1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

NCCR-Mageuzi nayo yateua wagombea urais

George Njogopa7 Agosti 2020

Vyama vya siasa nchini Tanzania vimeendelea kupitisha majina ya wagombea urais katika uchaguzi mkuu wa Oktoba 28 hatua ambayo inaashiria huenda safari hii kukawa na idadi kubwa ya wagombea.

https://p.dw.com/p/3gaw0
Tansania | Mitglied der NCCR-Mageuzi-Partei | Konferenz
Picha: DW/S. Khamis

Chama cha NCCR Mageuzi kimefanya mkutano wake mkuu  maalumu siku ya Ijumaa, kwa ajili ya kumchagua mgombea wa Urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Zanzibar.

Hadi sasa tayari vyama vinne ikiwamo CCM wagombea wake wameshachukua fomu katika Tume ya Taifa ya Uchaguzi NEC na kuacha uwanja kwa vyama vingine ambavyo vinaendelea kujipanga.

NCCR Mageuzi ambacho katika miaka ya hivi karibuni kiliwakaribisha wabunge watatu waliokuwa Chadema kinaendelea na mkutano wake na kinatarajia kupitisha jina moja miongoni mwa wagombea watatu waliojitokeza kuwania nafasi hiyo.

Mkuuu wa idara ya mawasiliano na uenezi kwa umma  wa chama hicho, Edward Simbeye amesema mkutano huo pia utapitisha jina la mgombea wa kiti cha urais kwa Zanzibar ambapo ni mwanachama mmoja tu aliyetokeza kwenye nafasi hiyo.

Tansania | Wahlen 2020 | James Mbatia
Mwenyekiti wa NCCR-Mageuzi James MbatiaPicha: DW/S. Khamis

Suala la maridhiano na ushirikiano kuelekea kwenye uchaguzi huu miongoni mwa vyama vya upinzani limeendelea kujitokeza pia katika mkutano huu. Wimbo huu wa ushirikiano ambao bado haijajulikani namna utakavyopatiwa ufumbuzi imekuwa mada inayotajwa mara zote tangu kuanza kwa mchakato huu wa uchaguzi.

Huku hayo yakiarifiwa, naibu mwenyekiti wa CHADEMA Tundu Lissu ambaye tayari ameteuliwa na chama chake kuwa mgombea wa urais katika uchaguzi ujao, ameitwa katika mahakama ya Kisutu anakokabiliwa na kesi za uchochezi. Mahakama hiyo imemwamuru kufika mahakamani hapo Agosti 31 akiwa na wadhamini wake ili kujua hatma ya kesi yake. Hatua hiyo inakuja baada ya wadhamini hao kushindwa kutokea mahakamani hapo kwa muda mrefu, wakati Lissu akiwa ughaibuni kwa matibabu.

Wakati huohuo, Chama cha ACT Wazalendo kitawatambulisha wagombea wa urais wa pande zote mbili kwa wanachama wake wa Zanzibar siku ya Jumapili

Na George Njogopa/DW Dar es Salaam