1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

NATO kuipa ulinzi Uturuki

Admin.WagnerD20 Novemba 2012

Nchi wananchama wa jumuiya ya kujihami ya NATO wamekubali kuipa Uturuki silaha za teknolojia ya hali ya juu kwa ajili ya ulinzi wa mpaka wake na Syria.

https://p.dw.com/p/16m9F
Picha: dapd

Wakati huohuo waasi nchini Syria wamesema kuwa wameyateka makao makuu ya jeshi la serikali yaliyo karibu na barabara kuu inayoingia mjini Damascus kwa upande wa kusini.

Mazungumzo juu ya kutolewa kwa vifaa hivyo vifaa hivyo ambavyo lengo lake ni kupambana na kitisho cha uvunjifu wa amani kinachotokea Syria yako katika hatua za mwisho. Waziri wa mambo ya nje wa Uturuki Ahmet Davutoglu amewaambia waandishi wa habari kuwa kazi nzito iko njiani kuja na kwamba mazungumzo yameshafikia hatua ya mwisho.

Ahmet Davutoglu, waziri wa mambo ya nje wa Uturuki akiwa na mwenziwe Guido Westerwelle wa Ujerumani pamoja na Lakhdar Brahimi mpatanishi wa mzozo wa Syria
Ahmet Davutoglu, waziri wa mambo ya nje wa Uturuki akiwa na mwenziwe Guido Westerwelle wa Ujerumani pamoja na Lakhdar Brahimi mpatanishi wa mzozo wa SyriaPicha: picture-alliance/dpa

Davutoglu amesema pia kuwa nchi zinazotoa dhana hizo za ulinzi zinajulikana na kwamba tayari wameshakubaliana nazo na ombi rasmi litatolewa hivi karibuni.

Kwa mujibu wa taarifa nchi hizo ni Marekani, Ujerumani na Uholanzi. Hapo kabla waziri wa ulinzi wa Ujerumani Thomas de Maiziere alizungumzia suala ya kuipa usaidizi huo Uturuki na kusema

Nchini Syria kwenyewe, vikosi vya serikali vilifanya mashambulizi makubwa katika jitihada za kuzuia kuchukuliwa kwa makao ya jeshi lakini hayakuzaa matunda. Hayo yanakuwa makao makuu yaliyokaribu zaidi na mji mkuu wa Damascus kuwahi kutwaliwa na waasi tangu kuanza kwa mzozo huo.

Waasi wa Syria
Waasi wa SyriaPicha: Reuters

Majenerali wa vikosi vya waasi wa makundi ya Ansar al-Islam na Jund Allah wamesema katika tamko lao kuwa wameichukua ngome ya majeshi ya anga karibu na eneo la Hajar al-Aswad baada ya mapigano yaliyodumu kwa siku nne mfululizo.

Wilaya hiyo imekuwa makaazi ya maelfu ya wakimbizi wanaotokea eneo la Syria katika milima ya Golani ambalo linashikiliwa na Israel. Ni eneo ambalo lilikuwa mstari wa mbele katika kuupinga utawala wa Rais Bashar al-Assad siku za mwanzoni mwa maandamano ambayo sasa yamegeuka vita vya wenyewe kwa wenyewe.

Taarifa za hivi karibuni zinaarifu kuwa mabomu mawili yamelipiga jengo la wizara ya habari ya Syria mjini Damascus na kusababisha uharibifu lakini hakuna mtu aliyejeruhiwa. Kituo cha televisheni cha taifa kinaarifu kuwa mashambulizi hayo yamefanywa na magaidi kikiwa na maana kuwa ni waasi.

Mripuko katika mji wa Damascus
Mripuko katika mji wa DamascusPicha: Reuters

Bado hali ya kugawanyika kwa upinzani nchini Syria inaendelea ambapo makundi ya wapiganaji wa kiislamu wenye msimamo mkali katika mji wa Aleppo yametangaza kuukataa muungano mpya wa upinzani ulioundwa hvi karibuni.

Makundi hayo yanayoundwa na watu wenye nguvu na wenye umaarufu ndani ya Aleppo yamesema kuwa yanataka kuunda taifa la kiislamu ndani ya Syria.

Mwandishi: Stumai George/Reuters

Mhariri: Mohammed Abdul-Rahman