1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Nchi za IGAD zautaka Umoja wa Mataifa kuiwekea vikwazo Eritrea.

21 Mei 2009

Eritrea inalaumiwa kwa kuwapa silaha pamoja na mafunzo wanamgambo wa al Shabaab nchini Somalia.

https://p.dw.com/p/Hupo
Wanamgambo nchini Somalia.Picha: AP

Nchi majirani wa Somalia zimeuomba umoja wa mataifa kuweka vizuizi vya angani, kwenye bahari pamoja na ardhini, katika taifa hilo la pembe ya Afrika na pia kuiwekea vikwazo Eritrea kwa kuwaunga mkono wanamgambo wa kiislamu walio na nia ya kuiangiusha serikali ya Somalia.

Kundi la wanamgambo la al Shabaab pamoja na lile la Hizbul Islam yalitekeleza uvamizi katika mji wa Mogadishu wiki mbili zilizopita, yakiwa na lengo ya kuitimua mamlakani serikali dhaifu inayoongozwa na rais Sheikh Sharif Sheikh Ahmed, mwislamu mwenye mtazamo wa ukadirifu na ambaye wakati mmoja alikuwa mshirika wa wanamgambo.

Karibu wa mia mbili wengi wao raia wameuawa na zaidi ya wengine mia tano kujeruhiwa tangu mapigano hayo yaanze. Umoja wa mataifa unasema kuwa zaidi ya watu elfu arobaini na tano wameutoroka mji wa Mogadishu kwa muda wa wiki mbili zilizopita

Eritrea imekuwa ikilaumiwa kwa kuwapa silaha pamoja na mafunzo wanamgambo nchini Somalia huku muungano wa nchini za IGAD unaozijumuisha nchi kama Kenya, Ethiopia na Somalia ukisema kuwa Eritrea lazima ilaumiwe.

IGAD sasa imetoa wito kwa baraza la usalama la umoja wa mataifa kuiwekea vikwazo Eritrea bila kukawia, wakati huo huo IGAD, imeutaka umoja wa mataifa kuzuia safari zote za ndege zinaoelekea viwanja vya ndege nchini Somalia isipokuwa zile zinazo tumika kusafirisha misaada na pia kufunga bandari zinazoingia nchini Somalia, ili kuzuia kile ambacho kilnatajwa kuwa sio tu silaha kuingia bali wapiganaji wa kigeni wanaoingia nchini Somalia kujiunga katika vita hivyo.

Serikali ya Sheikh Sharif inayoungwa mkono na wanajeshi elfu nne na mia tatu wa kulinda kutoka muungano wa Afrika hasa kutoka Uganda na Burundi, inadhibiti eneo dogo la mji wa Mogadishu huku wanamgambo wakidhibiti eneo kubwa na kusini na kati kati mwa Somalia.

UN-Gebertreffen in Brüssel - Somalia
Rais wa Somalia Sheikh Sharif Sheikh Ahmed, (kushoto)Picha: AP

Hata hivyo serikali ya Somalia ilipata uungwaji mkono siku ya jumapili baada ya kiongozi wa kundi la Hizbul Islam kujiubga na upande wa serikali pamoja na wapiganaji wake.

Sheikh Sharif ameidhinisha kutumika kwa sheria za kiislamu Sharia, na amekuwa akifanya jitihada za kuboresha uhusiano na makundi ya wanamgambo. Lakini wanamgambio wanasema kuwa Sheihk Sharif anaegemea sana upande wa nchi za Magharibi.

Rais Sheihk Sharif aliingia madarakani mapema mwaka huu kufuatia mchakato wa amani ulioongozwa na umoja wa Mataifa.

Mapigano hayo yaliyoibuka baada ya wanajeshi wa Ethiopia kuingia nchini Somalia mwaka 2006 ili kuwatimua wapiganaji wa mahakama za kiislamu, yamesababisha vifo vya zaidi ya elfu kumi na saba wengi wao raia.

Wanajershi wa Ethiopia waliondoka ,nchini Somalia mwezi Januari mwaka huu lakini katika siku za hivi majuzi kuna madai kuwa wanajeshi hao wamevuka tena mpaka na kuingia nchini Somalia.

Mamilioni ya wasomalia wameyakimbia makwao na sasa wanaishi katika kambi za wakimbizi nchini Kenya , Ethiopia pamoja na katika nchi zingine.

Somalia imekabiliwa na mzozo tangu mwaka 1991 alipong`olewa mamlakani Mohamed Siad Barre.

Mwandishi :Jason nyakundi/DPA

Mhariri : Mohammed Abdul Rahman.