1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Nchi tajiri zalima katika nchi zinazoendelea

12 Agosti 2009

Nchi tajiri zinazidi kuwekeza katika kilimo kwa kukodi ardhi katika nchi zinazoendelea,nchi ambazo mara nyingi hushindwa hata kulisha umma wake. Biashara hiyo ina faida lakini inawaathiri vibaya masikini.

https://p.dw.com/p/J8EX

Orodha ya nchi hizo inachekesha. Sudan imeziruhusu nchi za Ghuba, Misri na Korea ya Kusini kulima katika ardhi ya rutuba.Kuwait imekodi ardhi nchini Cambodia. Misri pia ina mashamba ya ngano na mahindi nchini Uganda. Pakistan nayo ipo tayari kuzikodisha nchi za Ghuba ardhi ya kilimo. Nchi kama China na zile za Ghuba zinataka kuhakikisha usalama wa vyakula vyao kwa kukodi ardhi ya kilimo katika nchi masikini lakini matokeo yake yana madhara makubwa.

Kwa mfano ni mwaka mmoja tu tangu Ethiopia ilipoomba msaada wa chakula kutoka jumuiya ya kimataifa. Kama watu milioni 4 na nusu walihitaji chakula kwa dharura.Nako Somalia zaidi ya watu milioni 3 hawana uwezo wa kujilisha. Watoto waliyokondeana na matumbo yaliyotuna ni picha za umasikini barani Afrika na Asia.

Je, itakuaje kuwa hivi karibuni tu, Ethiopia ilisafirisha Saudi Arabia maelfu ya tani za mchele kutoka mashamba yaliyokodiwa katika nchi ya ukame na nchi iliyo na utajiri wa mafuta? Habari za mara kwa mara, juu ya maafa ya njaa katika nchi za Sahel, zinaambatana vipi na mamilioni ya hekta za mashamba ya ngano yanayolimwa na Libya nchini Mali? Kwanini Tanzania ina matatizo ya kulisha umma wake na wakati huo huo Saudi Arabia imeuziwa hekta 500,000 za ardhi ya kilimo?

Jawabu ni wazi: Hapo kinachohusika ni pesa. Gharama za kuwekeza au kununua ardhi katika nchi zinazoendelea ni kati ya dola bilioni 30 hadi 40 lakini faida inayopatikana ni kubwa zaidi. Ardhi ya kilimo ina thamani na thamani hiyo inazidi kwenda juu. Na ardhi hiyo hununuliwa kule iliko rahisi katika nchi zinazoendelea.

Lakini huo sio ukoloni mambo leo, kwani nchi zinazoendelea zinakubali kufanya biashara hiyo kwa matumaini ya kupata fedha,teknolojia ya kisasa na uwezekano wa kupata nafasi za ajira. Hayo ni matumaini ya muda mfupi na kupotosha.

Kwanini nchi zenye kilimo duniani -na sio zenye njaa tu barani Afrika- hazijatambua kuwa hatimae zinapaswa kuwa na sera endelevu za kilimo badala ya kuendelea kutumaini kwamba kazi hiyo, itafanywa na mwengine kutoka nje? Kama ilivyo kawaida safari hii pia, suluhisho linatafutwa nje, lakini nchi masikini zinaathirika.

Kwanini nchi kama Msumbiji yenye uwezo wa kukidhi mahitaji yake ya chakula haina miundo mbinu ya kisiasa katika sekta ya kilimo na inaagizia chakula kutoka nje?

Kwanini katika nchi kama Kenya iliyoendelea kwa kiasi fulani, mara kwa mara kuna uhaba wa chakula kwa sababu sera zake na uhaba wa miundo mbinu hazisaidii kuipatia nchi hiyo chakula cha kutosha?

Lakini hata nchi za kaskazini pia zina wajibu wake. Nchi hizo zingeweza kupunguza kile kinachoitwa misaada ya kiutu katika nchi zinazoendelea kama nchi hizo tajiri zingesita kupeleka nje shida zao na kuzitumia nchi zinazoendelea kama maeneo ya kujipatia huduma na mali ghafi.

Mhariri: U.Schaeffer /ZPR