1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mzozo wa Gaza- Ban Kii Moon azuru Gaza

Eric Kalume Ponda20 Januari 2009

Wanajeshi wa Israel wamesema kuwa wafuasi wa chama cha Hamas leo wamevumirisha roketi dhidi ya Israel , ikiwa ni siku tatu baada ya pande hizo mbili kutangaza hatua ya kusimamisha mapigano.

https://p.dw.com/p/Gcr3
Wakaazi wa Gaza walioachwa bila makao wakisubiri misaada ya binadamu.Picha: AP


Shambulio hilo limetokea wakati katibu mkuu wa Umoja wa mataifa Ban Kii Moon akizuru Ukanda wa Gaza kukadiria hali ilivyo katika eneo.


Jeshi la Israel limeonya vikali kuhusu tukio hilo linalolitaja kuwa ukiukaji wa tangazo la kusimamisha mapigano katika eneo la Ukanda wa Gaza.


Tukio hilo limezua hofu kubwa kwamba huenda Israel ikatekeleza ahadi yake ya kujibu shambulio lolote kutoka kwa upande wa Hamas wakati wa muda wa kusimamishwa mapigano.


Punde tu ving´ora vilipolia wanajeshi wa Israel ambao wamekuwa wakiondoka Gaza kwa tahadhari kubwa, walipinda mpango huo na kujiweka tayari kujibu shambulio lolote kutoka kwa Hamas.


Inadaiwa Kombora hilo lilianguka katika ardhi isiyo na maakaazi na kwamba hakuna majeruhi walioripotiwa.


Tukio hilo limeitia dosari ziara ya katibu mkuu wa Umoja wa mataifa Ban Kii Moon ambaye leo alitembelea makao ya mashirika ya Umoja wa mataifa mjini Gaza yaliyoshambuliwa na wanajeshi wa Israel wiki iliyopita.


Jamii ya kimataifa inaendelea kutoa wito wa kuchunguzwa kwa Israel kuhusiana na shambulizi lake dhidi ya makao hayo ya mashirika ya Umoja wa mataifa ambapo zaidi ya watu 40 waliuawa.


Ban Kii moon ndie afisa wa ngazi za juu wa kimataifa kulitembelea eneo hilo tangu chama cha Hamas kilipochukua uongozi wa Gaza mwaka 2007. Kadhalika katibu mkuu huyo alitarajiwa kuwa na mazungumzo na wanaharakati wa chama hicho cha Hamas.


Mashirika ya misaada ya binadamu yaliendelea na juhudi zake za kulepeka misaada kwa wakaazi wa eneo hilo la Gaza baada Israel kutoa hakikisho la usalama wao. Zaidi ya malori 500 yamekuwa yakiingia Gaza kila siku yakiwa yakisafirisha madawa, chakula misaada mingine.


Wakati huo huo maelfu ya wafuasi wa Hamas leo waliandamana katika mji wa Gaza uliobomolewa kwa kile walichokitaja kusherehekea ushindi dhidi ya uvamizi wa Israel.


Wafuasi hao walimiminika katika bustani iliyoko karibu na majengo ya bunge yaliyobomolewa huku wakibepa bendera ya Hamas na kutoa matamshi ya kukipongeza chama cha Hamas. Wafuasi hao walishtumu vikali serikali ya Israel na baadhi ya mataifa ya Kiarabu miongoni mwayo Misri na utawala wa rais Mahmud Abbas katika ukingo wa magharibi.


Maiti zaidi ziliendelea kufukuliwa katika vifusi vya majengo yaliyobomolewa wakati wa mashambulio hayo mjini Gaza, na kuifikisha idadi ya waliofariki kuwa watu 1,310. Zaidi ya watu 50,000 wameachwa bila makaazi kutokana na kuharibiwa kabisa makaazi yao na mapigano hayo yaliyoanza Disemba 27.