1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Tofauti za wazi zaibuka katika serikali ya Zuma

19 Oktoba 2016

Waziri Gordhan anayeheshimika nchini humo na ambaye alitarajiwa kustaafu kwa amani, sasa ndiye anaonekana kuwa mpinzani mkuu wa Rais Zuma, akisema mashtaka dhidi yake yamechochewa kisiasa.

https://p.dw.com/p/2RN3D
Südafrika Pretoria Präsident Zuma und Finanzminister Pravin Gordhan (R)
Picha: Imago/Gallo Images

Serikali ya Afrika Kusini imejitosa katika vita vya wazi huku tofauti kati ya Rais Jacob Zuma na waziri wake wa fedha ikifungua mabishano mapya yanayoweza kuitumbukiza nchi hiyo kwenye hali ya kukosa utulivu.

Shirika la uwekezaji la Afrika Kusini Oakbay sasa limedai kuwa kesi iliyowasilshwa mahakamani na waziri wa fedha wa nchi hiyo Pravin Gordhan iliyomhusisha rais Zuma na familia ya Gupta kwenye sakata ya ufisadi ilikuwa potovu.

Taarifa hiyo imejiri siku chache baada ya Gordhan kufichua mahakamani nyaraka za malipo ya dola milioni 496 kwa kampuni za Gupta zinazoongozwa na vijana wake watatu, ambao ni Ajay, Atul na Rajesh. Licha ya watatu hao kudaiwa kuwa na ushawishi mkubwa katika serikali ya Zuma, Zuma ameyakanusha.

Shirika hilo limesema kuwa habari katika nyaraka hizo za kurasa 72 zilizowasilishwa mahakamani na Gordhan si kweli.

Mabenki na makampuni kadhaa yamekatisha uhusiano na shirika la Oakbay bila kuweka wazi sababu zao.Chama kinachotawala cha African National Congress ANC kinaonekana kukumbwa na ugomvi mbaya huku uongozi wake ukikabiliwa na kufifia kwa uungwaji mkono, uchumi unaoyumba na vurugu kutokana na maandamano ya wanafunzi.

Waziri wa fedha Pravin Gordhan anayeheshimika nchini humo na ambaye alitarajiwa kustaafu kwa amani, sasa ndiye anaonekana kuwa mpinzani mkuu wa Rais Zuma.

Mwezi ujao, Gordhan mwenye umri wa miaka 67, anatarajiwa kufika mahakamani kuyajibu mashtaka anayosema yamechochewa kisiasa, kwa dhamira ya kumuondoa afisini baada ya kutofautiana na Zuma na madai yake ya washirika wa ufisadi wanaohusishwa na urais.

Waandamanaji mjini Johannesburg wanaotaka Zuma kujiuzulu
Waandamanaji mjini Johannesburg wanaotaka Zuma kujiuzuluPicha: Reuters/S. Sibeko

Lakini kisa cha Gordhan kimevutia baadhi ya wakuu serikalini kuwa upande wake, miongoni mwao ni Naibu Rais Cyril Ramaphosa na mawaziri kadhaa. Jumapili iliyopita, Ramaphosa aliandika kwamba "Ninamuunga mkono waziri Gordhan anapokabiliana na mashtaka dhidi yake”.

Mchambuzi wa kisiasa katika chuo kikuu cha Pretoria Prince Mashele amesema "watu katika ANC wameanza kuelewa ukubwa wa tatizo ambalo taifa limo ndani yake. Hawa si watu wa kawaida tu, bali wanachama waandamizi ambao sasa wamevunja uhusiano akiwemo Ramaphosa, hali ambayo nitasema kuwa tikisiko la ardhi kisiasa”

Mwezi Disemba mwaka jana rais Zuma japo shingo upande, alimteua Gordhan kuwa waziri wa fedha, kama njia ya kutafutia suluhisho sekta ya fedha iliyokuwa ikiyumba baada ya kuwafuta kazi mawaziri wawili wa fedha kwa kipindi cha siku nne. Awali, Gordhan alihudumu kama waziri wa fedha kati ya mwaka 2009 hadi 2014 ambapo alijizolea heshima.

