1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mzozo wa Gesi baina ya Russia na Ukriane wazidi kupamba moto.

Eric Kalume Ponda5 Januari 2009

Athari za mzozo wa gesi baina ya Russia na Ukraine sasa zimeanza kushuhudiwa miongoni mwa mataifa yanayoitegemea sana Russia kwa bidhaa hiyo.

https://p.dw.com/p/GSR2
Bomba la gesi nchini Ukraine ambalo limekauka baada ya Russia kufunga mifereji yake.Picha: AP


Serikali hiyo ya Russia imepunguza kwa theluthi moja utoaji wa gesi kwa taifa la Ugiriki, Bulgaria na Croatia, na sasa mzozo huo ulioanza tarehe mosi mwezi huu kutokana tofauti zilizozuka baina ya mataifa hayo mawili kuhusu bei na deni linalodaiwa Ukraine, haonyeshi dalili ya kufika kikomo hivi karibuni, licha ya juhudi ya viongozi wa kanda hii kuushulughisha.


Hatua iliyochukuliwa na kampuni ya Gesi ya Gazprpom inayomilikiwa na serikali ya Russia, kufunga mifereji yake inayosafirisha gesi hadi nchini Ukraine, imezua hofu kubwa miongoni mwa mataifa yanayotegemea gesi kutoka Russia, na sasa mataifa hayo hasa miongoni mwa mataifa wanachama wa Umoja wa Ulaya, yameanza kutilia shaka kuhusu iwapo Russia ni taifa la kutegemewa katika utoaji wa gesi katika kanda hii.


Wajumbe kutoka mataifa wanachama wa Umoja wa Ulaya wanakutana leo mjini Brussels Ubeligiji kujadilia suala hilo, ili kuepusha kutokea tena hali iliyokumba mataifa haya miaka mitatu iliyopita.


Ingawa hadi sasa mataifa mengi ya Umoja wa Ulaya hayajaathirika, wadadisi wanasema kuwa hatua hiyo ni changamoto kubwa na tayari viongozi wa umoja huo wanatoa wito wa kutafutwa njia zingine za kupatia mahitaji ya gesi, ili kuepukana na vitisho vya mara kwa mara kutoka Russia.


Mzozo huo ulizuka tarehe mosi mwezi huu baada ya Russia kuishtumu Ukraine kwa kuiba gesi inayonuiwa mataifa ya Umoja wa Ulaya, mbali na kushindwa kwa Ukraine kulipa deni lake la muda mrefu.Kampuni hiyo ilidai kuwa Ukraine iliiba kiasi cha kiwango cha Cubic mita milioni 25 iliyokuwa imekusudiwa mataifa ya Umoja wa ulaya.


Mkuu wa, Alexei Miller anasema kuwa serikali ya Russia ililazimika kuongeza bei ya gesi kutokana na hasara inayopata kutokana na wizi huo.


Waziri mkuu wa Russia Vladimir Putin alitarajiwa kukutana na mkuu huyo wa kampuni ya Gazprom ingawa haijabainika mazungumzo hayo yatahusu nini na mwelekeo utakaochukuliwa na Russia kuhusu mzozo huo.



Wakati matokeo ya mkutano huo yanaposubiriwa kadhalika ujumbe mwengine wa mawaziri wa biashara kutoka jumuiya ya umoja wa ulaya umewasili nchini Ukraine kufanya mashauri na Rais Viktor Yuschenko katika juhudi za kutafuta njia ya kumaliza mzozo huo.


Ugiriki imesema kuwa Russia imepunguza kiwango kiwango cha gesi ilichokuwa ikiagiza kutoka Russia, ambapo sasa inapata Cubic mita millioni 4 kila siku ikilinganishwa na Cubic mita milioni sita inazohitaji.


Hali kadhalika kiwango hicho kimepungua jamhuri ya Croatian ambayo imekua ikiagiza asilimia 40 ya mahitaji yake ya gesi kutoka Russia. Matifa mengine yaliyoathirika na mzozo huo, ni pamoja na Uturuki, Hungary, Romania, Poland na Bukgaria.


Mkuu wa kampuni ya gesi nchini Bulgaria Dimitar Gogov alisema kuwa taifa hilo limekumbwa na upungufu wa Gesi ya kati ya kiwango cha asilimia 10 na 15 tangu kuanza kwa mzozo huo.


Ukraine inadai kuwa madai yanayotolewa na Russia hayana msingi, na huenda dhamira ya taifa hilo kutaka kuendelea uhasama wake dhidi ya taifa hilo tangu pale lilipotangaza kujiunga na shirika la NATO, hatua ambayo haikuifurahisha Russia.