Nagelsmann: Bayern haikutumia nafasi zake | Michezo | DW | 04.10.2021
  1. Inhalt
  2. Navigation
  3. Weitere Inhalte
  4. Metanavigation
  5. Suche
  6. Choose from 30 Languages
Matangazo

Michezo

Nagelsmann: Bayern haikutumia nafasi zake

Kocha wa Bayern Munich Julian Nagelsmann amesema vijana wake walishindwa magoli mawili kwa moja jana na Eintracht Frankfurt nyumbani kwao Allianz Arena kwa kuwa hawakuzitumia nafasi zao vyema.

Nagelsmann ambaye aliichukua mikoba ya kuinoa Bayern mwanzoni mwa msimu anasema kutoebuka na pointi tatu katika mechi ya Jumapili ni jambo linalomtia uchungu mwingi kwa kuwa ni mechi waliyostahili kuishinda.

Kwa sasa Bundesliga inakwenda mapumzikoni ila watakaporudi, mabingwa hao wana kazi nyengine kubwa ya kupambana na timu iliyoko katika nafasi ya pili Bayer Leverkusen uwanjani Bay Arena.

Borussia Dortmund wako katika nafasi ya tatu

Leverkusen kwa sasa wanaishikilia nafasi ya pili kwenye msimamo wa Bundesliga kutokana na uchache wa magoli waliyo nayo ila wote wako sawa kialama, wakiwa na pointi kumi na sita kila mmoja.

Borussia Dortmund kwa sasa nafasi wanayoishikilia ni ya tatu wakiwa pointi moja tu nyuma ya Leverkusen na Bayern Munich na katika mtanange ujao watakuwa wanakwaana na Mainz katika mechi ya mapema Jumamosi, kwa hiyo iwapo wataishinda mechi hiyo na Leverkusen na Bayern watoke sare huko Bay Arena basi watakuwa wamekwea hadi kileleni mwa jedwali la Bundesliga.

Fußball Bundesliga | Borussia Dortmund - FC Augsburg

Wachezaji wa Dortmund wakisherehekea goli dhidi ya Augsburg

Bayer Leverkusen wao waliendeleza mchezo wao wa kuridhisha msimu huu ambapo kufikia sasa wamefungwa mechi moja tu. Mwishoni mwa wiki waliwapepeta vibonde Arminia Bielefeld magoli 4-0 huku mshambuliaji wao mahiri Patrick Schick akicheka na wavu mara mbili halafu Moussa Diaby na Kerem Demirbay wakatia pilipili kwenye kidonda cha Bielefeld kwa kufunga hayo mengine mawili.