Nchi za SADC zatakiwa kupunguza utegemezi wa kigeni | Matukio ya Afrika | DW | 18.08.2014
  1. Inhalt
  2. Navigation
  3. Weitere Inhalte
  4. Metanavigation
  5. Suche
  6. Choose from 30 Languages
Matangazo

Matukio ya Afrika

Nchi za SADC zatakiwa kupunguza utegemezi wa kigeni

Rais Robert Mugabe wa Zimbabwe amezitaka nchi za kusini mwa Afrika kupunguza utegemezi wao wa msaada wa kigeni na kutumia vizuri rasimali zao za asili kama vile madini na ardhi ili kukuza uchumi.

Rais Robert Mugabe Mwenyekiti mpya wa jumuiya ya SADC.

Rais Robert Mugabe Mwenyekiti mpya wa jumuiya ya SADC.

Rais Robert Mugabe wa Zimbabwe amezitaka nchi za kusini mwa Afrika kupunguza utegemezi wao wa msaada wa kigeni na kutumia vizuri rasimali zao za asili kama vile madini na ardhi ili kukuza uchumi kwa kutegemea zaidi usafirishaji nje wa bidhaa badala ya mali ghafi. Wakati wa ufunguzi wa mkutano huo wa viongozi wa nchi wanachama 15 wa jumuiya ya SADC Mugabe amesema kuendelea kwao na utegemezi wa kupindukia wa nia njema ya washirika wao kunahatarisha umiliki wao wa jumuiya hiyo ya ishirikiano wa maendeleo ya SADC.

Amekaririwa akisema rasilmali zao zilizojaa chekwa chekwa badala ya kuuzwa kama mali ghafi kwa bei ya chini ziongezewe thamani kwa kufanywa bidhaa za kusafirishwa nje.

Kiongozi huyo mwenye umri wa miaka 90 amekabidhiwa uwenyekiti wa jumuiya ya SADC na Rais Peter Mutharika wa Malawi baada ya kutengwa kushika nyadhifa za madaraka katika jumuiya hiyo kwa takriban muongo mzima.Pia anatazamiwa kuungoza Umoja wa Afrika kuanzia mwakani.

Mwanamapinduzi aliegeuka dikteta

Rais Robert Mugabe wa Zimbabwe.

Rais Robert Mugabe wa Zimbabwe

Mugabe ameitawala Zimbawe tokea nchi hiyo ijipatie uhuru wake hapo mwaka 1980 lakini mfululizo wa matatizo ya kiuchumi,chaguzi ziliokuwa na kasoro na ukandamizaji wa kikatili wa upinzani umepelekea nchi hiyo kuwekewa vikwazo na Umoja wa Mataifa na kumfanya mwanamapinduzi huyo wa zamani kuwa dikteta wa mataifa ya magharibi.

Alikuwa ni kiongozi pekee kutoka nchi za kusini mwa Afrika ambaye hakualikwa kuhudhuria Mkutano wa Kilele kati ya Marekani na Afrika uliofanyika mjini Washigton mapema mwezi huu ambao ulijumuisha karibu viongozi wakuu wa nchi 45 wa bara hilo.

Kuaminika kwa SADC mashakani

Viongozi wa SADC katika mojawapo ya vikao vyake

Viongozi wa SADC katika mojawapo ya vikao vyake.

Siku chache kabla ya kufanyika mkutano huo wa kilele wa SADC mashirika ya haki za binaadamu yakiwemo ya Human Rights Watch lenye makao yake Marekani na Amnesty International la Uingereza pamoja na shirika la Wanasheria wa Haki za Binadamu la Zimbabwe wamesema kuaminika kwa chombo hicho kuko hatarini iwapo halitoshughulikia suala la haki za binaadamu miongoni mwa nchi wanachama wake ukiwemo ukamataji wa wanaharakati wa kisiasa na waandishi wa habari.

Wamezitaja Angola,Malawi na Zambia kwa kuhusika na ukiukaji wa haki za binadamu na kuishutumu serikali ya Zimbabwe kwa kuburuza miguu katika kuwafikisha mahakamani wahusika wa ghasia za kisiasa wakati wa chaguzi zilizopita na kushutumu hali ya siri ilioko katika haki za machimbo ya madini pamoja na migodi ya almasi yenye kuzalisha faida kubwa nchini humo.

Mugabe hakuzungumzia madai hayo katika hotuba yake bali amesema jumuiya hiyo inajivunia rekodi nzuri katika suala la amani usalama na demokrasia.Suala la usalama na maendeleo ya kijamii na uchumi yamepewa kipau mbele katika mkutano huo unaomalizika leo.

Mwandishi : Mohamed Dahman/Reuters/AFP

Mhariri : Yusuf Saumu