Gordhan aliapa kutumia fursa hiyo kuufufua uchumi wa Afrika kusini kwa kudhibiti matumizi ya pesa, kuleta mageuzi kwenye kampuni za serikali zilizokuwa zikileta hasara na kukabiliana na ufisadi ulikithiri.

Lakini kazi yake ikamweka katika upinzani mkubwa na washirika wa rais Zuma mfano familia tajiri ya Gupta, ambayo inadaiwa kuwa na ushawishi mkubwa katika serikali ya Zuma.  

Wiki jana, Rais Zuma alifika mahakamani kutaka kuzuia kutolewa ripoti rasmi ya uchunguzi wa ufisadi kuhusu uhusiano wake na familia ya Gupta. Hali inayodaiwa kuchangia katika ukinzano wa kisiasa.

Tangu achukue urais, Zuma amenusurika visa kadhaa vya ufisadi dhidi yake, lakini hali hiyo imekighrimu chake chake ambacho kiliongoza vita vya ukombozi dhidi ya ubaguzi wa rangi, chini ya marehamu Nelson Mandela mwaka 1994.

Wabunge wa upinzani wakiondoka bungeni baada ya kiongozi wao alipoamriwa kuondoka bungeni wakati wa kumuuliza rais maswali
Wabunge wa upinzani wakiondoka bungeni baada ya kiongozi wao alipoamriwa kuondoka bungeni wakati wa kumuuliza rais maswaliPicha: Getty Images/AFP/D. Harrison

Mwezi machi Zuma alikabiliwa na kesi katika mahakama ya juu kwa tuhuma za kutumia vibaya pesa za umma kulikarabati boma lake kijijini, na pia anakabiliwa na kesi nyingine ya kupinga agizo la mahakama ambalo linaweza kurejesha kesi 800 za ufisadi dhidi yake.

Huku uchaguzi mkuu ukitarajiwa mwaka 2019, matokeo ya uchaguzi wa mitaa uliofanyika Agosti, yalionesha chama cha ANC kikifanya vibaya zaidi kuwahi tokea. ”Afrika Kusini ipo katika eneo la giza. Tumepoteza maadili na hadhi ya juu tuliyokuwa nayo". Mashele amesema.

Zuma ambaye bado anao wafuasi wengi katika ngome za ANC, anatarajiwa kuondoka madarakani mwaka 2019 baada ya kukamilisha mihula yake miwili. Wanaopigiwa upatu kupigania kiti hicho ni naibu wake Ramaphosa na aliyekuwa mke wake Nkosazana Dlamini-Zuma.

Ukuaji wa uchumi wa Afrika kusini ni sufuri mwaka huu. Ukosefu wa ajira unaendelea kuwa tatizo kwa asilimia 27 nayo ghadhabu za umma kutokana na ukosefu wa maendeleo tangu enzi za utawala wa ubaguzi wa rangi zimeishia kuzua vurugu kufuatia maandamano ya wanafunzi wa vyuo vikuu.

Susan Booysen ambaye ni mchambuzi wa kisasa kutoka chuo kikuu cha Witwatersrand ameliambia shirika la habari la AFP kuwa ”Mengi yameharibika kwa kuendelea kuwa na Zuma kama rais. Si ANC wala waafrika kusini ni washindi. Hatujawahi kushuhudia kiwango hiki cha mgawanyiko ndani ya ANC na serikali katika utawala wa Zuma. Ni nadra sana kwa mawaziri kuzungumza waziwazi”

Inaonekana kuwa Zuma ameshindwa kumfuta kazi Gordhan kwani akifanya hivyo itasababisha waekezaji wengi kujiondoa Afrika Kusini. Mchambuzi Ranjeni Munusamy na ambaye alikuwa mshauri wa rais huyo aliandika siku ya Jumatatu kuwa, hatua yoyote dhidi ya Gordhan huenda ikachochea mgogoro zaidi. Anakabiliwa na hatari ya kutengwa kwani wandani wake na maafisa wake wanamuunga mkono Gordhan”.

Mwandishi: John Juma/ AFPE

Mhariri: Gakuba Daniel