama hata kama kulitokea kitu kingine kikubwa zaidi kama kuzimika kwa injini zote za ndege, rubani angeweza kupata muda wa kutoa taarifa za kuomba msaada.

Kushindwa kupiga simu, "kuna maana kwamba kuna kitu kilitokea kwa ghafla na kwa nguvu sana," amesema William Wadlock, ambaye anafundisha masuala yanayohusu uchunguzi wa ajali katika chuo kikuu cha safari za anga cha Embry-Riddle mjini Prescott, Ariz.

Shirika la ndege la Malaysia limesema kuwa linahofia hali mbaya zaidi baada ya ndege yake hiyo kupotea, na shirika hilo linafanyakazi kwa pamoja na kampuni ya Marekani ambayo inashughulikia zaidi maafa.

Flugzeugabsturz Malaysia
Ndugu wa abiria waliokuwa katika ndege ya Malaysia wakisubiri kupata taarifaPicha: Reuters

"Katika kuhofia hali mbaya zaidi, mtaalamu wa kushughulikia utafutaji wa maafa kama hayo kutoka Atlanta, Marekani atalisaidia shirika hilo la ndege la Malaysia katika wakati huu muhimu, shirika hilo limesema.

Marekani inasaidia katika msako

Ndege hiyo iliyokuwa imebeba abiria 227 na wafanyakazi 12 inafikiriwa kuwa imeanguka katika pwani ya Vietnam siku ya Jumamosi, baada ya kupoteza mawasiliano na waongoza ndege katika pwani ya mashariki ya Malaysia.

Marekani inatuma wafanyakazi wa shirika la FBI na wataalamu kusaidia kufanya uchunguzi juu ya kupotea kwa ndege hiyo, linaripoti gazeti la Los Angeles Times.

Kwa mujibu wa LA Times , wafanyakazi wa shirika la FBI watasaidia kuchunguza video kutoka uwanja wa ndege wa Kuala Lumpur kupata picha za wasafiri waliosafiri kwa ndege hiyo ambao wanaweza kuangalia katika data za shirika hilo katika kitengo cha ugaidi.

Meli za Vietnam na ndege zinazoitafuta ndege hiyo iliyopotea hawajagundua mabaki ya ndege mahali ambapo waliona kuvuja kwa kiasi kikubwa cha mafuta.

Malayis Airlines / Absturz / Ölspuren
Mafuta yaliyovuja baharini yanayoshukiwa kuwa ni kutoka ndege hiyoPicha: Reuters

Mlolongo wa meli za kimataifa na ndege umekuwa ukichunguza eneo la maji kati ya Malaysia na Vietnam ili kupata ishara ya ndege hiyo.

waligundua kiasi kikubwa cha mafuta yaliyovuja jana Jumamosi, ambayo maafisa wanasema huenda ni kutoka katika ndege hiyo.

Mwandishi: Sekione Kitojo / ape / dpae

Mhariri: Caro Robi