Nani ndiye Bosz? Changamoto zinazomkabili | Michezo | DW | 07.06.2017
  1. Inhalt
  2. Navigation
  3. Weitere Inhalte
  4. Metanavigation
  5. Suche
  6. Choose from 30 Languages

Michezo

Nani ndiye Bosz? Changamoto zinazomkabili

"Ntakata kucheza kandanda la kuvutia,” alisema kocha mpya wa Borussia Dortmund Peter Bosz wakati alizinduliwa. Lakini nini kinamsubiri uwanjani Westfaelnstadion?

 Mholanzi huyo mwenye umri wa miaka 53 anachukua usukani kutoka kwa Thomas Tuchel, ambaye muda wake wa miaka miwili katika klabu ya BVB ulimalizika mwishoni mwa mwezi Mei kufuatia msururu wa matukio ya kutoelewana hadharani na wachezaji vigogo na usimamizi wa klabu hiyo.

Lakini licha ya mkwaruzano wa nje ya uwanja, msimu wa BVB wa 2016/2017 ulikuwa wenye mafanikio, kwa kupata tikiti ya moja kwa moja ya kucheza Champions League, wakashinda Kombe la Shirikisho la Ujerumani DFB Pokal na kutinga robo fainali ya Champions League. Chini ya Bosz watatarajiwa kuendelea kufanya vyema. DW inaangazia baadhi ya maswala ambayo Bosz atatarajiwa kuyashughulikia katika klabu yake mpya ya Dortmund.

Mustakabali wa Aubameyang

Bundesliga 34.Spieltag - Aubameyang und seine Torjägerkanone (picture alliance/dpa/B.Thissen)

Atabaki au ataondoka? Pierre-Emerick Aubameyang

Mfungaji wa mabao mengi katika Bundesliga Pierre-Emerick Aubameyang amesema wazi kuwa siku moja angetaka kuihama Borussia Dortmund na fununu zilipamba moto kuelekea mwishoni mwa msimu. Licha ya mchezaji huyo kuitaja mara kwa mara Real Madrid kuwa klabu angependa kuichezea, ripoti za karibuni kutoka Ufaransa zinadokeza kuwa Paris Saint-Germain imekubali mkataba wa euro milioni 70 kuipata saini ya Mgabon huyo, ripoti ambazo zilikanushwa haraka na Dortmund. Wakati kukiwa na Ousmane Dembelé, Christian Pulisic, André Schürrle, Shinji Kagawa na Marco Reus, pamoja na wachezaji wapya Mahmoud Dahoud, Dan-Axel Zagadou na Maximilian Philipp, hakuna uhaba wa ubunifu katika uwanja wa Westfalenstadion. Lakini kama Aubameyang ataondoka, Bosz atahitaji kutafuta mbinu ya kulijaza pengo la mchezaji anayeweza kufunga mabao 31 katika mashambulizi ya Dortmund.

Safu dhaifu ya ulinzi

Fußball Dortmund PK neuer Trainer Bosz (Reuters/W. Rattay)

Kocha mpya lazima aweke uhusiano mzuri na uongozi

Ijapokuwa ni timu tatu pekee za Bundesliga zilizofungwa idadi ndogo ya magoli kuliko Borussia Dortmund msimu uliopita, msimu wa vijana hao wa njano na nyeusi hata hivyo ulikumbwa na mapungufu katika safu ya ulinzi. Wakati Thomas Tuchel alikuwa akibadilisha kati ya mabeki wanne na mabeki watano na kushindwa kuamua safu imara ya ulinzi, Dortmund aghalabu walikuwa wakikunywa mabao.

Kwenye ligi, walifungwa mabao mawili au zaidi katika mechi kumi wakati katika Champions League, licha ya kuweka rekodi ya mabao mengi yaliyofungwa katika hatua ya makundi, bado walifungwa mabao manne katika mechi dhidi ya Legia Warsaw. Katika robo fainali, mabingwa wa Ufaransa Monaco waliwazaba mabao sita katika mikondo miwili.

Ajax ya Peter Bosz ilikuwa na safu imara kabisa ya ulinzi Uholanzi wakati walimaliza katika nafasi ya pili. Lakini walionyesha wasiwasi wa kufungwa hasa katika mechi za ugenini Ulaya.

Mvutano wa madaraka

Wingu kubwa linaloigubika Dortmund kufikia mwisho wa msimu lilitoka kwenye ofisi za uwanja wa Westfalenstadion, ambako viongozi na ubinafsi wao walikabiliana kwa miezi kadhaa. Mahusiano kati ya Tuchel na Hans-Joachim Watzke ulikuwa umeathirika tangu afisa huyo mkuu mtendaji alimuuza Mats Hummels, Ilkay Gundogan na Henrikh Mkhitaryan kinyume cha mapenzi ya kocha, kabla ya wawili hao kutofautiana hadharani baada ya shambulizi la basi ya timu hiyo.

Fußball borrussia Dortmund Tuchel und Watzke (imago/Martin Hoffmann)

Hans Joachim-Watzke alitofautiana na Tuchel

Kulikuwa na mvutano kikosini pia. Wachezaji chipukizi kama vile Dembele na Pulisic walielezea hadharani shukrani zao kwa Tuchel lakini wachezaji vigogo, wenye ushawishi mkubwa kikosini aghalabu waliziona mbinu za kiufundi za Tuchel kuwa ngumu sana na wakahoji ujuzi wake wa kibinafsi. 

Wakati Nuri Sahin aliondolewa kwenye kikosi cha fainali ya Kombe la Shirikisho la Ujerumani – DFB Pokal dakika ya mwisho mwisho, nahodha Marcel Schmelzer alihoji hadharani uamuzi wa kocha na wakaungwa mkono na mchezaji mwenza. Kama Bosz ataweza kuweka uhusiano mzuri na waajiri wake na wachezaji wake itajulikana karibuni, aliondoka Ajax kufuatia ukosefu mzozo kuhusu mbinu za kiufundi na timu yake ya kiufundi, akiwemo naibu wake Dennis Bergkamp.

Vijana

Umri wa wastani wa wachezaji wa kikosi cha kwanza cha Borussia Dortmund msimu uliopita ulikuwa miaka 25.2 – lakini kilikuwa karibu miaka mitatu zaidi ya umri wa wastani wa timu ya Ajaz aliyoiongoza Bosz iliyokuwa na miaka 22.4. Huku wachezaji kama vile Dembele (20), Pulisic (18), Julian Weigl (21), Raphael Guerrero (23) na Mathias Ginter (23) wote wakiwa wachezaji muhimu kikosini, Bosz hatakuwa na uhaba wa chipukizi wa kufanya kazi nao katika BVB. Sasa pia anahitaji kupata mchanganyiko mzuri kikosini kama uliowasaidia Feyenoord na Manchester United kuwazaba Ajax katika ligi kuu ya kandanda Uholanzi na Manchester United katika Europa League.

Mwandishi: Bruce Amani/DW
Mhariri: Iddi Sessanga

Matangazo

Unaweza kusikiliza matangazo yetu hapa

Kusikiliza matangazo ya Idhaa ya Kiswahili ya DW, tafadhali bonyeza alama ya spika ya masikioni hapo chini, na kuwasiliana nasi, tafadhali tuandikie moja kwa moja kupitia: kiswahili@dw.com