1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Nchi zenye nguvu duniani kujadili mkataba wa nyuklia wa Iran

2 Aprili 2021

Nchi zenye nguvu duniani pamoja na Iran, zitakutana Ijumaa kwa njia ya video, kujadili uwezekano wa Marekani kurudi kwenye mkataba wa kimataifa kuhusu mpango wa nyuklia wa Iran.

https://p.dw.com/p/3rWAM
Hassan Rouhani Iran
Picha: picture-alliance/AP Images/E. Naroozi

Marekani imekaribisha mkutano huo ambao ulitangazwa na Umoja wa Ulaya siku ya Alhamisi.

Hapo jana Alhamisi, msemaji wa wizara ya mambo ya nje ya Marekani Ned Price, alisema wako tayari kutafuta njia ya kurudi katika mkataba huo kulingana na ahadi zilizowekwa chini ya shirika linalofuatilia utekelezaji wake JCPOA na kwa kuhakikisha Iran pia inatimiza ahadi zake.

"Marekani inazungumza na washirika kuhusu njia bora zaidi ya kutimiza hilo ikiwemo kupitia misururu ya hatua za mwanzo", amesema Price.

"Tumekuwa tukitafakari njia mbalimbali za kufanya hili, ikiwemo mazungumzo ya moja kwa moja na washirika wetu wa Ulaya." Price ameongeza.

Mkutano wa Ijumaa utakuwa wa kwanza wa halmashauri ya pamoja ya utekelezaji wa mkataba wa Iran kuhusu nyuklia tangu Rais Joe Biden alipochukua madaraka.

Iran ilitishia kuanza kurutubisha madini ya urani baada ya Marekani kujitoa kwenye mkataba huo.
Iran ilitishia kuanza kurutubisha madini ya urani baada ya Marekani kujitoa kwenye mkataba huo.Picha: picture-alliance/AP Photo/V. Salemi,

Wawakilishi kutoka China, Ufaransa, Ujerumani, Urusi, Uingereza pamoja na Iran ambazo ndizo nchi zilizosalia kwenye mkataba huo baada ya Marekani kujitoa, watashiriki.

Wawakilishi hao watajadili pia namna washirika wote kwenye mkataba huo watahakikisha utekelezaji wake kamili.

 Mkutano huo utakaoongozwa na mwanadiplomasia wa ngazi ya juu wa Umoja wa Ulaya Enrique Mora kwa niaba ya mkuu wa sera za nje wa Umoja wa Ulaya Josep Borrell, pia utashirikisha shirika ambalo limekuwa likihusika na utekelezaji wa mkataba huo JCPOA, lakini ambalo limekuwa chini ya kitisho tangu rais Donald Trump alipoitoa Marekani kwenye mkataba.

Hata hivyo Biden ameahidi kuirudisha Marekani kwenye mkataba huo, lakini kwa masharti kwamba Tehran ianze kuheshimu ahadi zake ambazo iliancha kutekeleza kama kulipiza kisasi dhidi ya uamuzi wa Trump.

Rais wa Marekani Joe Biden
Rais wa Marekani Joe BidenPicha: Evan Vucci/AP Photo/picture alliance

Wizara ya mambo ya nchi za nje ya Marekani ilitangaza pia kwamba imeiruhusu Iraq muda wa kununua gesi kutoka Iran.

Muda huo wa siku 120 unajiri kabla ya mazungumzo ya kimkakati kati ya Washington na Baghdad ambao umepangwa kufanyika kwa njia ya video Aprili 7.

Mapema mwezi uliopita, kiongozi mkuu wa kidini wa Iran Ayatollah  Ali Khamenei alisema nchi yake iko tayari kuanza tena kuheshimu kikamilifu ahadi zake kwa JCPOA ikiwa Tehran itahisi Washington imeheshimu ahadi zake.

Mkataba huo ulisainiwa Vienna mwaka 2015 kati ya Iran, Marekani, China, Urusi, Ujerumani, Ufaransa na Uingereza.

Ulikusudiwa kuzuia taifa hilo ambalo ni Jamhuri ya Kiislamu kupata zana za nyuklia kwa kuiwekea vikwazo vikali kwenye mpango wake wa nyuklia na kuilazimisha kusalia kuwa taifa löa kiraia na lenye amani.

(AFPE)