1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Nato kuimarisha ulinzi Ulaya mashariki

Abdu Said Mtullya16 Aprili 2014

Katibu Mkuu wa mfungamano wa kijeshi wa NATO, Rasmussen amesema,kwamba mfungamano huo utaimarisha ulinzi katika nchi za Ulaya ya mashariki ili kuikabili hali ya wasiwasi inayotokana na matukio ya nchini Ukraine

https://p.dw.com/p/1Bjly
Katibu Mkuu wa Nato Anders Fogh Rasmussen
Katibu Mkuu wa Nato Anders Fogh RasmussenPicha: Reuters

Rasmussen ameyasema hayo wakati Waziri wa mambo ya nje wa Marekani John Kerry anaelekea Geneva kuhudhuria mkutano juu ya mgogoro wa Ukraine.Kutokana na mgogoro wa nchini Ukraine mfungamano wa kijeshi wa Nato utaimarisha ulinzi katika nchi wanachama za Ulaya mashariki.

Hayo ameyasema Katibu Mkuu wa mfungamano huo Anders Fogh Rasmussen.Akizungumza mjini Brussels bwana Rasmussen alieleza kuwa Nato itaimarisha ulinzi wa angani, majini na wa nchi kavu katika nchi za Ulaya mashariki.

Katibu Mkuu wa NATO Rasmussen amesema hatua hizo zitatekelezwa mara moja lakini hakutoa maelezo ya undani. Bwana Rasmussen pia ameitaka Urusi isimame katika upande wa kuleta suluhisho la mgogoro wa nchini Ukraine.

Suluhisho ni kuzitambua haki za wote

Juu ya mgogoro huo Waziri wa mambo ya nje wa Urusi Sergei Lavrov amesema wakati wa ziara yake nchini Vietnam, kwamba Ukraine inapaswa kuwa na katiba mpya itakayozingatia haki na maslahi ya watu wote wa Ukraine. Waziri Lavrov amesema bila ya kupitisha katiba kama hiyo itakuwa vigumu kwa Ukraine kuutatua mgogoro wake.

Rais Wladimir Putin wa Urusi pia amewasiliana na Kansela wa Ujerumani Angela Merkel juu ya mgogoro wa nchini Ukraine. Rais Putin amemwambia Kansela Merkel kwa njia ya simu kwamba kuongezeka kwa mvutano nchini Ukraine kumeisogeza nchi hiyo kwenye ukingo wa vita vya wenyewe kwa wenyewe.

Mkutano wa Geneva

Katika juhudi za kuutatua mgogoro wa Ukraine, Waziri wa mambo ya nje wa Marekani John Kerry anaelekea mjini Geneva ambako atakutana na mwenzake wa Urusi Lavrov na Waziri wa mambo ya nje wa Ukraine Andriy Deshchytsa.Mkuu wa sera za nje wa Umoja wa Ulaya Cathrine Ashton pia atahudhuri mkutano huo hapo kesho.Hata hivyo wachambuzi wana mashaka iwapo mkutano huo utafanikiwa.

Nchini Ukraine kwenyewe, idara ya usalama ya nchi hiyo imesema mawasiliano iliyoyadakiza yameonyesha itikeli ya mawakala kama wale walioshiriki katika kulichukua jimbo la Krimea mwezi uliopita. Msemaji wa kitengo cha kupambana na ujasusi kwenye idara ya usalama ya Ukraine Vitaly Naida aliwaambia waandishi wa habari kwamba wameweza kuyabainisha hayo kutokana ishara ambazo majasusi hao wa Urusi wanazitumia.

Mwandishi:Mtullya Abdu.afpe,rtre.

Mhariri:Mohammed Abdul-Rahman