1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mzozo wa Ukraine Magazetini

3 Machi 2014

Mada moja tu imehodhi vichwa vya habari vya magazeti ya Ujerumani hii leo:Mgogoro wa Ukraine na kutumwa wanajeshi wa Urusi katika Ghuba ya Crimea.

https://p.dw.com/p/1BIY8
Maandamano mbele ya Ubalozi wa Urusi mjini BerlinPicha: picture-alliance/dpa

Wahariri wanazungumzia hofu zilizoenea barani Ulaya kutokana na kuzidi makali mzozo uliofikiriwa umemalizika wa Ukraine. Gazeti la "Rheinpfalz" linaandika:"Ndiyo kusema vita vinakurubia kuripuka Ulaya?Wiki moja iliyopita suala kama hilo lilikuwa muhali kulifikiria.Hii leo lakini kitisho cha kweli kimeibuka.Kilichobakia ni kutaraji tu kwamba wanadiplomasia watafanikiwa na kukubaliana kubuni haraka tume ya usimamizi na mkakati wa kisiasa ili kuituliza hali ya mambo.Putin anahoji hivyo ndivyo atakavyo-kwa hivyo siku zijazo zitadhihirisha kama kweli."

Gazeti la "Donaukurier" linajiuliza kuhusu hatima ya jimbo lenye utawala mkubwa wa ndani la Crimea na kuandika:"Yadhihirika kana kwamba hapatapita muda Crimea itageuka kuwa ya Urusi na pengine hata Ukraine ikagawika,sehemu ya magharibi ikatafuta kinga katika Umoja wa Ulaya na jumuia ya kujihami ya NATO na sehemu ya mashariki ya Ukraine ikaelemea Urusi.Mgawanyiko kama huo ni bora kuliko ugonvi wa daima,kama yanavyoonyesha maarifa yanayotokana na kugawanyika Jamhuri ya zamani ya Tchekoslovakia mwaka 1992 na kugeuka kuwa Jamhuri yaTcheki na Slovakia.Pengine huo ndio ufumbuzi ambao wakaazi wengi wa Crimea wangeutaka.

Putin afichua makucha yake

Gazeti la "Lausitzer Rundschau" linajiuliza kuhusu dhamiri halisi za rais wa Urusi Vladimir Putin.Gazeti linaendelea kuandika:"Kuepukana na utawala wa kiimla wa Janukowich tu ni kishindo hasa kutokana na uchungu uliosababishwa na idadi kubwa ya watu waliouwawa.Lakini ukosefu wa nia ya kufikia maridhiano katika nchi hiyo yenye mchanganyiko mkubwa wa jamii zenye tamaduni tofauti inafanya iwe muhali kuupatia ufumbuzi mzozo uliopo.Putin,kwa kutishia kuingilia kijeshi-wanajeshi kusema kweli wameshaanza kupelekwa,anaonyesha kutoijali jumuiya ya kimataifa.Na hali hii ni mpya katika siasa ya Urusi."

Ukraine Russland Konflikt Krim 1. März 2014
Vifaru vya kijeshi vya Urusi vimwekwa karibu na mpaka wa UkrainePicha: REUTERS

Gazeti la "Hannoversche Allgemeine " linaimulika siasa ya rais wa Urusi Vladimir Putin na kuandika:"Atafanikiwa vipi kuigeuza Urusi iwe ya kimambo leo ikiwa anazidi kuitenga?Putin anahitaji wananchi wenye kipaji kuyanusuru makampuni yaliyopitwa na wakati ya nchi yake.Na watu hao hao ambao ni muhimu kwa mustakbali wa Urusi ndio anaowapuuza.Uamuzi wake kuhusu Ukraine umezidi kulipanua pengo kati ya wenye kupigania hisia za kizalendo za Urusi na wale waliochoshwa na vita,watu wa tabaka ya kati wanaoishi mijini nchini Urusi.Jana tu vijana na wasomi wameonyesha wanaiangalia vipi siasa ya kupenda vita ya Putin.Kuanzia Moscow mpaka kufikia St.Petersburg watu wameteremka majiani kuandamana:Na kwa mara nyengine tena mamia wamekamatwa."

Mwandishi:Hamidou Oummilkheir/Inlandspresse

Mhariri: Mohammed Abdul-Rahman