1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Wapinzani wanakamatwa Uturuki

Othman, Miraji2 Julai 2008

Mvutano wa kisiasa ndani ya Uturuki unazidi kuwa mkubwa na wa hatari.

https://p.dw.com/p/EV2B
Waziri mkuu wa Uturuki, Recep Tayyip ErdoganPicha: AP

Wapinzani maarufu wa serekali wamekamatwa na inasemakana kutokana na kesi inayoendelea sasa mahakamani na ambayo inataka chama tawala cha AKP cha waziri mkuu Recep Tayyip Erdogan kipigwe marufuku. Zaidi kuhusu sakata hili, huyu hapa Othman Miraji...

Habari za kukamatwa wapinzani hao hapo jana zilienea kwa mlio mkubwa kama mpasuko wa bomu. Mjini Ankara, majenerali wawili wa wa zamani walio maarufu, mwandishi wa habari na kiongozi wa jumuiya ya wafanya biashara walitiwa ndani, wakituhumiwa kwamba ni wanachama wa jumuiya ya siri ya wazalendo vichwa ngumu. Mtandao wao, ambao unataka kuwa na Uturuki yenye mamlaka kama yale ya zamani, unasemekana ulipanga kuipinduwa serekali kwa kutumia nguvu. Licha ya hayo, madai yanaendelea kusema kwamba watu hao walikuwa nyuma ya kuuliwa padre wa Kitaliana pamoja na mwandishi wa habari wa Ki-Armenia, Hrant Dink. Inadaiwa pia kwamba kikundi hicho kilitaka kumuuwa mwandishi sanifu Orhan Pamuk na mwanasiasa wa kike wa Ki-Kurd, Leyla Zana.

Mwanzoni mwa mwaka huu mtandao huo ulichunguzwa, na darzeni tatu ya watu walikamatwa. Karibu na mji wa Istanbul kuligunduliwa ghala ya sialaha. Lakini wapinzani walio na siasa za kizalendo za vichwa ngumu wanasema kukamatwa watu hao kunafungamana na jaribio la serekali ya waziri mkuu Erdogan kuwafumba midomo wapinzani. Msemaji wa chama cha upinzani cha CHP alisema serekali imeanzisha utawala wa kuwatia hofu wananchi. Kiongozi wa upinzani, Deniz Baykal, amesema mtindo huo wa polisi unakumbusha uasi dhidi ya dola. Mwenyewe waziri mkuu Tayyip Erdogan amesema hao wanaoshukiwa watashtakiwa karibuni ili upatikane mwangaza kutoka kiza kilioko. Hao watu wanaoshukiwa wamekariri kutaka chama cha Haki na Maendeleo, AKP, cha waziri mkuu Edogan kipigwe marufuku. Operesheni ya sasa ya polisi imefanyika wakati mwendeshaji mkuu wa mashtaka wa Uturuki hapo juzi alitoa hoja zake mahakamani kutaka Chama cha AKP kipigwe marufuku. Alielezea tena kwanini anaona kwamba mfumo wa utawala wa Uturuki unaotaka dola na dini zitenganishwe unahatarishwa na waziri mkuu Erdogan na wafuasi wake.

Mwendesahji mkuu wa mashtaka alielekeza hasa hoja yake kwa ile nia ya serekali kutaka kuondosha amri ya kukataza wanawake kuvaa ushungi katika vyuo vikuu. Pia alitaja juu ya mafungamano baina ya duru za chama cha AKP na mtandao wa kigaidi wa al-Qaida, japokuwa hajatoa ushahidi thabiti. Alidai kwamba Chama cha AKP kinajaribu kuigeuza Uturuki kuwa nchi yenye kufuata itikadi za Kiislamu, hivyo akataka waziri mkuu Erdogan apigwe marufuku kuendesha shughuli za chama cha kisiasa kwa miaka mitano.

Leo Chama cha AKP kitatoa utetezi wake mbele ya mahakama ya kikatiba. Lakini wimbi hilo la kukamatwa wapinzani hapo jana limedhihirisha kwamba serekali imeamua kupambana na wapinzani wake.