Naibu Kansela wa Austria Heinz-Christian Strache ajiuzulu | Matukio ya Kisiasa | DW | 18.05.2019
  1. Inhalt
  2. Navigation
  3. Weitere Inhalte
  4. Metanavigation
  5. Suche
  6. Choose from 30 Languages
Matangazo

Matukio ya Kisiasa

Naibu Kansela wa Austria Heinz-Christian Strache ajiuzulu

Heinz-Christian Strache amejiuzulu kama naibu kansela wa Austria huku akikabiliwa na madai ya kashfa ya ufisadi. Strache amenaswa katika video akihonga mikataba ya biashara ili asiandikwe vibaya katika vyombo vya habari.

Kansela wa Austria Sebastian Kurz amekubali barua ya kujiuzulu ya Naibu Kansela Heinz-Christian Strache, baada ya kusambaa ukanda wa video unaomuonesha Strache akihonga mikataba ya serikali ili asiandikwe vibaya katika vyombo vya habari.

Katika taarifa aliyoitoa Jumamosi mchana akiwa ofisini kwake, Strache aliyeonekana kuwa na hasira amesema anajiuzulu ili kuzuia kuanguka kwa muungano unaotawala nchini Austria, lakini aliongeza kwamba amelengwa na kampeni yenye lengo la kuharibu jina na sifa yake.

"Mtu mmoja hapaswi kuwa sababu ya kufuta kabisa [kazi hii], na labda kutoa kisingizio cha kuvunja serikali hii, kwa sababu hiyo ndiyo lilikuwa lengo la hatua hii," alisema. "Hii ilikuwa ni njama ya kisiasa," aliongeza.

Chama cha kihafidhina cha Kurz cha Austrian People's Party (ÖVP) kinatawala kwa sasa nchini Austria katika serikali ya muungano na chama cha Strache cha siasa kali za mrengo wa kulia cha Freedom Party of Austria (FPÖ). Strache pia amejiuzulu kama mkuu wa chama hicho cha FPÖ, na kumkabidhi madaraka hayo naibu kiongozi na Waziri wa Usafiri wa Austria Norbert Hofer.

Baada ya Strache kujiuzulu, kansela wa Austria anaweza kuamua kuivunja serikali na kuitisha uchaguzi mpya, au kujaribu kuendelea na muungano uliopo na chama cha FPÖ chini ya kiongozi mpya.

Kuhonga vyombo vya habari

Strache amenaswa kwenye ukanda wa video unaomuonesha akitoa mikataba ya biashara ya serikali kwa mwanamke mmoja tajiri kutoka Urusi, ili amsaidie kukitangaza na kukijengea jina zuri chama chake cha FPÖ kupitia vyombo vya habari.

Video hiyo iliyonaswa katika kisiwa cha Ibiza nchini Uhispania Julai 2017, na kusambazwa Ijumaa jioni, imezua mgogoro ndani ya serikali ya Austria, huku vyama vya upinzani vikidai kuitishwe uchaguzi mpya.

Katika sehemu ya video hiyo iliochapishwa na magazeti ya Ujerumani ya Der Spiegel na Süddeutsche Zeitung, mwanamke anaejiita Alyona Makarova anasikika akimwambia Strache na kiongozi wa kikundi cha bunge cha FPÖ Johann Gudenus kwamba yeye ni tajiri mkubwa na anataka kumiliki asilimia 50 ya gazeti kubwa la Austria, la Kronen Zeitung.

Österreichs Vizekanzler Strache vor dem Aus

Kansela wa Austria Sebastia Kurz (Kkushoto) akiwa na Naibu Kansela Heinz-Christian Strache (Kulia)

Kulingana na Süddeutsche Zeitung, mkutano huo ulichukua masaa kadhaa, ambapo Strache na Gudenus (wake zao pia wakiwepo) walijadiliana na Makarova jinsi michango ya kifedha isiyo ya moja kwa moja inavyoweza kukisaidia chama hicho cha siasa kali za mrengo wa kulia kuandikwa vizuri katika vyombo vya habari.

Ukanda huo wa video ulirikodiwa miezi kadhaa kabla ya uchaguzi mkuu wa Austria wa Oktoba 2017, ambapo chama cha FPÖ kilipata aslimia 26 ya kura zote zilizopigwa na kuunda serikali ya muungano na Kansela Kurz.

Mikataba ya miundombinu na michango ya chama isiyo ya moja kwa moja

Makarova amesikika pia akidai kwamba amevutiwa na gazeti hilo ili aweze kukiandikia chama hicho cha FPÖ kabla ya uchaguzi. Strache na Gudenus walimueleza njia ambazo wafadhili matajiri wanazoweza kuzitumia kuificha michango yao kwa chama cha FPÖ na moja wapo ni kupitia mashirika yasiyo ya kiserikali.

Strache alimuambia Makarova iwapo watakubaliana, gazeti la Kronen litaweza kukisaidia pakubwa chama chake cha FPÖ na kukisogeza mbele katika uchaguzi ili kupata asilimia 34 ya kura badala ya 27. Strache pia alimuahidi njia tofauti za kumlipa mwanamke huyo, ikiwa ni pamoja na kumpatia mikataba ya ujenzi wa miondombinu ambayo kwa sasa inashughulikiwa na kampuni kubwa ya ujenzi Austria ya Strabag.

Wakiyajibu magazeti ya Der Spiegel na Süddeutsche Zeitung baada ya kuchapisha video hiyo, Strache na Gunenus wamesema wakati wa mazungumzo yao walisisitiza "umuhimu wa kuzingatia sheria za Austria," na kwamba walikuwa wakizungumzia uwezekano wa michango kwa chama cha FPÖ na mashirika yasiyo ya kiserikali.

Wanasiasa hao pia wamjitetea kwa kusema kwamba mazungumzo yao yalifanyika katika "mazingira ya starehe na yasiyo rasmi," na pia kulikuweko na tatizo la kutofahamiana lugha na kwamba hakukuweko mfasiri rasmi. Katika video hiyo, Gudenus anasikika akitafsiri Kirusi.

(dpa, Reuters, AFP)