1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Nchi zinazoendelea zataka kuongoza Benki Kuu ya Dunia

21 Machi 2012

Waziri wa fedha wa Nigeria Ngozi Okonjo-Iweala na waziri wa zamani wa fedha wa Colombia Jose Antonio Ocampo wanatarajiwa kutajwa kama watu waliopendekezwa kugombea nafasi ya kuiongoza Benki Kuu ya Dunia.

https://p.dw.com/p/14OQY
Benki kuu ya dunia
Benki kuu ya duniaPicha: picture-alliance/dpa

Taarifa za kupendekezwa kwa Okonjo-Iweala na Ocampo, ambao wana ujuzi mkubwa wa masuala ya uchumi na diplomasia, zinaleta changamoto kwa Marekani kwani hapajawahi kuwa na mtu wa kuwania nafasi ya kuiongoza benki kuu ya dunia asiyetoka nchini humo. Lakini inatarajiwa kwamba mtu atakayechukua nafasi ya Robert Zoellick, ambaye kwa sasa ndiye rais wa benki kuu ya dunia, atatokea Marekani. Hii ni kwa sababu Marekani inaungwa mkono na nchi nyingi, hasa zile za Ulaya. Zoellick ataacha madaraka yake mwezi Juni mwaka huu, pale ambapo muhula wake utakapomalizika.

Marekani imekuwa ikishikilia urais wa Benki Kuu ya Dunia tangu kuanzishwa kwa taasisi hiyo ya fedha baada ya vita vikuu vya pili vya dunia. Kwa upande mwingine, kiongozi wa mfuko wa kimataifa wa fedha IMF daima amekuwa akitokea barani Ulaya.

Changamoto kwa Marekani

Ijumaa hii ndiyo itakuwa siku ya mwisho ya kuwasilisha mapendekezo ya watu wa kuiongoza benki kuu ya dunia. Utawala wa Rais Barack Obama wa Marekani umesema kwamba utakuwa umekwishatoa pendekezo lake hadi kufikia siku hiyo.

Rais wa Benki Kuu ya Dunia, Robert Zoellick
Rais wa Benki Kuu ya Dunia, Robert ZoellickPicha: dapd

Kwa muda mrefu, nchi zinazoendelea na zile zinazoinuka kiuchumi zimekuwa zikitaka kubadili mfumo wa Benki Kuu ya Dunia na Mfuko wa Kimataifa wa Fedha IMF kuongozwa na Marekani na nchi za Ulaya. Lakini mpaka sasa nchi hizo zimeshindwa kuungana ili kubadili hali hiyo.

Bodi ya Benki Kuu ya Dunia kufikia uamuzi mwezi ujao

Vyanzo vitatu vya habari vimesema kwamba Ocampo, ambaye sasa ni Professa katika chuo kikuu cha Columbia nchini Marekani, atapendekezwa rasmi na Brazil. Chanzo kimoja cha habari kimesema kwamba Okonjo-Iweala angewza kupendekezwa leo, wakati vyanzo vingine viwili vimeeleza kwamba angependekezwa Ijumaa.

Mwaka uliopita, Ngozi Ikonjo-Iweala aliachia nafasi yake ya mkurugenzi mtendaji wa Benki Kuu ya Dunia ili kuchukua wadhifa wa uwaziri wa fedha nchini mwake Nigeria. Yeye pamoja na Ocampo, ambaye alikuwa naibu katibu mkuu wa masuala ya uchumi na ya kijamii katika Umoja wa Mataifa, wataungana na Jeffery Sachs, ambaye ni mtaalamu wa masuala ya uchumi kutoka Marekani, katika orodha ya waliopendekezwa kuwa rais wa benki kuu ya dunia.

Majina ya waliopendekezwa yanawasilishwa kwa bodi ya benki kuu ya dunia inayoundwa na nchi 25. Bodi hiyo imeeleza kwamba itafikia uamuzi juu ya rais mpya wa benki kuu ya dunia mwezi ujao.

Mwandishi: Elizabeth Shoo/RTRE

Mhariri: Mohammed Abdul-Rahman