Nani ahakku wa kuunda serikali mjini Düsseldorf? | Magazetini | DW | 11.05.2010
 1. Inhalt
 2. Navigation
 3. Weitere Inhalte
 4. Metanavigation
 5. Suche
 6. Choose from 30 Languages

Magazetini

Nani ahakku wa kuunda serikali mjini Düsseldorf?

Karata zaanza kupigwa kumsaka ataka atakaeongoza serikali ya muungano ya jimbo la North Rhine Westphalia baada ya uchaguzi na kishindo chake kwa serikali kuu mjini Berlin

default

Nembo ya jimbo la North Rhine Westphalia

Karata zinaanza kuchanganywa ili kuunda serikali ya muungano mjini Düsseldorf na jinsi matokeo ya uchaguzi wa North Rhine Westfalia yanavyomlazimisha kansela Angela Merkel aweke kando mipango ya kupunguza kodi za mapato.Na juhudi za kuinusuru sarafu ya Euro ni miongoni mwa mada zilizochambuliwa na wahariri wa magazeti ya Ujerumani hii leo.

Tuanze lakini na juhudi za kuunda serikali ya muungano mjini Düsseldorf.Nani anastahiki kuunda serikali hiyo linajiuliza gazeti la "Main-Echo" la mjini Aschaffenburg na kuandika:

Hannelore Kraft anahisi yeye ndie ahakku wa kuunda serikali.Imekuaje?Muungano wa nyeusi na manjano waapiga kura wameupinga,lakini matokeo ya uchaguzi huo wa jimbo la North Rhine Westphalia hayakumpatia pia Hannelore Kraft uwezo wa kuwa waziri mkuu mjini Düsseldorf.SPD wameteleza na kujikingia asili mia 34.5-wako mbali na asili mia 37.1 walizojipatia mwaka 2005.Na wakati ule kiwango hicho kiliangaliwa kuwa ni cha chini kabisa kuwahi kushuhudiwa tangu mwaka 1958 .Isingekua vibaya kwa hivyo kama wanasiasa wangeutambua ukweli wa mambo.Au sivyo?

Gazeti la mjini Berlin "Berliner Zeitung" linajiuliza pia nani wanaweza kuunda serikali mjini Düsseldorf.Gazeti linaendelea kujiuliza.

Eti mazungumzo kati ya CDU na SPD yanaweza kupelekea kuundwa serikali ya muungano wa vyama vikuu.Jibu ni ndio-lakini kama Hannelore Kraft atakuwa waziri mkuu.Jee CDU wanaweza kufunika kawa na kumwachia bibi Kraft aongoze mustakbal wa jimbo hili?Jibu ni la.Kwasababu huo ungekuwa ushahidi kwamba jimbo la Nord Rhine Westphalia ni ngome imara ya wana Social Democratic ambako CDU walivumiliwa kwa muda tuu.Ushupavu huo ndio utakaopelekea kuundwa serikali ya muungano wa mrengo wa shoto-SPD-Die Linke na walinzi wa mazingira-Die Grüne na kuzipatia tija pande zote mbili.SPD kwasababu wataongoza serikali na CDU, kwasababu mtafaruku wowote utakaoitikisa serikali hiyo wataweza kuutumia katika kampeni za uchaguzi mkuu mwaka 2012.

Kampeni za uchaguzi wa mwaka 2012 zimeshaanza kuandaliwa tangu wakati huu,linaandika gazeti la "Westfällischer Anzeiger" la mjini Hamm,na kuendelea:

Hazijapita hata saa 24 baada ya pigo kubwa walilolipata washirika wa serikali ya muungano wa nyeusi na manjano jumapili iliyopita,kansela Angela Merkel amejitokeza na msimamo bayana kabisa kuwahi kushuhudiwa katika kipindi cha miezi sita iliyopita.Mipango ya kupunguza kodi za mapato inaachwa kando,angalao kwa sasa.Ni kauli thabiti hiyo ya kansela kwa wananchi,ikipambwa na onyo la uchungu kwa waliberali wasiokubali kuregeza kamba.Na huo ni mwanzo tuu,kwasababu kansela aonyesha hatimae kuuelewa ujumbe wa wananchi -hata kama amekawia kufanya hivyo."

Mada yetu ya mwisho magazetini inahusu juhudi za kuinusuru sarafu ya Euro.Gazeti la "Sächsische Zeitung" linaandika:

Nini kimekwenda kombo?Tangu mgogoro wa fedha wa kimataifa uliporipuka mwaka mmoja na nusu uliopita,wanasiasa wa Ujerumani na wa kimataifa hawakufanya vya kutosha kuwazuwia walanguzi.Zaidi ya hayo Umoja wa ulaya hawajanyanyua kidole kulalamika dhidi ya jinsi Ugiriki na nchi nyengine wanachama wanavyoshughulikia madeni yao.Yote hayo lazma yabadilike hivi sasa.La sivyo sarafu ya Euro haitakawia kudhoofika na akiba za wajerumani kujikuta zikipoteza dhamani.

Mwandishi: Hamidou Oummilkheir

Imepitiwa na: Abdul Rahman

 • Tarehe 11.05.2010
 • Mwandishi Oumilkher Hamidou
 • Chapisha Chapisha ukurasa huu
 • Kiungo https://p.dw.com/p/NLBC
 • Tarehe 11.05.2010
 • Mwandishi Oumilkher Hamidou
 • Chapisha Chapisha ukurasa huu
 • Kiungo https://p.dw.com/p/NLBC
Matangazo

Unaweza kusikiliza matangazo yetu hapa

Kusikiliza matangazo ya Idhaa ya Kiswahili ya DW, tafadhali bonyeza alama ya spika ya masikioni hapo chini, na kuwasiliana nasi, tafadhali tuandikie moja kwa moja kupitia: kiswahili@dw.com