1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Nawaz Sharif arejea Pakistan

Josephat Charo10 Septemba 2007

Kurejea kwa Nawaz Sharif nchini Pakistan ni changamoto kubwa kwa rais Pervez Musharaf ambaye anataka kuendelea kuitawala nchi hiyo.

https://p.dw.com/p/CB1S

Waziri mkuu wa zamani wa Pakistan, Nawaz Sharif, amewasili leo nchini Paksitan baada ya kuishi uhamishoni nchini Uingereza kwa miaka saba. Sharif anapania kupambana na rais wa Pakistan, Pervez Musharaf, katika uchaguzi mkuu ujao uliopangwa kufanyika mwishoni mwa mwaka huu nchini humo. Imeripotiwa kwamba rais Musharaf alipanga kumkamata Nawaz Sharif katika uwanja wa ndege wa mjini Islamabad.

Maafisa wa usalama nchini Pakistan wameimarisha usalama katika uwanja wa ndege wa Islamabad na kuwakamata zaidi ya wafuasi 4,000 wa Nawaz Sharif. Alipokuwa akiondoka uwanja wa ndege wa Heathrow nchini Uingereza, Nawaz Sharif alisema lengo lake kubwa ni kuirejesha Pakistan katika utawala wa demokrasia na kuongeza kuwa bila kufanya hivyo nchi hiyo itaendelea kuwa katika hali mbaya.

´Nchi iko katika hali mbaya na naenda kuitoa kutoka hali hiyo sasa. Na nadhani narudi ili nifanye jukumu hilo nchini mwangu kwa sababu nchi leo iko mikononi mwa dikteta wa kijeshi ambaye ameziharibu taasisi zote na amelifanya bunge kuwa chombo cha kuidhinisha ayatakayo na tuna mfumo wa bunge nchini Paksitan ambapo mambo yote yanaamuliwa na rais mwenyewe.´

Kurejea kwa Nawaz Sharif nchini Paksitan ni changamoto kubwa kwa rais Pervez Musharaf ambaye amepoteza umaarufu tangu alipojaribu kumfuta kazi jaji mkuu wa nchi hiyo mnamo mwezi Machi mwaka huu.