1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Nato wajadili mageuzi

Saumu Mwasimba
1 Desemba 2020

Mawaziri wa nchi wanachama wa jumuiya hiyo ya kiusalama wanajadili mapendekezo juu ya mageuzi ya chombo hicho ambapo kinakabiliwa na hali ya baadhi ya wanachama kutoridhika na hali ilivyo sasa

https://p.dw.com/p/3m4nt
Brüssel | NATO Treffen in Brüssel
Picha: Reuters/F. Lenoir

Mawaziri wa mambo ya nje wa nchi 30 wanachama wa jumuiya ya kujihami ya NATO wanajadili kwa mara ya kwanza ripoti mpya ya kitaalamu ambayo imesheheni mapendekezo kadhaa ya mageuzi. Ripoti hiyo imekuja baada ya kuchochewa na mitizamo ya baadhi ya nchi wanachama wa jumuiya hiyo kuhoji uwezo wa chombo hicho katika kutimiza malengo yake.

Kikao cha Jumuiya ya Nato ni cha siku mbili na ndani ya kipindi hicho kikubwa kinachojadiliwa ni mapendekezo lukuki yaliyotolewa kuhusu kuifanyia mageuzi jumuiya hiyo. Mageuzi yanayopendekezwa yanalenga kuuimarisha tena ushirikiano huo wa kiusalama.

Kuuimarisha katika nafasi yake kama jukwaa la ushauri pamoja na kuzuia matumizi ya kura ya turufu au Veto katika suala la kuchukuliwa hatua au uamuzi wa pamoja. Mkutano huu unafanyika baada ya baadhi ya washirika wa muungano huo kuwashutumu wenzao kwa kuwapa jicho la upande au kuwatenga katika maamuzi muhimu ya kiusalama,mfano suala la Uturuki kuvamia kaskazini mwa Syria mwaka jana.

Kombobild Präsident Recep Tayyip Erdogan und Emmanuel Macron
Picha: Adem ALTAN and Ludovic Marin/various sources/AFP

Ni hatua hii iliyowachochea watu kama rais Emmanuel Macron wa Ufaransa kusema kwamba jumuiya hiyo ya Nato inaugua ugonjwa wa kupooza ubongo,kiasi kama mwaka mmoja uliopita. Mawaziri wa mambo ya nje wa NATO pia watajadili kwenye mkutano huu suala la ujumbe wake nchini Afghanistan baada ya Marekani kutangaza kwamba kuna uwezekano ikaondowa wanajeshi wake zaidi nchini humo.

Brüssel NATO-Ministerrat Maas
Picha: DW/Teri Schultz

Tayari waziri wa Ujerumani Heiko Maas ameshasema kwamba anatarajia vikosi vya Marekani nchini Afghanistan vitaendelea kutowa uungaji mkono,lakini pia akatahadharisha kwa kusema

''Mchakato wa amani nchini Afghanistan haupaswi kuhujumiwa kwa kuondowa wanajeshi mapema. Ndio sababu tulilichukulia tangazo la Marekani katika kipindi cha wiki kadhaa zilizopita kwa tahadhari,kwasababu hatukufahamu,ni athari gani litasababisha kwa Taliban. Hii ndio sababu kwanini ni muhimu kwetu kulinda mchakato huu na pia kwa kuzingatia sera ya usalama''

Jumuiya ya Nato ina wanajeshi Afghanistan kwa takriban miaka 20 kufuatia uvamizi wa Marekani katika taifa hilo uliochochewa na mashambulizi ya Septemba 11 mwaka 2001. Ikumbukwe kwamba rais Donald Trump anapanga kupunguza wanajeshi wa Marekani Afghanistan kwa nusu kufikia katikati ya Januari na kubakisha wanajeshi 2500 tu lakini  yapo matumaini miongoni mwa wakosoaji wa mpango huo kwamba mrithi wake Joe Biden atakayeapishwa Januari 20 huenda akabadili mkondo wa suala hilo.